Prime
SIO ZENGWE: TFF, DRFA zionyeshe uongozi mgogoro TEFA

Muktasari:
- Hii ni kwa sababu uongozi wa soka mkoani Dar es Salaam, DRFA na ule wa kitaifa, TFF, umeshindwa kuonyesha uongozi katika kumaliza mgogoro huo unaoelekea mwaka wa pili sasa, hii ikiwa ni pamoja na kutoa mwongozo na kuchukua hatua stahiki katika kutafuta suluhisho na kuruhusu mpira wa miguu wilayani Temeke uchezwe kwa utulivu.
NI rahisi sana kupotoshwa kuhusu mgogoro wa uongozi unaoendelea katika Chama cha Soka cha Wilaya ya Temeke (Tefa) ambako kwa sasa kuna makundi mawili ya viongozi tangu kufariki kwa mwenyekiti wa zamani, Peter Mhinzi.
Hii ni kwa sababu uongozi wa soka mkoani Dar es Salaam, DRFA na ule wa kitaifa, TFF, umeshindwa kuonyesha uongozi katika kumaliza mgogoro huo unaoelekea mwaka wa pili sasa, hii ikiwa ni pamoja na kutoa mwongozo na kuchukua hatua stahiki katika kutafuta suluhisho na kuruhusu mpira wa miguu wilayani Temeke uchezwe kwa utulivu.
Binafsi nilishangaa kwamba Kamati ya Maadili ya TFF kutaka kumchukulia hatua kiongozi wa zamani wa Tefa kwa kuwa ni mamlaka mbili tofauti zilizo katika ngazi tofauti na zinazotegemeana katika uamuzi, yaani uamuzi wa kwanza na baadaye rufaa.
Na bado nashangaa kwa sababu walioitwa na kudaiwa kushiriki uchaguzi usio halali, bado wanatakiwa waadhibiwe na mamlaka za eneo lao, yaani wilayani na baadaye mkoani ambako rufaa yao ingesikilizwa kama wangepinga uamuzi wa awali.
Mimi naamini ndio utaratibu sahihi. Lakini ukiambiwa eti katika ngazi ya mkoa hakuna kamati ya maadili wala nidhamu ndio maana shauri hilo limefika Kamati ya Maadili ya TFF, unashikwa na butwaa zaidi. Uchaguzi wa viongozi wa DRFA ulimalizika lini hadi imekuwa shida kwa viongozi kuunda vyombo vyake vya haki hadi leo? Na kama havipo DRFA imefanya nini kuhusu sakata la Tefa?

Ni kweli, kwa mtu wa nje kuambiwa kuwa uongozi unaotambulika sasa wa Tefa, ukiongozwa na Ali Kamtande ulichaguliwa na wapigakura 12 kati ya zaidi ya 100 waliojiandikisha, ni kitu cha kuchekesha, lakini habari kwamba ilikuwaje, inafikirisha na hairuhusu kucheka hata kidogo.
Wajumbe zaidi ya 100 walijiandikisha kupiga kura na katika chumba cha uchaguzi wengi waliamua kumzomea mgombea pekee aliyepitishwa, huku hao 12 tu wakishiriki kupiga kura. Kama kanuni za uchaguzi zingekuwa zinalazimisha mgombea lazima apate asilimia 50+ ya kura, ingeeleweka kuwa mgombea pekee hatakiwi kuidhinishwa.
Lakini kamati ya uchaguzi ikampitisha kuwa ndiye mshindi na hivyo kurithi mikoba ya Mhinzi. Bado uongozi huu haujapata ushirikiano wa kutosha kutoka mamlaka za juu za soka katika ngazi ya mkoa na taifa. Kwa hiyo, hapo unaona tatizo jingine la kiuongozi.
Awali, uchaguzi wa Tefa uliopangwa kufanyika Agosti 2, 2024 ulizuiwa na Mahakama Kuu baada ya Jaji Obadia Bwegoge kukubali ombi la zuio la muda lililowasilishwa na wanachama wa Tefa ambao ni Lawrence Kimea, Mwinjuma Kondo na Twaha Uwesu ambao walifungua kesi dhidi ya Kamtande, Bodi ya Udhamini ya Tefa na Kamati ya Uchaguzi ya Tefa.

Moja ya hoja zao ilikuwa ni kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo kwa kutumia katiba mpya ambayo ilikuwa na mabadiliko ya sifa za wagombea, ambazo ni pamoja na kiwango cha elimu kwa wagombea kuwa elimu ya sekondari. Hata hivyo, shauri hilo lilitupwa na mahakama kwa hoja kwamba masuala ya mpira wa miguu yana vyombo vyake vya uamuzi ambavyo ni lazima kwanza vifanye uamuzi ndipo shauri liwasilishwe katika mahakama ya kiraia.
Suala la shughuli za Tefa kwenda mahakamani limekuwa la kawaida na huoni mamlaka za juu zikichukua hatua za kiuongozi kulitatua kiasi kwamba baadhi ya viongozi wa juu wa TFF sasa wanatuhumiwa kuhusika katika mgogoro huo.
Mbali na mahakamani, masuala ya uchaguzi Temeke yameshafika hadi serikalini ambako Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lililazimika kuzuia uchaguzi huko nyuma. Na hata DRFA imeshawahi kutangaza kutotambua viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho enzi za Mhinzi.
Mgogoro ni wa muda mrefu kuanzia kama mwaka 2015, lakini hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa kuumaliza, zaidi ya vyombo vya habari kutoa taarifa ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiegemea upande mmoja.

Kuna hatua za kisheria na za kikanuni zinazotakiwa zichukuliwe kumaliza mgogoro huo, lakini ni lazima juhudi zifanyike kwanza kutafuta chanzo ni nini na hatimaye makubaliano yafanywe kwa kuzingatia kanuni.
Kwa mfano, si kitu cha kupuuzia kwamba wapigakura zaidi ya 100 kukataa kupiga kura na uchaguzi ukaonekana wa kawaida tu hata kama katiba haitaji kiwango cha kura kinachotakiwa kumthibitisha mshindi. Hata katika hayo marekebisho ya katiba, suala hilo lilitakiwa liangaliwe na kutafutiwa ufumbuzi.
Kama DRFA na TFF zinakubaliana kuwa uchaguzi ulioitishwa na uongozi wa Kamtande ulikuwa halali na matokeo ni halali, basi vyombo hivyo viwili havina budi kutangaza kwa kauli thabiti kuwa viongozi halali wameshapatikana na kuomba vyombo vinavyosimamia usalama wa raia na mali zao, vihakikishe viongozi wapya wanafanya kazi yao kwa amani hadi uchaguzi mkuu mwingine utakapoitishwa.
La kama wanachama hawatamkubali Kamtande na viongozi wenzake, katiba huwa inawapa wanachama kuitisha vikao vya dharura kujadili viongozi wao na kutoa uamuzi wa kumuondoa au kuendelea naye kwa kuwa mkutano mkuu ndio chombo cha juu kabisa katika chama.
La sivyo, damu itakuja kumwagika, hasa Temeke ambako chama hicho kina mali za uwekezaji zinazoweza kukiingizia fedha nyingi.
TFF na DRFA hazina budi kuonyesha uongozi katika mgogoro huo kuepuka mambo hayo kuenea kwenye vyama vingine vya wilaya na hata mikoa na baadaye taifa.