Prime
RIPOTI MAALUM -3: Njia za kuinua na kuendeleza michezo

Muktasari:
- Ukiweka kando mchezo wa mpira wa miguu ambao angalau tumekuwa tukijivunia hasa kwa mwaka 2024 kushuhudia timu zetu za taifa kufanya vizuri ikiwemo kufuzu michuano ya Afcon chini ya miaka 17, 20 na ile ya wakubwa upande wa wanaume na Wanawake, pia klabu za Simba na Yanga nazo zinaibeba nchi kimataifa upande wa klabu.
KUSUASUA kwa Tanzania katika mashindano ya kimataifa kunasababishwa na mambo mengi ikiwemo miundombinu mibovu ya kujifunzia, kukosa fedha za uendeshaji wa klabu za michezo sambamba na usimamizi duni wa viongozi waliopewa mamlaka kwa mujibu wa sheria.
Ukiweka kando mchezo wa mpira wa miguu ambao angalau tumekuwa tukijivunia hasa kwa mwaka 2024 kushuhudia timu zetu za taifa kufanya vizuri ikiwemo kufuzu michuano ya Afcon chini ya miaka 17, 20 na ile ya wakubwa upande wa wanaume na Wanawake, pia klabu za Simba na Yanga nazo zinaibeba nchi kimataifa upande wa klabu.
Msimu huu 2024-2025, Simba na Yanga zimecheza hatua ya makundi katika mashindano ya CAF, Simba imefanikiwa kupenya robo fainali, wakati Yanga ikiishia hatua ya makundi. Hata hivyo, bado nchi yetu ina nafasi ya kuingiza klabu nne kwenye mashindano ya msimamo ujao, ni nafasi inazopata nchi chache kila msimu na hiyo haiji kwa urahisi, bali ni kwa kuonyesha kiwango bora.
Wakati mpira wa miguu ukionyesha mwanga, michezo mingine bado inajikongoja.
Ili nchi ijivunie zaidi kupitia michezo mbalimbali katika kupasua anga, hakuna budi kufanya haya yafuatayo;
UWEKEZAJI KATIKA MIUNDOMBINU
Serikali inapaswa kuangalia uwezekano wa kutafuta wawekezaji ambao wataifanya miundombinu kuwa bora ili wanamichezo washiriki michezo katika hali nzuri lakini pia kujenga vituo vingi vya michezo hapa nchini.
Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha, amesema kwa mwaka huu Serikali itaanza na ujenzi wa kituo cha mafunzo cha michezo cha riadha katika Mkoa wa Manyara.

Katika hatua nyingine, suala la matengenezo ya viwanja, imeelezwa kwamba gharama za ujenzi wa bwawa la kuogelea lenye viwango vya Olimpiki si chini ya Sh1.9 bilioni.
Mei 24, 2022, Mbunge wa Makete, Festo Sanga katika vikao vya Bunge, alihoji Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho ya viwanja vya mpira wa miguu ambavyo hali yake si nzuri.
Sanga alihoji hivyo kufuatia mwaka mmoja nyuma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutoa maagizo kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kufanya marekebisho ya viwanja.
“Ni takribani mwaka mmoja sasa umeshapita tangu Rais atoe maelekezo kwenye wizara kufanya marekebisho ya viwanja nchini lakini hadi sasa hakuna kiwanja kilichofanyiwa marekebisho kupitia wizara, ni ipi kauli ya Serikali kwa sababu hali ya viwanja nchini ni mbaya na bado wanamichezo wanaendelea kuweka matumaini kwa Serikali.” Hiyo ilikuwa hoja ya Sanga aliyoitoa Mei 24, 2022.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul, alijibu kwa kusema: “Kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali kama ifuatavyo. Sisi kama wizara tunashirikiana na wadau mbalimbali kurekebisha viwanja, hivi ninavyoongea tunakamilisha maridhiano na Chama Cha Mapinduzi ambao wanamiliki viwanja nchi nzima kwenye mikoa vile viwanja vikubwa na tunategemea tutaanza ukarabati wa viwanja hivi na mwaka huu unaoanza tutaanza na viwanja saba zaidi ya bilioni 10 tumekwenda kutenga kwa ajili ya kukarabati hivi viwanja.”
Kwa kuonyesha hali ya viwanja si rafiki, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu akakazia kwa kusema: “Hivi viwanja navyo mnavyoruhusu TFF kuvichezea ligi na nyie mvifuatilie, jana (Mei 23, 2024) watu wameshindwa kucheza mpira vizuri Mwanza kutokana na viwanja vibaya.”
Hivi karibuni, Chama Cha Mapinduzi kinachomiliki viwanja zaidi ya 10 huku baadhi vikitumika kwa mechi za Ligi Kuu Bara ambavyo ni CCM Kirumba (Mwanza), Jamhuri (Dodoma), Ali Hassan Mwinyi (Tabora), Lake Tanganyika (Kigoma), Sokoine (Mbeya) na Liti (Singida), kimesema kinafikiria kuendeleza kuviendesha viwanja vyake au watafutwe wawekezaji kuifanya kazi hiyo.
Sababu ya kufikiria hilo ni kile kilichoelezwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla kwamba gharama za kuhudumia kiwanja katika mechi moja, inazidi kiwango cha fedha inayolipwa kwa mchezo mmoja.
Makalla aliyasema hayo Februari 21, 2025 katika mahojiano maalum na Gazeti la Mwananchi yaliyofanyika kwenye ofisi za gazeti hilo zilizopo Tabata jijini Dar es Salaam.
“Unatumia maji kumwagilia unaambiwa mechi itachezwa CCM Kirumba, bili ya maji ya kumwagilia uwanja na utaratibu uliowekwa na TFF unakuja kupewa fedha hazitoshi hata gharama za utunzaji wa uwanja,” amesema Makalla.
Kutokana na hilo, amesema ndio maana CCM inafikiria kuona iwapo inapaswa kuendelea kuviendesha viwanja au itafute wawekezaji wa kushirikiana na chama hicho kuviendesha.
“Ni mjadala lakini lengo ni kuhakikisha viwanja hivi vinaendelea kuwa katika viwango vizuri, lakini nikiri gharama za matunzo ya hivi viwanja ni kubwa mno kukiko mapato yanayopatikana,” amesema.
Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha, amesema Serikali imepanga kutoa maelekezo kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu zikiwemo Simba na Yanga kuwa na viwanja vyao vitakavyotumika kwa mechi za mashindano kwa sababu miundombinu ni uti wa mgongo wa michezo nchini.
kwa upande wa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, anasema: “Ni wajibu wetu kuhakikisha maeneo ya kuchezea yanakuwa bora na salama kwa wachezaji wetu. Serikali kwa sasa inachofanya ni kutekeleza miundombinu mbalimbali.
“Ukipita pale Benjamin Mkapa kwa nyuma utaona ujenzi ukiendelea wa kituo cha michezo na vinajengwa viwanja vya kisasa vya michezo mbalimbali.”
Kwa mujibu wa bajeti ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2024-2025, imetajwa kuwa na ongezeko kutoka Sh35.4 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023-2024 hadi Sh285.3 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024-2025.
Ongezeko hilo limetokana na uwepo wa michuano ya Chan 2025 na Afcon 2027 ambayo itafanyika nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda. Fedha za miradi ya maendeleo zimeongezeka kwa asilimia 2,082 kutoka Sh11.8 bilioni hadi Sh258.2 bilioni.
Fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa soka wa Arusha ni Sh125.2 bilioni. Uwanja huo kwa ajili ya fainali za Afcon, utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000, unajumuisha miundombinu ya eneo la kukimbilia riadha, uwanja wa ndani (Indoor stadium), viwanja vya mpira wa mikono, pete na netiboli.
Oktoba 17, 2024, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Prof. Madundo Mtambo kwenye kikao Cha Baraza hilo aliwashauri wajumbe wa kikao hicho kuendelea kutafuta maeneo ya kujenga miundombinu ya michezo sanjari na kuhamasisha viwanja vikiwemo vya shule viweze kuimarishwa ili kuhamasisha wadau kushiriki katika michezo kwa wingi.
UWEZO WA KITAALUMA
Kuwa na viongozi wa michezo wenye taaluma ya kile wanachokisimamia itasaidia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa michezo hapa nchini. BMT imelitambua hilo na mara kwa mara imekuwa ikitembelea mikoa mbalimbali kuendesha mafunzo.
Serikali nayo imesisitiza vyama kuwasilisha mipango yao juu ya makocha na waamuzi kisha kushirikiana nao ili kufanikisha kile kinachohitajika.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, amesema: “Serikali ipo tayari kuendelea kuvisaidia vyama vya michezo katika mafunzo ya makocha na waamuzi wetu ili kuwa na wataalamu wa kutosha wa kufundisha maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

“Nichukue nafasi hii pia kutoa rai kwa viongozi wote wa michezo nchini kuzingatia dhana ya uongozi bora ndani ya vyama vya michezo wawe wawazi, wawajibikaji pia wawashirikishe wadau wa michezo wanaowaongoza kwa maslahi ya michezo hapa nchini.
“Ninaamini kwa kuzingatia dhana ya uongozi bora katika michezo tutajenga taswira njema na wanachama na viongozi wetu wataepuka migogoro isiyo na tija wala ulazima ndani ya vyama vya michezo,” amesema kiongozi huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa BMT, Najaha Bakari, anasema: “Ifahamike kwamba kuna BMT ndani ya mkoa ambayo ni Kamati ya Michezo Mkoani na kila wilaya kuna Baraza la Michezo la Wilaya, ambapo kati ya hao ndio wale Katibu Tawala wa Mkoa na Wilaya ambao ndiyo wenyeviti wa kamati za michezo katika kila mkoa na wilaya.
“Lakini vilevile makatibu wao ni maafisa michezo katika sehemu hizo ingawa kwingine kuna maofisa utamaduni ambao ndio wanasimamia michezo.
“Baraza limeweka utaratibu kuzitembelea hizo kamati kuzikumbusha majukumu yao ni yapi kwa mujibu wa sheria ya Baraza la Michezo la Taifa ambayo ni kusimamia vyama vilivyopo katika ngazi yao na vilabu, maafisa michezo ndio wasajili wasaidizi licha ya kwamba wao ni makatibu ngazi ya wilaya lakini yeye ndiye msajili msaidizi wa chama cha mchezo.
“Kama maana hiyo taasisi yoyote ile inayotaka kujihusisha na mchezo wowote ikiwemo shule za michezo, hizo akademi, vilabu, vyama vyenyewe vya michezo lazima visajiliwe kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo.
“Kwa hiyo wakishasajili wanaleta ngazi ya taifa kwa msajili wa Baraza la Michezo la Taifa.”
KUONGEZA VYANZO VYA MAPATO
Oktoba 17, 2024, Mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Mkurugenzi wa (PPRA), Denis Kwambe Simba, wakati wa kikao cha Baraza la 15 la BMT, aliishauri sekretarieti ya Baraza kwa kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kujiimarisha zaidi pamoja na kuwapa mikakati ya mafanikio kwa wepesi.
Katika kutimiza ushauri huo, Ofisa Habari wa BMT, Najaha Bakari anasema ni muhimu kuwa na vyanzo vingi vya mapato ili kujiimarisha kiuchumi.
“Ada pekee za wanachama hazitoshi kufanya shughuli za maendeleo ya michezo, hivyo lazima tuwe na vyanzo vingi vya mapato ili kufanikisha jambo hili ambalo si rahisi, Baraza tuna dhamana hiyo na lazima tufanye juhudi kuhakikisha hakuna kinachoshindikana,” anasema Najaha.