Stumai, mtaalamu wa kutikisa nyavu asiye na bahati WPL

Muktasari:
- Fikiria ukiambiwa mshambuliaji wa JKT Queens, Stumai Abdallah hana tuzo ya kiatu cha mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake utaamini? Lakini ndio hivyo ni kama hana bahati.
WAKATI mwingine neno bahati lina maana kubwa kwenye maisha ya mwanadamu. Si kila aliyefanikiwa ametumia nguvu kubwa, wengine ni bahati tu.
Fikiria ukiambiwa mshambuliaji wa JKT Queens, Stumai Abdallah hana tuzo ya kiatu cha mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake utaamini? Lakini ndio hivyo ni kama hana bahati.
Mwanadada huyo ni fundi haswa wa kufumania nyavu hasa msimu huu ambao anaendelea kuweka rekodi mbalimbali ikiwamo kufunga mabao saba peke yake kwenye mchezo mmoja yaani double hat-trick sio mchezo!
Uwezo wake wa kufunga mabao umewaliza makipa wengi Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu hasa Mlandizi Queens ambayo imekubali nyavu zake kutikiswa mara 11 na Stumai pekee, mzunguko wa kwanza akiwafunga mabao manne na wa pili saba.

MISIMU 5 BILA KIATU
Kwenye misimu mitano aliyoichezea mshambuliaji huyo akiwa na uzi wa JKT hajafanikiwa kubeba tuzo hiyo.
Msimu wa 2019/20 alicheza mechi 18 akifunga mabao 22, 2020/21 alicheza mechi tatu na kufunga mabao saba, msimu uliofuata alikaa msimu mzima akiuguza jeraha la goti.
Wakati Jentrix Shikangwa wa Simba Queens anachukua kiatu cha dhahabu msimu huo, Stumai alimaliza na mabao 14 kwenye mechi tisa ikiwa siku chache tangu atoke kuuguza majeraha yake.
Msimu jana alicheza mechi 18 na kuweka kambani mabao 19, wastani wa kufunga bao moja kwa kila mchezo na msimu huu hadi sasa ndio kinara.

2019/2020 - mechi 18 mabao 22
2020/21 - mechi tatu mabao saba
2021/22 - hakucheza alikuwa majeruhi
2022/23 - mechi tisa mabao 14
2023/24 - mechi 18 mabao 19
2024/25 - mechi 12 mabao 23
HUU ATAWEZA?
Kwa muendelezo alionao kwenye kila mchezo kufunga angalau bao moja ama akikutana na timu nyingine kufunga hat-trick ni wazi ana malengo ya kuchukua kiatu msimu huu.
Msimu takribani mitano sasa tangu aingie kwenye vita ya upachikaji mabao mshambuliaji huyo amekuwa akiishia tatu bora na kushuhudia wengine wakinyakua.
Lakini msimu huu ni kama mambo yamebadilika kwani kila anapopata nafasi ya kucheza basi lazima nyavu za timu pinzani zikisike.
Hata hivyo, kwenye mabao hayo ni timu mbili tu ndizo ambazo hajazifunga Stumai yaani Simba na Yanga lakini zilizosalia zimefumuliwa.
Licha ya kuongoza kwa upachikaji lakini ndio mchezaji aliyefunga hat-trick nyingi akiweka nne msimu huu, Jentrix Shikangwa ana tatu, wakati wenye moja kila mmoja ni Neema Paul (Yanga Princess), Asha Djafar (Simba Queens), Ariet Adong (Yanga Princess), Milembe Ndalahwa (Alliance Girls) na Annastazia Lucian (Mashujaa Queens).

Stumai aliifunga Mlandizi hat-trick mbili za mzunguko wa kwanza akifunga mabao manne kwenye ushindi wa 7-0 uliopata JKT Queens, Novemba 05.
Februari 04 zilipokutana tena timu hizo, JKT ilipata ushindi wa mabao 12-0, Stumai akafunga mabao saba peke yake.
Timu nyingine alizozifunga mshambuliaji huyo ni Alliance, Januari 21 kwenye ushindi wa mabao 4-0 na Machi 12 akikamilisha hat-trick ya nne dhidi ya Gets Program.
KUVUNJA REKODI YA MASAKA?
Imepita miaka minne sasa bila rekodi ya Aisha Masaka aliyetimkia Brighton & Hove Albion kuvunjwa katika Ligi Kuu Wanawake ya kufunga mabao mengi.
Msimu 2020/21 Masaka aliibuka mfungaji bora wa WPL akiweka kambani mabao 35 akiwa mzawa wa mwisho kufunga mabao hayo.
Tangu hapo msimu uliofuata Mrundi wa Simba Queens, Asha Djafar alifunga mabao 27, msimu 2022/23 akachukua tena Mkenya, Jentrix Shikangwa akifunga mabao 17 na mwaka jana Aisha Mnunka wa Simba akiweka kambani mabao 20.
Ulikuwa msimu wenye ushindani kwa wachezaji wazawa kwani mfungaji bora alijulikana kwenye mechi za mwisho wa msimu.
Hadi mechi za mwisho Opah Clement wakati ule yupo Simba alikuwa na mabao 34 mechi ya mwisho iliamua Masaka akachukua kiatu baada ya kufunga hat-trick.
Hata hivyo, baada ya kuondoka kwa nyota hao waliopata timu nje ya nchi hakukuwa na ushindani kwa wachezaji wazawa jambo linaonyesha kuna pengo kwa washambuliaji hao.
Kwa sasa Stumai anachuana na Shikangwa ambaye ni Mkenya wakitofautiana mabao manne tu kwenye mechi 13 zilizochezwa WPL.

Hali hiyo inaonyesha namna gani wazawa wamekataa ushindani kwenye upachikaji mabao na badala yake wamemuachia mzigo Stumai.
Zimesalia mechi tano msimu kumalizika na ili Stumai aifikie rekodi ya Masaka anapaswa kufunga mabao 12 kwenye mechi hizo na ili azivunje mabao 13.
MSIKIE KOCHA
Akizungumzia mshambuliaji huyo wa timu ya taifa, Twiga Stars, locha wa JKT Queens, Esther Chabruma anasema anatamani nyota huyo achukue kiatu msimu huu baada ya kukiwania bila mafanikio kwa msimu wa tatu mfululizo. “Nadhani watu wanapaswa kuendelea kumuombea ashinde tuzo mara hii.”