Sitoshangaa Ibenge akiondoka Azam FC
Muktasari:
- Ni jambo la kawaida nchini kwa sababu Azam FC ni timu kubwa kama ilivyo kwa Ibenge ambaye ni kocha mwenye jina kubwa hapa na Afrika kijumla.
TAARIFA za Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge kuwa kipaumbele katika orodha ya makocha wanaotakiwa kuinoa timu ya Taifa ya Mali inaendelea kuwa habari ya mjini.
Ni jambo la kawaida nchini kwa sababu Azam FC ni timu kubwa kama ilivyo kwa Ibenge ambaye ni kocha mwenye jina kubwa hapa na Afrika kijumla.
Kana kwamba haitoshi, anatakiwa na Mali ambayo ni miongoni mwa mataifa makubwa kisoka Afrika.
Hapa kijiweni tumeona na kusikia taarifa kutoka kwa uongozi wa Azam FC ukikanusha suala la kocha huyo kuondoka huku ukisisitiza Ibenge ni kocha wao na ana mkataba nao.
Lakini pamoja na makanusho hayo, hatuoni kama itakuwa jambo la ajabu kwa Ibenge kuondoka Azam FC na kujiunga na Mali na kama ikitokea wala hatuwezi kushangazwa na hilo.
Kwanza, kwa kuifundisha Mali, wasifu wa Ibenge utapanda maradufu kulinganisha na Azam FC ambayo bado ni klabu inayopambana kutengeneza alama yake katika soka la Tanzania na Afrika kijumla.
Ukilinganisha hata daraja la wachezaji wa Mali na Azam FC ni vitu viwili tofauti.
Wale wa Mali ni wachezaji wakubwa ambao wanaweza kufanya vitu vitokee kwa urahisi kulinganisha na wachezaji wa Azam FC.
Lakini kitu kingine ni kwamba matokeo ya Azam FC msimu huu hasa kwenye Ligi Kuu yanamsuta Ibenge kwa daraja lake alilojiwekea katika soka la Afrika kwani hayaendani na ukubwa wa jina lake.
Kocha kama Ibenge sio wa kutoka sare mechi 10 kati ya 25 za ligi. Kuna namna ana deni Azam FC.