SPOTI DOKTA: Beki wa Arsenal kufanyiwa upasuaji iko hivi

Muktasari:
- Beki huyo ambaye wiki mbili zilizopita alikuwa katka majukumu magumu ya kuitumikia timu yake ya Taifa ya Brazil katika mechi za kutafuta tiketi ya kombe la Dunia.
Klabu ya Arsenal ilipata pigo wiki iliyopita siku ya jumannne katika mchezo wa ligi kuu EPL dhidi ya Fulham mara baada ya beki wake toka nchini Brazil Gabriel Magalhàes kupata majeraha mabaya ya paja.
Beki huyo ambaye wiki mbili zilizopita alikuwa katka majukumu magumu ya kuitumikia timu yake ya Taifa ya Brazil katika mechi za kutafuta tiketi ya kombe la Dunia.
Wakati akiwa amerudi katika majukumu ya klabu ndipo siku ya mchezo huo alipata majeraha hayo ya paja ambayo yamesabisha kufanyiwa upasuaji wa misuli ya paja.
Jeraha hili litamfanya mchezaji huyo beki wa kati tegemea kukosa mechi zote za msimu huu zilizosalia. Hata katika mchezo wa jana wa ligi ya Mabingwa Ulaya UEFA dhidi ya Madrid alikuwa mtazamaji.
Kwa mwanasoka kufanya majukumu ya Taifa lake na huku ya klabu hali kama hii ya kutumika sana ni moja ya jambo linawaweka katika hatari ya kupata tatizo la kuchanika misuli.

Tatizo aliopata kitabibu hujulikana kama hamstring injury au tears daraja la 3. Ambalo linahusisha msuli kuchanika na kuachana pande 2 au mkia wa msuli yaani tendoni kukwanyuka toka katika mfupa.
Aina hii ndio ambayo imesababisha beki huyu kisiki wa Arsenal kufanyiwa upasuaji wa kisasa wa matundu ili kukarabati msuli huo na tishu jirani na msuli huo.
Mara nyingi aina ya kwanza na ya pili ndio mara kwa mara huwakumba wanasoka na hutumia muda mfupi kupona. Mara baada ya uchunguzi wa picha ilionyesha kuchanika vibaya kwa misuli ya nyuma ya paja.
Daktari huweza kubaini tatizo hilo kwa uchunguz wa kawaidai na majaribio na vile vile kwa vipimo kama xray, picha za CT Scan na MRI hutoa taswira bora za eneo lililojeruhiwa.

Misuli inayochanika ni ipi?
Ni kundi la misuli mikubwa ya nyuma ya paja ambayo iko mitatu, kazi yake ni kusaidia kupiga goti, kunyoosha mguu na kuuzungusha mguu katika mhimil wake.
Misuli hìi kwa mwanasoka ndio inamsaidia sana katika kucheza soka hatimaye kutumika sana. Hii ndio sababu kwa maelfu ya wanasoka kupata majeraha haya mara kwa mara.
Misuli hii huwa na mikia ijulikanayo kitabibu kama tendon ambayo huunganisha msuli katika mfupa. Nyuzi hizi huwa ngumu sana, lakini hupata majeraha ya kuvutika sana au kukatika.
Nyuzi hizo zilizoshikamana kama bunda huvutika na kujikunyata, huwa na muishilio yaani tendoni.
Misuli hii huwa na pande mbili pale msuli inapoanzia na kuishilia, msuli wenyewe huwa katikati, tendon ambazo huwa ni ngumu sana zenyewe zimejipachika katika vichuguu vya maungio ya mifupa ya kiuno upande wa nyuma na huishilia kujishikiza sehemu ya chini katika mifupa ya maungio ya goti upande wa nyuma.

Mchezaji alijeruhiwa sana hujisikia hivi
Wachezaji wanavyopata majeraha na hasa yanapokuwa makali huweza kupata maumivu makali ambayo huanzia nyuma ya paja na kuanzia katika kalio.
Hupata maumivu makali ambayo hayavumiliki ikiwamo kuhisi kama amechomwa na kisu au risasi. Na huwa ni vigumu kuutumia mguu huo kusimamia au hata kuunyoosha.
Kwa kawaida hupata ghafla, maumivu makali nyuma ya paja yenye kupwita, pale panapominywa huleta maumivu, huvimba eneo la nyuma ya mguu dakika chache baada ya kuumia na hupata maumivu wakati wa kukaa chini.
Vile vile uwepo wa michubuko na kubadilka rangi ndani ya siku chache katika mguu uliojeruhiwa. Kwa jeraha kama la daraja la 3 mlio usio wakawaida unaweza kusika hasa kama tendoni imechomoka.

Uanishaji wa majeraha ya misuli
Daraja la 1:
Ni jeraha dogo la msuli wa paja, mara nyingi huitwa mkazo au kuvutwa kuliko ustahimilivu wake. Hii huweza kupona bila dawa na huchukua siku 2 mpaka wiki. Kupumzika kucheza, barafu, kufunga bandeji na kunyanyua ni tiba ya awali bila dawa.
Daraja la 2:
Hapa misuli ya paja huwa imechanika sehemu tu ya misuli au tendon. Hii inaweza kuchukua wiki 2 mpaka mwezi. Upasuaji hauhitajiki lakini dawa za maumivu na matibabu hutolewa.
Daraja la 3:
Hapa misuli ya paja huchanika kabisa na huenda tendon zinazoshikanisha misuli ya paja kwenye mfupa zimeng'oka au kuchomoka.
Sababu za kuchanika misuli
Mara nyingi wanasoka wa kiwango cha juu na hutumiwa sana na timu kuweza kupata mafaniko hivyo misuli ya miili yao iwajibike kutumika kupita kiasi ili kusaidia timu kushinda.
Pale misuli hii inapozidiwa na kazi nyingi huchoka, piia wakati wa kucheza kufanyiwa faulu na kuanguka husababisha majeraha madogo madogo ambayo baadaye huwa makubwa.
Pale majeraha ya ndani kwa ndani na yakiwa madogo baadaye mchezaji anapotumia nguvu kupita kiasi misuli hii huchanika ghafla.
Sababu kuu inayosababisha kuchanika ni kutokana na kuzidiwa uwezo au kupata kazi nzito kupita kiasi.
Vile vile nyuzi nyuzi ndogo za misuli huweza kukunjuka kupita kiasi na kukatika kwa ndani ya msuli wa paja pasipo mchezaji kujua.
Pale mchezaji anapokimbia kwa kasi umbali mfupi vile za mita 100 misuli hii ndio inayoirudisha miguu nyuma huku ukikanyagia na vidole gumba.
Wakati misuli hii ikifanya kazi hujikuta ikielemewa kwa kupata shinikizo kubwa la uzito wa mwili na wakati huo huo huwa na kazi ya hujirefusha na kijifupisha ile kwenda kasi na hapo ndipo pia misuli hupata madhara.

Kupunguza na kujikinga kuchanika misuli
Njia ya kwanza na rahisi ni mchezaji kuhakikisha anazingatia kupasha mwili moto kabla na baada ya mazoezi au mchezo. Mazoezi hayo ni yale ya viungo na ya kuchochea uponaji.
Kuzingatia lishe anayopewa na mtaalam wa lishe za wanamichezo, kuzingatia unywaji maji yakutosha.
Mchezaji asicheze au kufanya mazoezi kabla ya kupona. Muhimu kufanyiwa tathimini kuona kama majeraha hayo yamepona kabisa.
Chukua hii
Wachezaji wenye mchaniko daraja la 3 huweza kufanyiwa upasuaji wa kisasa wa matundu ambao huwa na jeraha la dogo la upasuaji, damu inayopotea ni chache na muda wa kukaa hospitali ni mmchache.
Baada ya upasuaji jeraha daraja la 3 huchukua miezi 3-6 kupona, kipindi hiki mchezaji huwa katika mpango maalum wa uuguzi ili kuhakikisha anapona na kurudi akiwa kama hapo awali.
Kwa sasa Gabi yupo katika uangalizi wa madaktari, huduma yake kwa klabu hiyo ambayo juzi ilichapa Madrid mabao 3-1 katika ligi ya Mabingwa Ulaya UEFA itakosekana kwa msimu wote uliobaki.