Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bodi ya Ligi na TFF wakae, wamalize tofauti zao

Pichani ni Rais wa TFF Jamal Malinzi

Muktasari:

Pamoja na malengo mbalimbali ya kuanzishwa kwake, wadau hao walikuwa wakitaka uhuru katika usimamizi wa ligi pamoja na kuboresha udhamini kwa lengo la kuzineemesha klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Bara.

KABLA ya kuanzishwa kwa Bodi ya Ligi, baadhi ya wadau wa soka hasa viongozi wa klabu walihimiza juu ya kuanzishwa kwa bodi hiyo.
Pamoja na malengo mbalimbali ya kuanzishwa kwake, wadau hao walikuwa wakitaka uhuru katika usimamizi wa ligi pamoja na kuboresha udhamini kwa lengo la kuzineemesha klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Bara.
Hoja hizo zilikuja baada ya baadhi ya viongozi wa klabu kulalamika kutoridhishwa kwao na mapato yatokanayo na udhamini, kwamba klabu zimekuwa zikipunjwa.
Klabu zilitaka kuwa na chombo chao ambacho kingesimamia maslahi yao ndani ya TFF na baada ya malumbano ya muda mrefu hatimaye chombo hicho kilianzishwa.
Hata hivyo tuseme ukweli kwamba bado chombo hicho hakijaweza kukidhi matarajio yaliyokuwa yakizungumzwa awali, bado kina kazi kubwa ya kufanya kukidhi matarajio hayo.
Tunaamini kadri siku zinavyokwenda chombo hicho kinaweza kukidhi malengo ya kuanzishwa kwake kwani bado mapema mno, chombo chenyewe hakijatimiza hata miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake.
Kwa upande wetu tunaamini umoja na mshikamano kati ya Bodi ya Ligi na TFF ni kitu muhimu kutokana na ukweli kwamba vyombo hivyo vinatakiwa kufanya kazi pamoja kwa maslahi ya soka la Tanzania.
Ni taasisi ambazo kila moja ina kazi yake lakini mwisho wa siku wote msingi wa chochote wanachokifanya unaangukia katika maendeleo ya soka, tofauti zozote baina ya vyombo hivyo ni kikwazo katika maendeleo ya soka.
Tumeshitushwa na habari za hivi karibuni zilizotolewa na Rais wa Bodi ya Ligi, Ahmed Yahya kwamba TFF imekuwa ikiingilia utendaji wao.
Kauli hiyo imeonyesha kwamba umoja na mshikamano kati ya vyombo hivyo viwili haupo kwani kama ungekuwapo ni wazi kwamba mambo hayo ya kuingiliana majukumu yangemalizwa katika vikao vya ndani. Ingekuwa rahisi kuitisha mkutano na kujadiliana juu ya baadhi ya mambo madogo na makubwa na hatimaye kila upande unaridhika na kwa hakika huo ndio ushirikiano wa kuendesha gurudumu la soka nchini.
Ni kweli kwamba Bodi ya Ligi ni chombo kilichoundwa ndani ya TFF lakini kina haki ya kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na inapobidi kuingiliwa basi liwe jambo ambalo limekwenda kinyume na taratibu za soka au kinaharibu mipango ya maendeleo ya soka.
Kwa kauli ya bosi wa Bodi ya Ligi ni wazi kwamba kuna mambo ambayo bodi inayafanya na TFF haikubaliani nayo hali inayodhihirisha kuwapo maelewano duni kati ya TFF na Bodi ya Ligi.
Wakati yote haya yanatokea, ni hivi karibuni tu zimeibuka habari za kupanguliwa ghafla kwa ratiba ya mechi za Ligi Kuu Bara ambazo zilipaswa kuchezwa juzi Jumatano.
Ni dhahiri kwamba tofauti zilizoanikwa na bosi wa Bodi ya Ligi zinamfanya mtu aamini kwamba hata upanguaji mara kwa mara wa ratiba ya mechi za Ligi Kuu kiini chake ni tofauti kati ya TFF na Bodi ya Ligi.
Kwa mantiki hiyo ni vyema viongozi wa TFF na Bodi ya Ligi wakakaa pamoja haraka na kumaliza tofauti zao ambazo madhara yake yanakwenda moja kwa moja kwenye soka la Tanzania.
Ugomvi au maelewano duni ya TFF na Bodi ya Ligi yanaweza kuhusishwa moja kwa moja na usemi wa wagombanapo fahari wawili ni nyasi ambazo huumia, kwa maana nyingine anayeumia katika ugomvi huo ni klabu na soka la Tanzania kwa ujumla.