Tizi la Simba Morocco hadi raha

RABAT, MOROCCO. MABOSI wa Simba jana waliwasapraizi mashabiki wao kwa kumtambulisha mrithi wa Luis Miquissone, huku kambi yao iliyopo Rabat imenoga baada ya msafara wa pili wa timu hiyo akiwamo beki Henock Inonga Kaba ‘Varane’ kutua na kumfanya Kocha Didier Gomes kucheka na fasta kuwatengenezea programu ya kuwapigisha vijana wake tizi mara mbili ili kuwaweka fiti kwa msimu ujao wa ligi ya ndani na kimataifa.
Simba iliyowapiga bei nyota wake Clatous Chama na Luis Miquissone imemtambulisha Duncan Nyoni ‘Monster’ kutoka Malawi.
Winga huyo anayetumia miguu yote miwili ana umri wa miaka 23 na ni mmoja ya wachezaji wa timu ya taifa Malawi na amejiunga na Simba akitokea Silver Strikers.
Wakati winga huyo akitambulisha Dar, kule Morocco Simba iliyojichimbia katika hoteli ya Dawliz Resort & SPA, ikianza na kundi la kwanza la wachezaji na baadhi ya watu wa benchi la ufundi, jana ilinoga zaidi baada ya kupokea kundi la pili akiwamo Varane.
Wachezaji 15 waliokuwa katika msafara wa kwanza kwenye kambi hiyo ya Rabat, walianza kupigishwa tizi la maana katika mazoezi yaliyofanyika viwanja vya Dawliz. Awamu hiyo ilifanyika Alhamisi kuanzia saa 3 asubuhi (sawa na saa 6 mchana kwa Tanzania) kwa wachezaji hao kupigishwa tizi mbalimbali ya gym.
Chini ya kocha wa viungo, Adel Zrane aliwahenyesha kwenye viungo, kunyonga baiskeli, kukimbia huku wanaruka vihunzi, kukimbia katika mashine maalumu na mengineyo.
Baada ya mazoezi hayo magumu yaliyofanyika kwa zaidi ya saa 1:30 wachezaji wote walikwenda kupata chakula cha mchana na kupumzika wengi wao wakienda kulala katika vyumba ndani ya hoteli ya kishua ya Dawliz Resort & Spa.
Ilipofika saa 10:30 jioni ya Morocco wachezaji hao walikwenda katika mazoezi ya awamu ya pili ambayo yalifanyika uwanjani na hapo, Adel alianza kusimamia shoo nzima kabla ya Didier Gomes na Seleman Matola nao kutoa yao.
Wachezaji hao 15 walionekana kuwa na furaha kila mmoja akijituma katika zoezi ambalo anapatiwa - liwe gumu kiasi gani ila alitaka kuonyesha benchi la ufundi kuwa ana uwezo wa kulifanya vizuri.
Jioni ya jana ambayo ilikuwa siku ya pili kwa kundi la kwanza kufanya mazoezi kulikuwa na furaha baada ya wachezaji wa kundi la pili kuwasili Rabat na kuungana nao katika ratiba y mazoezi.
Katika kundi la kwanza walikuwepo Jonas Mkude, Joash Onyango, Gadiel Michael, Peter Banda, Kennedy Juma, Hassan Dilunga, Aishi Manula, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Benno Kakolanya, Erasto Nyoni, Taddeo Lwanga, Bernard Morrison, Mzamiru Yassin, Larry Bwalya na Shomary Kapombe.
Kundi la pili waliowasili jana Ijumaa ni Inonga ‘Varane’, Yusuph Mhilu, Abdulsamad Kassim, Israel Patrick Mwenda, John Bocco, Chriss Mugalu, Ibrahim Ame, Ally Salim, Ibrahim Ajibu na kocha wa makipa Milton Nienov.
Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema kwanza wanafurahi kuwa Rabat kutokana na hali ya hewa na kutokana na kazi ambayo wamepanga kuifanya katika kpindi cha mazoezi.
Gomes alisema kila kitu ni kama mshangao kwao kwani kuna mazingira mazuri ya kufanyia mazoezi kama gym, uwanja wa nyasi bandia na viwanja vizuri vyenye nyasi asilia ambavyo wanavitumia.
“Tumeanza mazoezi kwa awamu mbili - asubuhi na jioni, siku ya kwanza Agosti 12 na kundi la wachezaji wa awamu wa kwanza na nategemea Agosti 13, kupokea kundi la wachezaji wengine jioni,” alisema Gomes.
“Katika mazoezi yetu ya awamu ya kwanza tumeanzia chini taratibu ila ambacho nimekiona kila mchezaji yupo tayari kwa ajili ya kushindana katika maandalizi ya msimu mpya.”