Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA: Popote alipo Sir Alex Ferguson, pua nyekundu na hasira moyoni

BABU Pict

Muktasari:

  • Nadhani misuli midogo ya damu ya puani kwake ilikuwa inamsaliti pindi alipokuwa na hasira kali. Na pale Carrington kwenye Uwanja wa mazoezi wa Manchester United karibu kila mchezaji wake alikuwa amepitia makali ya ukali wake yaliyotambulika kama ‘Hair dryer treatment’.

WAZUNGU - Waingereza katika kilele chao cha ubora wa uchokozi walimuita Sir Alex Ferguson ‘Mr Red Nose’. Mscotland mwenye hasira kama alivyo, popote ambapo angekuwa amekasirika pua yake ilikuwa inageuka kuwa na rangi nyekundu.

Nadhani misuli midogo ya damu ya puani kwake ilikuwa inamsaliti pindi alipokuwa na hasira kali. Na pale Carrington kwenye Uwanja wa mazoezi wa Manchester United karibu kila mchezaji wake alikuwa amepitia makali ya ukali wake yaliyotambulika kama ‘Hair dryer treatment’.

Inadaiwa kuwa Paul Scholes ndiye mchezaji ambaye hakuwahi kufokewa na Sir Alex. Wengine? Kila mmoja alionja makali yake. Kina Ryan Giggs, Paul Ince, Brayan Robson, Roy Keane, David Beckham ndio kabisa alirushiwa kiatu na Sir Alex ambacho kilikwenda kumchana juu ya jicho lake.

Na sasa miaka 12 baada ya kustaafu kufundisha Manchester United na soka kwa ujumla, Sir Alex lazima atajikuta mtu mwenye hasira kali wikiendi hii. Hawezi kusema wazi, lakini moyo wake utakuwa unaugulia maumivu makali.

BA 01

Imekuwaje Liverpool wanaifikia Manchester United kwa mataji ya Ligi Kuu England? Sir Alex atakuwa anajiuliza hivi. Wakati Sir Alex akiingia Manchester United 1986, Liverpool walikuwa na mataji 16 wakati Manchester United ilikuwa na mataji saba.

Kitu alichojiapiza ni kuiondoa Liverpool katika kilele cha mataji ya Ligi Kuu pale England. Ilionekana ni mawazo ya kichaa. Na ilionekana Sir Alex alikuwa na mawazo ya kiendawazimu zaidi baada ya Liverpool kuongeza mataji mengine mawili 1988 na 1990.

Sir Alex alianza kazi hii ya kufikirika 1993 wakati alipoiwezesha Manchester United kupata taji lake la nane la Ligi Kuu England. Kuanzia hapo alitwaa mataji 13 ya Ligi Kuu England na kwenda kufikisha mataji 20 ya Ligi Kuu England 2013 wakati alipotangaza kustaafu kufundisha soka.

BA 02

Liverpool walikuwa wamesimama porini wasijue wanafanya nini na wanakwenda wapi. Walisimama na mataji 18 yaleyale kuanzia 1990 na Sir Alex alikuwa akipepea tu. Wakapitwa walipokuwa licha ya kutawala soka la England kwa miaka mingi. Walikaa miaka 30 bila ya taji.

Na sasa Sir Alex hajui ‘vichaa’ wanaopishana katika ofisi za Carrington huwa wanafanya nini hasa wanapokwenda kazini. Mwaka 2020 hatimaye baada ya miaka 30 Liverpool wakafanikiwa kuzipata fahamu zao na kutwaa taji la 19 la Ligi Kuu England.

Wengine tuliliita taji hilo kama taji la Covid. Wakati ule ugonjwa wa Uviko 19 ulipokuwa umeishambulia dunia na mechi zilichezwa bila watazamaji. Lakini sasa wamebakiza pointi moja tu ambayo wanaweza kuipata kiulaini dhidi ya Tottenham Hotspurs kesho pale Anfield na watatangazwa kuwa mabingwa.

BA 03

Sidhani kama watapata pointi moja, hapana, wataondoka na pointi zote tatu. Kwa namna ninavyowaona Tottenham wanavyocheza nadhani Liverpool wataondoka na pointi tatu. Baadaye watashangilia kwa nguvu na kwenda vyumbani. Baadaye watarudi tena uwanjani wakiwa na fulana zao zilizoandikwa 20 wakimaanisha mataji 20 ya Ligi Kuu England.

Nani amewaruhusu haya? Litakuwa swali la Sir Alex ambalo atakuwa amejiuliza moyoni. Labda Sir Alex anaamini kwamba kama angeendelea kuwa kocha wa Manchester United, basi si ajabu angeongeza mataji yake Old Trafford. Angeuweza mpira wa kisasa wa kina Pep Guardiola? Hilo ni swali jingine. Angeweza kuendelea kuifanya kazi hii kwa ufasaha katika hali yake ya umri huu? Hilo nalo ni swali jingine.

BA 04

Kuanzia pale alipostaafu hadi sasa Manchester United inahangaika tu kutengeneza timu ya maana. Kitu kibaya zaidi ni kwamba kwa sasa Liverpool ipo katika nafasi nzuri ya kuongeza mataji mengine ya Ligi Kuu England kuliko wao.

Ukiambiwa utabiri nani anaweza kuwa bingwa msimu ujao hauwezi kuiweka Manchester United.

Kichekesho ni kwamba hata ukiambiwa uiweke Manchester United ‘Top Four’ ya msimu ujao nayo pia utasita kuiweka mbele ya Liverpool, Arsenal, Manchester City na Chelsea. Hapa ndipo Manchester United ilipofikia.

BA 05

Kinachoweza kumuudhi zaidi Sir Alex ni ukweli kwamba kama utaangalia nani ametwaa mataji makubwa zaidi katika soka la Kiingereza basi Liverpool inaweza kuwa klabu yenye mafanikio zaidi katika soka la England kuliko Manchester United.

Kama utapima mafanikio katika Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, basi Liverpool itaibuka mbabe kwa sababu itakuwa imetwaa taji la England mara 20 kama Manchester United huku ikiwa imetwaa taji la Ulaya mara sita wakati Manchester United ikiwa imetwaa mara tatu.

Wakati haya yakiendelea bado hatujui Manchester United inaumwa ugonjwa gani. Makocha, wachezaji au wamiliki? Hatujui. Kila siku wanabadili makocha, lakini Manchester United imeendelea kuwa ileile tu.

Baada ya Sir Alex wamekuja David Moyes, Louis van Gaal, Jose Mourinho, Ole Gunnar Solskjaer, Erik Ten Hag na sasa Ruben Amorim, lakini Manchester United imeendelea kuumwa ugonjwa uleule. Mashabiki hawaelewi.

Kama ni manunuzi ya wachezaji basi familia ya Glazer imejitahidi vya kutosha kununua wachezaji wa bei mbaya, lakini kila siku tunachosikia kutoka Old Trafford ni maandamano tu ya kutaka wamiliki waondoke zao. Wameleta mmiliki mwingine wa kutia nguvu, lakini United imeendelea kuwa ileile tu.

Itakuwa wikiendi ya kihistoria pale Anfield, lakini kwa Sir Alex popote alipo itamuacha akiwa na sura nyekundu. Mambo mawili ambayo Sir Alex aliwahi kujiapiza yote yamekwenda kombo. La kwanza ni hili la kuifuta kabisa Liverpool pale juu katika orodha ya timu zilizotwaa mataji mengine Ligi Kuu England.

BA 06

Jambo la pili alilojiapiza ni kwamba hawezi kuiona Manchester City ambao ni watani wao wa jadi wa Jiji la Manchester wakitwaa taji lolote la Ligi Kuu England labda afe. Wakati huo Manchester City walikuwa hawajanunuliwa na matajiri wa mafuta kutoka Uarabuni.

Hakujua. Ghafla City wakanunuliwa na matajiri wa Abu Dhabi na kuanza kutwaa mataji ya Ligi Kuu England. Walipotwaa taji la kwanza la Ligi Kuu England baada ya kununuliwa na Waarabu mashabiki wa City walisikika wakisema ‘Rest in peace Ferguson’. Si alikuwa amewaambia hawawezi kutwaa taji hilo labda afe. Basi wakatengeneza mzaha kwamba Sir Alex amekufa ndio maana wamechukua.