Prime
Sakata la Kariakoo limetuonyesha Mahakama ya Michezo

Muktasari:
- Sakata la mechi hiyo lilitokana na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kuahirisha mechi hiyo ya Ligi Kuu kinyume cha kanuni baada ya Simba kutishia kutokwenda uwanjani Machi 8 kutokana na kuzuiwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi hiyo kama kanuni zinavyotaka.
SAKATA la kuahirishwa kiutata kwa mechi ya mzunguko wa pili baina ya Yanga na Simba limeibua udhaifu katika maeneo kadhaa ya uendeshaji ligi za soka, usimamizi, uwajibikaji na mfumo wa usuluhishi wa matatizo.
Sakata la mechi hiyo lilitokana na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi kuahirisha mechi hiyo ya Ligi Kuu kinyume cha kanuni baada ya Simba kutishia kutokwenda uwanjani Machi 8 kutokana na kuzuiwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi hiyo kama kanuni zinavyotaka.
Kanuni hazielezi kuwa timu ambayo itazuiwa kufanya mazoezi mepesi siku moja kabla, itakuwa na haki ya kulazimisha mchezo huo usogezwe mbele. Wala hazielezi kuwa watu wanaohusika kuizuia kufanya mazoezi, wachukuliwe hatua kwanza ndipo mechi ichezwe.
Ikijua hayo, kamati hiyo ya usimamizi ikaamua kuahirisha mechi kwa kutumia hoja ya dharura, ambayo nayo haikuwa na mashiko siku hiyo. Kamati ilidai iliona viashiria vya kuvunjika kwa amani na rushwa, lakini kisheria masuala hayo yanashughulikiwa na Jeshi la Polisi na Takukuru.

Kwa ufupi hakuna mkusanyiko wala mechi inayoweza kuchezwa kama Jeshi la Polisi haliwahakikishii waandaaji suala la amani. Kwa hiyo, kuahirishwa huko kulitakiwa kuambatane na ushahidi wa Jeshi la Polisi kuwa intelijensia yake imeonyesha ingekuwa hatari mechi kuchezwa.
Kwa hiyo hapo kuna dosari kubwa katika usimamizi na uendeshaji. Lakini dosari nyingine ni katika suala la utawala bora. Viongozi wakuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) ndio haohao viongozi wakuu wa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji na ndio haohao viongozi wa Kamati ya Uongozi wa TPLB. Maana yake hakuna vyombo tofauti vinavyoweza kusimamiana na kuwajibishana.
Lakini jinsi ya kutatua tatizo hilo pia imekuwa ni kitendawili kingine. Kutokana na Simba na Yanga kuwa na misimamo tofauti, mwenyekiti wa TPLB, Steven Mguto alikaririwa akisema kama watashindwa kutatua tatizo hilo watatumia hata viongozi wa serikali.
Maana yake ni kuwa hakuna vyombo imara vya usuluhishi wa migogoro ndani ya Shirikisho la Soka (TFF) wala katika nchi kwa ujumla. Na ndio maana tumeshuhudia wiki iliyopita Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Palamagamba Kabudi akiingilia kati kutaka kutatua mgogoro huo.

Kawaida, kama suluhisho litaiumiza TFF, ni lazima utasikia yale maneno ya serikali kuingilia kati, lakini iwapo suluhisho litaifurahisha basi hutasikia maneno hayo.
Baada ya Wakenya kuwa katika migogoro ya michezo kwa muda mrefu, waliona kuna umuhimu wa kufanya marekebisho ya sheria ya michezo mwaka 2013.
Marekebisho hayo ya sheria ya mwaka 2013 yaliunda Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (Sports Disputes Tribunal), ambayo inashughulikia migogoro yote inayohusiana na michezo katika vyama vya kitaifa vya michezo.
Kwa mujibu wa kifungu cha 55 kinachounda mahakama hiyo, mwenyekiti wa chombo hicho ni jaji aliyefuzu wa mahakama kuu na atakuwa na mawakili angalau wawili wa mahakama kuu wenye uzoefu wa angalau miaka saba na ambao wana uzoefu wa masuala la sheria za michezo na angalau watu wengine wawili na au wasiozidi sita ambao wamekuwa wakihusika katika michezo kwa nafasi yoyote.

Wajumbe hao wote wanatumikia nafasi zao kwa miaka tano na wanaweza kuteuliwa kwa miaka mingine mitano.
Kwa maana hiyo, chombo hicho kipo kisheria na vyama vinatakiwa viridhie masuala yao kupelekwa SDT na mahakama pia iridhie kusikiliza masuala yao.
Sheria hiyo inaruhusu rufaa dhidi ya uamuzi wake zipelekwe Mahakama ya Michezo ya Kimataifa (CAS).
Kwa hiyo, yale mambo ya kufikiri Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) na CAS ndio pekee wanaoweza kutatua migogoro ya michezo, yanakwisha. Ni lazima masuala hayo kwanza yaanzie ndani badala ya kwenda kuiabisha nchi huko nje.
Kwa muda mrefu, vyama vya michezo vimekuwa vikiandika katiba zinazofunga milango kwa walio nje kuingia ndani. Ukiangalia uchaguzi uliopita wa viongozi wa TFF, utaona dhahiri kuwa milango ilifungwa sana kwa wale waliotaka urais angalau kufika kwenye boksi la kura.

Mfano kanuni za uchaguzi zinataka mgombea apitishwe na angalau vyama vitano na vinaruhusiwa kumuidhinisha mgombea mmoja. Lakini mtetezi wa kiti cha urais aliidhinishwa na zaidi ya vyama 30, hivyo kuwanyima wengine fursa ya kufika kwenye boksi la kura. Hii ilitakiwa ipelekwe mahakama ya michezo ili ifute kifungu hicho na kuruhusu ushindani.
Tumeshuhudia jinsi mgogoro wa Simba na Yanga ulivyokosa chombo cha usuluhishi. Yanga wamesema wazi kuwa hawana imani na mwenyekiti na ofisa mtendaji mkuu wa TPLB. Lakini rais wa TFF, Wallace Karia akaibuka na kuwakaripia Yanga kwa tamko lao, akijua kabisa kuwa hakuna chombo kinachoweza kuwasikiliza Yanga na kutolea uamuzi shauri lao.
Na kwa jinsi muundo wa TFF ulivyo, hakuna chombo kinachoweza kusikiliza shauri lao na bodi ya ligi ilishafanya kosa la kuahirisha mechi, huku ikiwa inalaumiwa kwa maamuzi mengi ambayo wanaona ni ya upendeleo. Itawezaje tena kukutana na kusikiliza hoja za kuipinga?
Kwa hiyo, unaona umuhimu Wa kuwa na chombo nje ya TFF kwa ajili ya kusuluhisha au kutolea uamuzi masuala yanayoibuka katika vyama vya kitaifa au mashirikisho.
Na chombo hicho si kingine. Ni Mahakama ya Mashauri ya Michezo tu. Kwanza muundo wake unaondoa hisia za upendeleo. Jaji wa Mahakama Kuu ni mtu aliyejijengea heshima katika taaluma na jamii na hivyo hawezi kuruhusu jambo lolote limuondolee heshima na haiba hiyo. Hapa unazungumzia haki.

Akijua kuwa kuna mamlaka nyingine juu yake kutokana na chombo hicho kuundwa kisheria, itakuwa ngumu kwake kufanya upendeleo au kushawishi wajumbe waegamie upande wake, hasa kutokana na ukweli kwamba atakuwa na mawakili angalau wawili wa mahakama kuu.
Hata uteuzi wa wajumbe hao unafanya kisheria na si ule unaofanywa na rais wa chama cha mchezo ambao huweka uwezekano wa kusimika mtu anayempenda.
Zaidi ya hayo, wajumbe hao hula kiapo kuahidi kuwa watatenda haki kwa kipindi chote watakachokuwa wanatumikia chombo hicho.
Huu ni wakati wa kufikiria mbele zaidi ya kuridhika na utamaduni wa kutumia wanasiasa kumaliza migogoro ya kimichezo. Michezo kama mpira wa miguu, imeshajibiasharisha na hivyo inahitaji umakini zaidi ya mazoea katika kuuendesha na kuusimamia.
Na juu ya hayo yote, unahitaji mahakama inayoweza kutoa haki sawa ili biashara ijengewe mazingira mazuri ya kujiendesha.