Ukitaka kucheza nje muulize Adam Salamba

Muktasari:
- Salamba anasimulia safari ya kucheza kwake nje na namna ambavyo changamoto hazichukulii kuwa sababu ya kuua ndoto zake, lakini kubwa akiwataka wachezaji wenzake kutumia fursa hizo bila kukata tamaa.
WAHENGA wanasema penye nia pana njia. Ukitaka kuamini msemo huo unafanya kazi ni namna anavyosimulia mshambuliaji wa zamani wa Simba, Adam Salamba ambaye msimu huu alicheza Ligi Kuu Libya.
Salamba anasimulia safari ya kucheza kwake nje na namna ambavyo changamoto hazichukulii kuwa sababu ya kuua ndoto zake, lakini kubwa akiwataka wachezaji wenzake kutumia fursa hizo bila kukata tamaa.
"Kwanza mchezaji kucheza nje ni utayari wake mwenyewe. Kutokata tamaa kujaribu kila wakati kwenda kufanya majaribio. Kutojihurumia namna ya kuishi nje na nyumbani na kumuomba Mwenyenzi Mungu. Naamini kuna siku milango itafunguka," anasema Salamba.
Katika mahojiano na Mwanaspoti anazungumza mambo mbalimbali kuhusiana na maisha ya nje, kutafutwa na waandaaji wa filamu na wanamuziki ili kutokea katika kazi zao kutokana na uvaaji wake.

ANAVYOPATA DILI NJE
Salamba anasema dili za kucheza nje zinatokana na kufanya kazi na mawakala tofauti, ambapo anayepata timu anampigia simu na akiona kuna maslahi yanalipa anasaini mkataba.
"Nchi za wenzetu suala la mawakala kuwepo uwanjani kwa wingi ni kawaida, akivutiwa na kiwango cha mchezaji anamfuata baada ya mechi na kumuomba kufanya naye kazi, kisha kubadilishana namba ili akipata timu iwe rahisi kuwasiliana naye," anasema Salamba na kuongeza:
"Wengi wanajiuliza na wengine wananifuata moja kwa moja kutaka kujua njia nayoitumia kupata timu nje, milango ilianza kufunguka baada ya kuichezea Al -Jahra ya Kuwait niliyojiunga nayo 2019 nikitokea Simba. Huko nilikutana na mawakala tofauti na sikutaka niwe chini ya mtu mmoja, ndiyo maana anayepata timu ananipigia nikiona maslahi yananifaa nasaini mkataba."
Salamba anasema japokuwa changamoto za kucheza soka nchi za Kiarabu ni nyingi, lakini anakomaa kwani anajua anachokitafuta na utakapofika muda wa kurudi kucheza nyumbani atafanya hivyo.
"Mfano tangu niende Libya sijawahi kukukutana na mwanamke barabarani. Nilipokuwa naishi nilikuwa nasikia vicheko tu kwa majirani. Tahadhari ya kwanza wakati najiunga na timu niliambiwa niheshimu wanawake na nisijaribu kufanya nao mazoea. Mtu anayefanya makosa hayo kifo kinamhusu, maana nchi hiyo huwezi kuishi wala kulala na mwanamke usiyemuoa," anasema.
"Changamoto nyingine ni chakula chao nilikuwa siwezani nacho, hivyo nikiwa naondoka nchini nabeba mchele, unga na maharage nakuwa najipikia mwenyewe jambo la msingi ni kuweka nguvu na umakini kufanya kitu kilichonipeleka huko."

UTOFAUTI WA SOKA TZ NA UARABUNI
Anasema kitu anachokiona ni cha tofauti kwa nchi alizocheza ni miundo mbinu kuhusiana vipaji anaona Tanzania vipo vikubwa :"Naona vipaji vya wenzetu ni vya kufundishwa zaidi, ukitofautisha na sisi na kama wengi wetu tungepitia katika vituo vya soka tungekuwa na mafanikio makubwa zaidi."
Vipi kuhusu kuitwa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' anasema akiwa Al Maalab ya Libya Tripoli kocha alimpigia simu ila kwa bahati mbaya akawa amevunjika taya, hivyo hakuweza kujiunga na wenzake.
"Timu ya Stars kipindi hicho ilikuwa inakwenda kuweka kambini Misri kujiandaa na michuano ya kufuzu Afcon iliyokuwa imechezwa Morocoo, lakini kutokana na kuumia taya ilitakiwa nikae miezi miwili kujiuguza,"anasema.
Anasema kutokana na changamoto za wachezaji kuumia viwanjani kuna umuhimu wa bima za afya ambazo zitawasaidia kutibiwa kirahisi:"Kama hujakumbana na changamoto ya majeraha huwezi kujua umuhimu wa bima, ninachoshukuru kwa timu za nje kila kitu cha matibabu kinakuwa kwao."

AKUTANA NA MDOGO WA BANEGA LIBYA
Anasema kocha wa viungo wa timu ya Benghazi ya Libya aliyemtaja kwa jina la Caro mdogo wake na Éver Banega mchezaji wa zamani wa Sevila na sasa anacheza CA Newell's Old Boys ya Argentina katika stori za hapa na pale akajua ni ndugu wa staa huyo.
Mwaka 2019 Simba ilicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Sevilla iliyowafunga mabao 5-4 baada ya dakika 90 Salamba aliomba viatu kwa Banega na akapewa jambo ambalo lilitrendi sana katika mitandao ya kijamii kipindi hicho.
"Katika stori za hapa na pale na kocha Caro akamtaja Ever Banega kuwa ni kaka yake wa kuzaliwa ndipo nikamsimulia stori yangu ya kumuomba viatu jambo ambalo lilimshangaza sana kuona nampa heshima mchezaji mwenzangu," anasema Salamba na kuongeza;
"Aliniambia ukimuona mchezaji anamheshimu mchezaji mwingine hadi kufikia hatua ya kubaki na kumbukumbu yake basi anakuwa na kitu kikubwa anakifanya uwanjani, kwani siwezi kushangaa kumuona shabiki akiomba jezi, viatu kusainiwa kitu chake hao wanafanya kwa ajili ya ushabiki.
Anaendelea kusimulia:"Baada ya kufahamiana tukawa washikaji kuna siku aliwahi kuzungumza na kaka yake kwa simu akamsimulia kwamba mliwahi kwenda Tanzania kuna mchezaji wa Simba alikuomba viatu nipo naye timu moja akaonyesha kufurahia na kuheshimu, kiukweli viatu hivyo vipo hadi leo, nimeviweka kwa ajili ya mwanangu wa kiume kwa sasa ana miaka minne, akijitambua nitamwelezea stori yake."
Anasema mtoto wake huyo anapenda sana mpira, anakumbuka wakati anaanza kutembea kulikuwepo na mpira mbele yake akawa anaufuata:"Natamani awe kuwa mchezaji mkubwa ikitokea hivyo akikua yeye ndiye atakaye vaa viatu vya Banega."

NJE KUMELIPA ZAIDI
Siyo muumini wa kuanika mafanikio yake, lakini anasema kucheza nje kumemlipa kwa asilimia kubwa, amefanikiwa kupata vitu vya ndoto zake na kuzidi.
"Mpira wa miguu umebadilisha maisha yangu kwa ujumla ndiyo maana naendelea kupambana ingawa siwezi kutaja kitu kimoja baada ya kingine nilivyovifanya, sioni kama ni jambo sahihi," anasema.
Ingawa alipoulizwa kuhusiana na tetesi za watu kuhusu kumiliki maduka ya dhahabu anasema:"Umeamua kunichimba ila hilo jambo si kitu kigeni kwangu kilikuwepo, kitakuwepo na nikistaafu soka nitajikita na ishu za dhahabu, kwa sababu washikaji zangu niliyokua nao wapo huko wanapesa sana."

MKALI WA MAVAZI
Anasema kwa asilimia kubwa ya watu wanadhani alianza kupendeza akiwa Simba, lakini ni kawaida yake tangu anacheza timu ya mtaani kwao Mwanza iliyokuwa inajulikana kama Madini kwani viongozi walikuwa wanawapa pesa ambazo aliweza kujikimu nazo kimaisha.
"Nilikuwa napenda kupendeza tangu nikiwa timu za mitaani, nilipojiunga na Stand United na Lipuli wachezaji wenzangu walikuwa wanapenda aina ya uvaaji wangu, isipokuwa ukubwa wa klabu ya Simba ulifanya nionekane na watu wengi ndio maana wakadhani nimeanza kupiga pamba nikiwa na Wanamsimbazi" anasema na kuongeza;
"Nikiipenda nguo naweza nikanunua kwa gharama kubwa ingawa siwezi kukutajia ni kiasi gani cha pesa kwa upande wa wachezaji ambao napenda aina ya uvaaji wao ni Himid Mao kwa mtu mwenye jicho la mavazi anaelewa pigo zake na kwa nje namkubali Neymar."

UVAAJI WAFUNGUA FURSA
Anasema amekuwa akitafutwa na waandaaji wa filamu wakubwa hapa nchini na wanamuziki wakimtaka atokee katika kazi zao, kutokana na muonekano wake ilikuwa ngumu kukubali ofa zao hakutaka kuchanganya mambo.
"Siwezi kuwataja watu ambao walinifuata nifanye nao kazi kwenye filamu na muziki, sikuwa tayari kukubaliana na ofa zao, kwani nahitaji kuwekeza nguvu zaidi katika mazoezi yatakayonifanya niwe bora uwanjani, labda kwa baadaye nikistaafu mpira naweza nikafungua duka la mavazi na kwenda kufanya kazi katika migodi ya madini, huko kwenye filamu na muziki sijioni ingawa wahusika wananiona naweza," anasema Salamba anayemtaja John Bocco ndiye straika wake bora wa muda wote.

MASTAA SIMBA, YANGA
Anasema kuna mastaa wa kigeni wanaofanya kazi nzuri, anamtaja kiungo wa Yanga Pacome Zouzou (mabao manane) na mshambuliaji wa Simba Charles Ahoua (kinara wa mabao 12) kwa wazawa Clement Mzize (mabao 11), Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' (mabao matano, asisti 12).
"Sina maana wengine hawafanyi vizuri ila kuna kuzidiana, hao wachezaji kwa sasa wapo katika kiwango kikubwa, ukiachana na hao wakati nacheza ligi ya ndani Bocco ni mshambuliaji wa muda wote kwangu, kuna Meddie Kagere, Emmanuel Okwi hao jamaa walikuwa hatari, ingawa nyuma yao alikuja Fiston Mayele akiwa Yanga," anasema.

TIMU ALIZOCHEZA
Timu alizocheza nje ni Ghaz El Mahalla ya Misri, Js Soura ya Algeria na Al Maalab ya Libya Tripoli, El Banes ya Benghazi Libya na anasisitiza ataendelea kukomaa nje hadi kieleweke.
Kwa Timu za hapa nchini ni Stand United, Lipuli ambako alifunga mabao tisa katika mechi 13 jambo lililoivutia Simba kumsajili 2018/19 na Namungo.
"Niliondoka Simba nikiwa nimefunga mabao saba, ninachokumbuka nilijiunga ikiwa na wachezaji katika nafasi yangu wakiwa kiwango cha juu kama Okwi, Bocco, Kagere hivyo kupata nafasi katikati yao ilikuwa uache kazi ufanye kazi, kitu kikubwa walinifunza kujiamini," anasema.