Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mukandayisenga: Namba zinambeba Yanga princess

SENGA Pict

Muktasari:

  • Timu hiyo iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara ilisajili karibu kikosi kizima na dirisha dogo ikafanya maboresho ya wachezaji watano.

KAMA kuna wanachojivunia mashabiki wa Yanga Princess msimu huu basi ni usajili bora walioufanya kuanzia dirisha kubwa na lile dogo.

Timu hiyo iliyopo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara ilisajili karibu kikosi kizima na dirisha dogo ikafanya maboresho ya wachezaji watano.

Miongoni mwa wachezaji hao watano yupo mshambuliaji wa zamani wa Rayon Sports ya Rwanda, Jeaninne Mukandayisenga.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Yanga katika dirisha dogo akitokea nchini Rwanda na namba zinambeba akicheza mechi tano na kufunga mabao manane.

Msimu uliopita akiwa na Rayon aliibuka mfungaji bora akiweka kambani mabao 31 na msimu huu aliondoka Rwanda akiwa tayari ameweka kambani mabao 13.


MECHI TANO

Kwa sasa ndiye mshambuliaji tegemeo kwenye kikosi cha Yanga Princess akicheza mechi tano na kufunga mabao manane na asisti moja, wastani wa kuhusika katika mabao mawili kwa kila mchezo.

Mechi ya kwanza alifunga mabao mawili dhidi ya Alliance Girls, Yanga ikiondoka na ushindi wa mabao 4-0, kisha akafunga bao moja moka katika mechi dhidi ya Bunda Queens, Mashujaa Queens, Mlandizi Queens na Simba Queens na kuiwezesha timu hiyo ya wananchi kuondoa unyonge dhidi ya watani wao hao.

Mrwanda huyo amevunja rekodi ya washambuliaji wa timu hiyo akicheza mechi chache lakini amefunga mabao mengi.

Straika wa Yanga Princess, Ariet Udong hadi anaumia Desemba 31 alikuwa amecheza mechi nane za Ligi na kufunga mabao matatu yote dhidi ya Ceasiaa Queens ya Iringa.


KAZIBA PENGO

Nyota huyo alisajiliwa kuziba nafasi ya Udong ambaye alipata majeraha ya goti ambayo yamemuweka nje kwa takribani mwezi mmoja.

Lakini usajili huo ni kama umewalipa Yanga ambao walikuwa na wasiwasi kumkosa mshambuliaji wao hatari, Udong.

Udong ndiye alikuwa mshambuliaji tegemeo wa Yanga lakini baada ya kuumia nafasi hiyo alikuwa anacheza Neema Paul kabla ya Mukandayisenga kusajiliwa.

Neema ambaye ndiye kinara wa mabao kwa Yanga akifunga 12, ni winga mwenye uwezo, lakini baada ya Yanga kumkosa Mhabeshi huyo, kocha Edna Lema alifanya uamuzi wa kumbadilisha Neema na kumsogeza mbele acheze kama mshambuliaji wa mwisho.


CLARA, MASAKA

Pengine huu ndio usajili bora walioufanya Yanga msimu huu kwenye eneo la ushambuliaji kwa takribani misimu misimu mitatu sasa.

Aisha Masaka, Clara Luvanga ni miongoni mwa washambuliaji waliocheza kwa ubora Yanga Princess.

Msimu uliopita Clara alitimkia Dux Lugrono ya Hispania na miezi mitatu tu baadaye akauzwa Al Nassr ya Saudi Arabia anakowasha moto kwa msimu wa pili sasa.

Masaka baada ya kumaliza kinara wa ufungaji msimu 2020/21 akiweka kambani mabao 35, msimu uliofuata akatimkia BK Hacken ya Sweden na sasa yuko zake Brighton katika Ligi Kuu ya Wanawake ya England.

Nyota kama Janet Bundi kutoka Vihiga Queens, Cidalia Cuta (Msumbiji), Zayonce na Mburkinabe Madina Traore walipita kwa nyakati tofauti lakini walishindwa kuonyesha uwezo wa kutikisa nyavu kwa Watanzania hao.

Kwa mabao ya Mukandayisenga ndani ya muda mchache aliocheza Yanga huenda akavunja rekodi mbaya za hivi karibuni baada ya kuondoka kwa Masaka na Clara.


MSIKIE MWENYEWE

Akizungumzia kiwango chake Mukandayisenga, alisema kila anapopata nafasi anatamani kufunga na kuisaidia timu yake licha ya ugumu wa mechi wanazocheza.

“Kikubwa kusikiliza maelekezo ya kocha tu na nashukuru Mungu napata ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu hilo linanifanya kuwa bora ukichanganya na jitihada zangu binafsi,” alisema Mukandayisenga.


ILIPO YANGA PRINCESS

Timu hii ambayo haijawahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake, inashika nafasi ya tatu hivi sasa ikiwa na pointi 33 baada ya kucheza mechi 15, nyuma ya vinara JKT Queens yenye pointi 38 baada ya kucheza mechi 14, na Simba Queens iliyo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 37 baada ya kucheza mechi 14. Zimebaki mechi tatu msimu kumalizika, huku JKT na Simba Queens zikiwa na kiporo cha mechi moja moja.

Kinara wa mabao katika ligi hiyo ni Stumai Abdallah wa JKT mwenye mabao 26, akifuatiwa na Jentrix Shikangwa wa Simba Queens mwenye mabao 19, na Neema Paul wa Yanga mwenye 12.