Tujifunze kwa anayofanya Chama
Muktasari:
- Kwa sasa ndiye amekuwa silaha muhimu ya Kocha Steve Barker katika eneo la mwisho la kiuchezaji la Simba ambalo ni lile la kushambulia.
CLATOUS Chama ameonekana kuwa wa moto sana tangu alipojiunga na Simba dirisha dogo la usajili mwezi Januari akitokea Singida Black Stars.
Kwa sasa ndiye amekuwa silaha muhimu ya Kocha Steve Barker katika eneo la mwisho la kiuchezaji la Simba ambalo ni lile la kushambulia.
Kabla ya mchezo dhidi ya Coastal Union jana mjini Tanga, Chama alifunga bao katika mechi tano mfululizo na kati ya hizo, mechi nne aliibuka mchezaji bora wa mchezo.
Alifunga dhidi ya TRA United katika Kombe la Shirikisho la CRDB, na kabla ya hapo alifunga mfululizo katika mechi za Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Mashujaa, Tanzania Prisons, JKT Tanzania na Yanga.
Katika mechi hizo nne za Ligi Kuu ambazo alifunga mfululizo, Chama aliibuka mchezaji bora wa mchezo hivyo akaweka rekodi ambayo haikuwahi kuwepo hapo nyuma katika ligi yetu.
Anachokifanya Chama, anatufundisha mambo mawili ambayo tunaweza kuyatumia katika maisha yetu ya kawaida na yakaleta matokeo chanya.
Kwanza ni kuhakikisha unaacha kazi yako iongee na kukutetea pale ambapo unapitia katika kipindi kigumu cha watu kukukatia tamaa au kupoteza imani na wewe.
Wengi walibeza usajili wa Chama Simba wakiamini mchezaji huyo hawezi tena kuwa na msaada kwa timu hiyo ambayo amerejea kwa mara ya pili tofauti.
Jambo la pili anatukumbusha umri ni namba tu. Kuwa na umri mkubwa au mdogo hakukuzuii kufanya mambo makubwa na muhimu ni kutumia zaidi akili na kipawa chako.