Si mchezo… Simba ya kibabe walipo kwa sasa

Muktasari:
- Lipo kundi linalodai haijawahi kutokea Simba kali zaidi ya ile ya 1974 iliyofika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika).
HUKO mtaani kuna ka-ligi flani ka ubishi kanakoendelea miongoni mwa mashabiki na wapenzi wa soka hasa wale Simba. Ubishani huo unahusu kikosi bora cha muda wote cha Simba tangu klabu hiyo ilipoasisiwa 1936.
Lipo kundi linalodai haijawahi kutokea Simba kali zaidi ya ile ya 1974 iliyofika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika).
Kundi lingine linadai Simba kali ni ile ya 1979 iliyopindua meza kibabe katika michuano ya CAF kwa kushinda 5-0 ugenini huko Zambia baada ya awali kulala 4-0 nyumbani.
Lakini, kuna wengine wanasema Simba kali ni ile ya 1993 iliyofika fainali ya Kombe la CAF na kama sio uzembe flani, Mnyama angebeba taji hilo mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast iliyoshinda 2-0 baada ya mechi ya awali ugenini kuisha kwa suluhu.
Kadhalika lipo kundi lingine linakitaja kikosi cha 2003 kilichoivua taji Zamalek ya Misri na kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza tangu michuano hiyo ilipobadilishwa mfumo.
Mashabiki na wapenzi hao wamekuwa wakijadili Simba kwa mafanikio ya michuano ya kimataifa kwa rekodi zilizowekwa wakijaribu kulinganisha na vikosi Simba vya kina Patrick Aussems na Sven Vandanbroeck vilivyoweka rekodi kadhaa na kuvitetemesha vigogo vya soka Afrika.
Hata hivyo, kwa upande wa soka la ndani wapo wanaokitaja kikosi cha msimu wa 2009-2010 kuwa ndicho kikali zaidi kutokana na rekodi kiliyoandikisha kwa kucheza mechi za msimu mzima wa Ligi Kuu Bara bila kupoteza mchezo.
Simba ilitwaa ubingwa kwa kucheza mechi 22, ikishinda michezo 20 na sare mbili dhidi ya Kagera Sugar na African Lyon, huku ikifunga mabao 50 na kufungwa 12 ikivuna pointi 62.
Kama hujui, Simba hiyo ilikuwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti Hassan Dalali, Omar Gumbo (makamu mwenyekiti), Mwina Kagududa (katibu mkuu), Mohammed Mjengwa (katibu msaidizi), Ally Hassan (mhazini) na msaidizi wake akiwa ni Chano Almasi ilhali Katibu Mwenezi akiwa ni Said ‘Seydou’ Rubeya.
Msimu huo Simba pia ilitoa Mfungaji Bora akiwa ni Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyemaliza akiwa na mabao 18 na kuiwezesha timu hiyo kuinyang’anya Yanga ubingwa mapema kabla msimu haujaisha.
Licha ya rekodi hiyo ilifikiwa na Azam FC msimu wa 2013-2014 na Yanga kuja kuivunja msimu wa 2021-2022 ikicheza mechi nyingi zaidi (30) kulinganisha na wenzao, yaani Simba (22) na Azam (26), bado Simba inatambia kuwa waasisi wa kucheza mechi nyingi bila kupoteza mbali kubeba ubingwa ikiwa na mechi mbili mkononi msimu huo.
Yanga ilibeba pia ubingwa kwani katika mechi 30 ilishinda 22 na sare nane ikivuna pointi 74, wakati Azam katika mechi 26 ilishinda 18 na kutoka sare nane ikivuna pointi 62 ikifunga mabao 51 na kufungwa 15.
Kwa wanaokumbuka ni kwamba Simba ya kibabe ilijihakikishia ubingwa kwa kuicharaza Azam mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa Machi 14, 2010 kwenye Uwanja wa Uhuru (zamani Uwanja wa Taifa) kwa mabao ya Mkenya Mike Baraza, huku ikiwa na michezo miwili mkononi ukiwamo dhidi ya Mtibwa Sugar iliyowanyoa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Mabao yalifungwa na Mgosi mawili, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ na Mohammed Kijuso kila mmoja akifunga moja.
Mchezo mwingine iliokuwa nao mkononi ni ule wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga uliopigwa Aprili 18, 2010 na Simba kushinda 4-3 na kuzinogesha sherehe za ubingwa kupitia mabao ya Uhuru Seleman, Mgosi aliyefunga mawili na lile la ushindi likifungwa ‘jiooni’ na Mkenya Hillary Echesa.
Katika mechi hiyo, Yanga ilionekana kama ingetoka sare ya 3-3 kwa mabao ya Athumani Idd na mawili ya Jerry Tegete likiwamo la dakika ya 89 kabla Echesa kuwatibulia dakika za majeruhi.
Mechi hiyo ilipigwa kabla ya ile ya Mtibwa iliyofunga pazia la msimu na Mgosi kutwaa Kiatu cha Dhahabu. Mashabiki wanakitaja kikosi cha msimu huo wa 2009-2010 ndicho kilikuwa kikali zaidi kwa kuandika rekodi ya kubeba taji la Ligi Kuu Bara bila kupoteza chini ya Mzambia Patrick Phiri.
Vikosi vilivyocheza pambano hilo la kihistoria vilipangwa hivi; SIMBA: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Mohammed Banka, Hillary Echesa, Ramadhan Chombo, Mussa Hassan, Michael Baraza/ Mohammed Kijuso, Ulimboka Mwakingwe/ Uhuru Seleman
AZAM: Vladimir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Malika Ndeule/Maulid Bofu, Tumba Sued, Salum Sued, Himid Mao, Dan Wagaluka/Ally Manzi, Salum Abubakar, John Bocco, Shaaban Kisiga, Said Sued/Suleiman Kassim
Mwanaspoti linawakumbushia walipo kwa sasa nyota wa Simba waliocheza mechi hiyo iliyowahakikishia ubingwa na kuweka rekodi iliyodumu kwa misimu minne kabla ya kufikiwa na Azam 2013-2014 kisha Yanga 2021-2022.

JUMA KASEJA
Huyu ndiye aliyekuwa kipa namba moja wa kikosi hicho na alikuwa langoni wakati Azam ikiwabariki kubeba ubingwa.
Kwa msimu huo, Kaseja aliwakalisha benchi Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’.
Kumbuka, Kaseja alikuwa amerejea Msimbazi kutoka Jangwani alikosajiliwa na kutumiwa msimu mmoja, alikuwa nguzo na mhimili imara wa Simba kubeba taji bila kupoteza mchezo.
Kwa sasa Kaseja ni kocha wa Kagera Sugar baada ya kustaafu 2022 huku akiwahi kuzitumikia timu tofauti kama kipa na kocha vilevile zikiwamo Mtibwa Sugar, Moro United, Mbeya City, KMC na Kagera Sugar.

HARUNA SHAMTE
Huyu ndiye aliyekuwa beki wa kulia wa Simba wakati ikitangaza mapema ubingwa. Beki huyo ambaye bado anaendelea kukipiga katika Ligi Kuu Bara, kipindi hicho alikuwa akipokezana kucheza na Salum Kanoni.
Shamte maarufu kama Terminator anaendelea kukiwasha kama kawaida licha ya kutokuwa na makali kama ilivyokuwa enzi zake na mara ya mwisho msimu uliopita alikuwa Mtibwa Sugar ilyomsajili kutoka Namungo. Mbali na Simba, Terminator amezitumikia Lipuli FC, Mbeya City, Ruvu Shooting na Villa Squad.

JUMA JABU
Beki wa kushoto aliyewazima mawinga hatari wa Azam katika pambano hilo na ndiye aliyesimama kama beki namba tatu.
Jabu aliyeanza kucheza soka tangu akiwa shule akikipiga Kagera Rangers ya Magomeni Mwembechai kabla ya kuibukia Ashanti United na baadae Simba, ndiye aliyekuwa beki tegemeo wa kushoto msimu huo akisaidiwa wakati flani na Mganda Joseph Owino aliyekuwa akimudu pia kucheza kama beki wa kati.
Kwa sasa Jabu amestaafu soka la ushindani na alijikita zaidi katika masomo.

JUMA NYOSSO
Beki huyo aliyekuwa akiogopeka kwa aina ya uchezaji wake, ndiye aliyecheza namba nne katika mchezo ambao Azam ililala 2-0.
Nyosso aliyekuwa akisifika kucheza kibabe na mgumu kupitika alikuwa akibadilishana namba na David Naftari. Kwa sasa beki huyo amestaafu baada ya kuzitumikia klabu mbalimbali ikiwamo Ashanti United, Mbeya City, Geita Gold na nyingine.

KELVIN YONDANI
Beki mwingine mtemi na ndiye aliyesimama kama namba tano wakati Azam ikifa, lakini katika msimu huo alikuwa akisimama kati akipokezana na kina Owino, Naftari na Nyosso na kuifanya Simba kuwa na mabeki wa kati wa kibabe walioifanya iruhusu idadi ndogo ya mabao (12) katika mechi hizo 22. Kwa sasa Yondani anakipiga KenGold baada ya kuzichezea Yanga, Polisi Tanzania na Geita Gold.

MOHAMMED BANKA
Kiungo fundi wa mpira aliyesimama kama kiungo mkabaji katika pambano hilo na aliwazima mastaa wa Azam wakiongozwa na Himid Mao ‘Ninja’ aliyepo Misri kwa sasa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ anayekipiga Yanga, mbali na Shaaban Kisiga ‘Malone’.
Banka aliyewahi pia kukipiga Yanga kwa sasa amestaafu soka, lakini ameacha alama katika soka la Tanzania kwa aina ya uchezaji wake wa akili na maarifa.
Mbali na kucheza Simba na Yanga, pia aliwahi kuzitumikia Moro United, Bandari Kenya, Coastal Union na Mwadui (sasa BigMan) na Friends Rangers pamoja na timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

HILLARY ECHESA
Kiungo huyo mshambuliaji Mkenya katika mchezo huo ndiye aliyeanza kuitia doa Azam kwa kumtengenezea Mike Baraza bao la kwanza dakika ya nane kwa kupiga krosi iliyomaliziwa wavuni na mfungaji kwa kichwa.
Echesa alikuwa na msimu mzuri akiwa na kikosi hicho kilichomsajili kutoka Indonesia alikokuwa akiitumikia timu ya Ligi Daraja la Pili ya Deltras, kwani mbali na kuisaidia Simba kuizima Azam na kubeba ubingwa mapema, aliinyamazisha Yanga katika mechi iliyofuata kwa kufunga bao la ushindi dakika za jioni, siku mnyama aliposhinda Dabi ya Kariakoo kwa mabao 4-3 na kuunogesha ubingwa akimtungua kipa Obren Curkovic kwa shuti la umbali wa mita 25 na kuwaduwaza matajiri wa Chamazi.
Kama hujui ni kwamba kiungo huyo aliwahi pia kukipiga Yanga kabla ya kuitumikia Simba, mbali na timu nyingine kama Rayon Sports, Tusker, Chemelil na Sofapaka.
Echessa alistaafu 2018 ikielezwa kwa sasa anajishughulisha na uchambuzi wa soka na kibiashara.

RAMADHAN CHOMBO
Mashabiki wa soka walimfananisha na kiungo wa zamani wa Argentina aliyewahi kuwika Real Madrid na AC Milan, Fernando Redondo. Katika mechi hiyo alisimama kama kiungo mshambuliaji sambamba na Kisiga.
Redondo ambaye alianza kutamba kupitia timu ya Tambaza kabla ya kwenda Sweden na baadae Asanti United na kuonwa na Simba alikuwa na msimu mzuri na kikosi hicho kabla ya kutua Azam mmoja baadae kisha kurudi Msimbazi.
Kwa sasa Redondo ameachana na soka la ushindani, lakini akiwa amewahi kuzitumikia Biashara United, Mbeya City, Geita Gold na African Lyon mbali na kuitumikia timu ya taifa.

MUSSA HASSAN
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa zamani wa Tanzania katika msimu huo alikiwasha na kuwakimbiza mastaa wengine wazawa na wa kigeni kwa kuibuka Mfungaji Bora alipofunga mabao 18.
Katika mchezo huo, Mgosi alipoteza nafasi kadhaa za wazi, huku akiwanyima raha mabeki wa kati wa Azam, Tumba Swedi ‘Kiwi’ na Salum Swedi ‘Kussi’ waliocheza pamoja kama wanandugu katika mchezo huo.
Mgosi alikuja kumalizia hasira katika Dabi ya Kariakoo, mchezo uliofuata kwa kufunga mara mbili wakati Yanga ikifa mabao 4-3 na kumalizia na mawili mengine wakiizamisha Mtibwa ikiwa nyumbani na kufunga hesabu na mabao 18.
Kwa sasa Mgosi ni kocha msaidizi wa timu ya soka ya wanawake ya Simba Queens, akiwa amewahi kuzitumikia pia JKT Ruvu, Mtibwa Sugar na Motema Pembe ya DRC.
MICHAEL BARAZA
Mshambuliaji mkongwe kutoka Kenya kipindi hicho aliyefupishwa jina na kuitwa Mike Baraza, ndiye aliyekuwa mwiba kwa Azam katika mchezo huo kwa kufunga mabao yote mawili, likiwamo la kwanza la dakika ya nane na lile la dakika ya 61.
Kama ilivyokuwa kwa Echessa, mshambuliaji huyo alikuwa msumbufu kwa chenga na uwezo wa kumiliki mpira na kuwatoka mabeki, na jinsi anavyojipanga katika eneo zuri la kuwaliza makipa.
Baraza alistaafu 2016 na sasa inaelezwa anaendelea na mishe zake nyingine kwao Kenya, lakini akiwa ameacha alama Msimbazi kwa kuipa ubingwa wa aina yake msimu wa 2009-2010. Kumbuka huo ulikuwa ni mchezo wa pili kwa Mkenya huyo kuanza kikosi cha kwanza na kufanya yake kabla a kutolewa kumpisha Mohammed Kijuso. Baadae alisajiliwa na Azam.

ULIMBOKA MWAKINGWE
Winga teleza wa kushoto kama ilivyokuwa kawaida yake alishirikiana na wenzake akiwamo Mgosi, Echessa na Baraza kuwapelekea moto mabeki wa pembeni wa Azam kina Ibrahim Shikanda na Malika Ndeule na wale wa kati.
Licha ya kwamba hakufunga, lakini kasi na chenga zake ziliwanyima raha mabeki wa Azam waliokuwa wakilindwa na kipa Mrundi Vladimir Niyonkuru.
Kwa sasa Ulimboka amestaafu soka na kugeukia ukocha akizinoa timu kadhaa ikiwamo Pamba Jiji na Kitayosce (sasa Tabora United) kabla ya kukumbwa na adhabu ya kufungiwa maisha kwa kosa la upangaji wa matokeo ya mechi za Ligi ya Championship kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Katika mchezo huo wa dhidi ya Azam, Ulimboka alitolewa kipindi cha pili kama ilivyokuwa kwa Mike Baraza na kumpisha Uhuru Seleman, mshambuliaji mwingine aliyekiwasha vilivyo msimu huo akiwa na Wekundu wa Msimbazi.
Kabla ya kutua Simba 2002 na kuitumikia hadi 2012 ikiwa ni misimu 10 mfululizo, Ulimboka aliichezea Reli Kigoma na alipoondoka Msimbazi alipita kidogo Majimaji Songea kisha kugeukia ukocha hadi alipokumbwa na rungu.

PATRICK PHIRI
Huyu ndiye aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho kilichoandika rekodi ya kubeba ubingwa msimu huo bila kupoteza. Kocha huyo Mzambia kwa sasa hana timu baada ya kuaachana na Lumwana Radiants iliyopo Ligi Kuu ya Zambia, lakini aliwahi kurejea tena Msimbazi msimu wa 2014-2015 ikiwa ni mara ya tatu kwake, kwani mara ya kwanza aliinoa msimu wa 2003-2005.
Hata hivyo, mara hii ya tatu hakuwa na maajabu, ila bado anakumbukwa Msimbazi kwa heshima kubwa aliyoiweka mwaka 2010 kwa kuipa Simba taji la 16 la Bara.