Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siku 15 ngumu kwa Simba SC

SIMBA Pict

Muktasari:

  • Mchezo huo utakaochezwa Jumapili hii nchini Afrika Kusini, Simba itaingia uwanjani ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani ilioupata Aprili 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

SIMBA tayari ipo Sauzi ikiendelea kujifua kujiandaa na mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Stellenbosch, huku kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids akikabiliwa na mtihani mgumu zaidi mbele yake.

Mchezo huo utakaochezwa Jumapili hii nchini Afrika Kusini, Simba itaingia uwanjani ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani ilioupata Aprili 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Kwa sasa Simba inahitaji sare tu au ushindi kutinga fainali ya michuano hiyo ambapo Fadlu ataweka rekodi ya kuirudisha tena timu hiyo fainali ya michuano ya CAF baada ya miaka 32 kutokana na mwaka 1993 kucheza fainali ya Kombe la CAF.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara mara 22, kiu yao kubwa ni kuona msimu huu unakuwa na mafanikio zaidi kwao na hilo wanaona linawezekana kutokana na kuwepo kwenye njia nzuri.

Hiyo inatokana na Simba kuwa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na Kombe la Shirikisho (FA), huku ikishika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ambapo vita yake ya kuwania ubingwa dhidi ya Yanga bado ipo wazi. Yeyote kati yao anaweza kubeba.

Hata hivyo, haitakuwa rahisi kwani hivi sasa Simba inakabiliwa na ratiba ngumu zaidi kuliko Yanga, kwani kuanzia Aprili 27 hadi Mei 11, itatakiwa kucheza mechi tano ndani ya siku 15 ikiwa ni wastani wa kucheza mechi moja kila baada ya siku tatu.

Wakati huo ambao Simba inacheza mechi tano za hesabu kali, watani wao wa jadi, Yanga hawana kingine zaidi ya kushiriki Kombe la Muungano ambapo Jumamosi watacheza dhidi ya KVZ, wakifanikiwa kushinda watakwenda kucheza nusu fainali ya michuano hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Mei Mosi. Endapo Yanga itafika hadi fainali, maana yake itacheza mechi tatu ndani ya siku sita.

Simba inayosaka ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuukosa kwa misimu mitatu mfululizo, Jumapili hii ikimalizana na Stellenbosch katika Kombe la Shirikisho Afrika, itarejea Tanzania kukabiliana na Mashujaa kwenye Ligi. Mchezo huo dhidi ya Mashujaa utachezwa Mei 2 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Ugumu wa mchezo huo unakuja kipindi hiki ambacho Mashujaa bado haijajihakikishia kubaki kwenye ligi, huku Simba ikianza kampeni yake ya kuisaka Yanga kileleni baada ya kuzidiwa pointi 13 na michezo minne. Zilipokutana duru la kwanza, Simba ilishinda 1-0 ugenini.

Kwenye msimamo wa ligi, Mashujaa inashika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 30, imebakiwa na mechi nne ambazo kwanza inatakiwa kupata angalau pointi moja ili kutokuwa katika mstari wa kushuka daraja moja kwa moja, kisha ipambanie pointi za kuepuka kucheza mtoano.

Simba itacheza tena Mei 5 dhidi ya JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar. Uwanja huo umekuwa mgumu kwa wapinzani kupata ushindi kwani JKT Tanzania msimu huu imepoteza mechi moja tu hapo dhidi ya Singida Black Stars ilipofungwa 1-0, Februari 13 mwaka huu, hivyo Simba inakwenda kukabiliana na mpinzani mgumu, hata mechi ya kwanza ilikuwa ngumu lakini Simba ikashinda 1-0 kwa bao la penalti lililofungwa na Jean Charles Ahoua dk 90+5.

JKT angalau ipo juu kwenye msimamo kuliko Mashujaa na KMC ikiwa nafasi ya saba na pointi 32.

Mei 8, Simba itacheza mechi nyingine ya ligi dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex. Huyu ni mpinzani mwingine ambaye naye yupo kwenye hatari ya kushuka daraja. KMC inashika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 30, mahitaji yao na Mashujaa yanafanana, hivyo haitakuwa mechi rahisi. Duru la kwanza Simba ilishinda 4-0.

Pamba Jiji ni mpinzani mwingine wa Simba katika mtihani alionao Fadlu ambapo mechi yao itachezwa Mei 12 kwenye Uwanja wa KMC huku wenyeji Simba wakiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi ya kwanza bao 1-0.

Kwa sasa Pamba Jiji inapiga hesabu za kujinasua kushuka daraja ikiwa nafasi ya 13 na pointi 27 kwenye mstari wa kucheza mechi za mtoano.

Baada ya kumaliza hapo, Simba itakuwa na michezo 26 ya ligi sawa na Yanga, hivyo matokeo yao yataamua gepu la pointi litakuwa ngapi katika kuwania ubingwa.

Kisha Simba mchezo wa 27 itaivaa Singida Black Stars utakaochezwa Mei 14 kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Siku moja kabla Yanga itatangulia uwanjani hapo kucheza dhidi ya Namungo.

Kocha Fadlu yupo katika mtihani mzito kuhakikisha gepu la pointi 13 walilonalo kwa sasa analipunguza kwa kushinda mechi zote za ligi ili kufikisha 69 na kuwa nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi moja pekee.

Katika mikakati ya kuhakikisha michezo hiyo yote Fadlu anaicheza vizuri bila ya kuathiri malengo yao, kocha huyo amesema kikosi chake kina wachezaji bora ambao kila atakayempa nafasi anaonesha uwezo, hivyo hana wasiwasi.

“Kila mechi inaamua jambo fulani, hivyo tutacheza kwa kiwango kilekile kusaka matokeo mazuri kwani nina wachezaji wanaojituma kupambania matokeo mazuri,” alisema Fadlu.

Hii ni mara ya pili kwa Fadlu msimu huu kuwa na mtihani wa kuiongoza Simba kucheza michezo mitano mfululizo ya mashindano tofauti katika kipindi cha takribani wiki mbili kwani alifanya hivyo kuanzia Desemba 15 hadi 28, 2024 huku ikishinda yote. Katika mechi hizo, moja ilikuwa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi na mingine Ligi Kuu Bara.

Matokeo ya mechi hizo ilizocheza ndani ya siku 14 yalikuwa hivi; Simba 2-1 CS Sfaxien (Desemba 15, 2024), Simba 2-0 KenGold (Desemba 18, 2024), Kagera 2-5 Simba (Desemba 21, 2024), Simba 1-0 JKT Tanzania (Desemba 24, 2024) na Singida BS 0-1 Simba (Desemba 28, 2024).