Mbeya City kujiuliza kwa Simba

Muktasari:
Mbeya City na Simba zimekutana mara saba katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya ambapo wenyeji wameshinda mechi moja, huku Simba ikishinda mara tano na zimetoka sare katika mchezo mmoja
Mbeya City itaikaribisha Simba leo Desemba 13 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, lakini swali ni je itaweza kurudia rekodi ya msimu wa 2014/2015 dhidi ya mabingwa hao watetezi?
Timu hiyo imekutana na Simba mara saba kwenye uwanja huo lakini imewahi kuwafunga wapinzani wao katika mechi moja tu iliyofanyika April 18, 2015 iliposhinda kwa mabao 2-0 huku mechi nyingine sita ikipoteza tano na kutoka sare moja.

Msimu wa 2014/2015 ndio ulikuwa bora kwa Mbeya City tangu ipande daraja mwaka 2013, ikiwa chini ya kocha Juma Mwambusi na ndio ilioifunga Simba katika mechi zote mbili ikianza kuichapa ugenini Dar es Salaam kwa mabao 2-1 (Januari 8, 2015) na kisha kuisulubu nyumbani kwa mabao 2-0.
Tangu hapo Mbeya City haijawahi kufanya hivyo tena kwani katika mechi 10 zilizofuata iliambulia vipigo mara tisa na sare moja dhidi ya Simba.
Msimu huu Mbeya City haijaanza vizuri Ligi kuu Bara huku ikidaiwa sababu kubwa ni kutokana na ugeni wa wachezaji wengi wa kikosi hicho.
Matokeo yake yalisababisha kutimuliwa kwa kocha wake Amri Said na kuajiriwa Mathias Lule ambaye leo ataiongoza timu mara ya kwanza dhidi ya Simba.

Mechi tatu zilizopita za ligi ambazo Mbeya City ilishinda ni dhidi ya JKT Tanzania kwa bao 1-0 na mbili ikitoka suluhu na Mtibwa Sugar pamoja na Coastal Union ambazo zimeonekana kuiongezea kasi timu hiyo ambayo ilicheza vizuri katika michezo hiyo.
Hata hivyo, Mbeya City inakabiliwa na wakati mgumu wa kuizua Simba ambayo inapambana kushinda mechi zake ili kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi, ambapo kwa sasa Yanga ndio inaongoza ikiwa na pointi 37 kileleni baada ya mchezo wa jana dhidi ya Mwadui.

Pia kasi ya ufungaji wa mabao ya wachezaji wa Simba inaweza kuwa mtihani kwa Mbeya City ambayo ni timu ya tano kwenye ligi iliyoruhusu mabao mengi, kwani Wekundu wa Msimbazi wameonekana hawatanii linapokuja suala la kufunga na ndio maana ndio timu pekee inayoongoza kwa kufunga idadi kubwa ya mabao kwenye ligi ikiwa imefunga 31.
Simba inaongozwa na pacha matata ya mabao John Bocco mwenye mabao saba, Clatous Chama aliyefunga sita na Meddie Kagere mwenye mabao manne wakati Mbeya City inamtegemea zaidi mshambuliaji Kibu Denis mwenye mabao matatu.
Ushindi wa leo kwa Simba utawafanya wawavutie kasi wapinzani wao wakubwa kwenye mbio za ubingwa, Yanga na Azam na kupunguza pengo la pointi huku ikiwa na mechi mbili mkononi.
Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema wataingia uwanjani huku wakiwapa heshima wapinzani wao licha ya kwamba hawajafanya vizuri katika michezo mingi iliyopita katika ligi.
“Licha ya kwamba hawapo sehemu nzuri kwenye msimamo wa ligi lakini mechi zao tano za mwisho hawajafanya vibaya kama walivyoanza, kwa hiyo tunajua mchezo utakuwa mgumu kiasi gani,” alisema Vandebroeck

Kocha wa Mbeya City, Mathias Lule alisema wataingia katika mchezo huo wakiiheshimu Simba kwani wanajua ni timu kubwa na ndio mabingwa bingwa watetezi wa kombe la Ligi Kuu.
“Hatupo katika nafasi nzuri na tunatakiwa kupata ushindi katika mechi zetu ili tuweze kupanda juu katika msimamo wa ligi,” alisema Lule.
“Simba ni timu nzuri na kubwa, hivyo tunapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa dhidi yao. Tumefanyia kazi upungufu wetu na jambo la msingi ni vijana kutumia vyema nafasi ambazo tutatengeneza (katika mchezo huo).”
Mechi nyingine leo zitakuwa kati ya Coastal Union itakayokuwa mwenyeji wa maafande wa Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Imeandikwa na Oliver Albert