Prime
Dabi ya moto, Miloud aitengea Simba siku mbili

Muktasari:
- Hata hivyo, kwa sasa mashabiki wa Yanga na Simba tambo zipo juu baada ya jana Wekundu wa Msimbazi nao kuwazima Coastal Union mjini Arusha kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na straika Steven Mukwala akiwa mcheza wa tatu kufunga hat-trick katika ligi msimu huu nyuma ya Prince Dube na Stephen Aziz KI.
YANGA ilirejea Dar es Salaa jana ikiwa na vaibu baada ya kuwafunga Pamba Jiji kwao, Mwanza kwa kipigo cha mabao 3-0, lakini mambo kwa sasa ni Dabi ya Kariakoo inayotarajiwa kupigwa Jumamosi ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Hata hivyo, kwa sasa mashabiki wa Yanga na Simba tambo zipo juu baada ya jana Wekundu wa Msimbazi nao kuwazima Coastal Union mjini Arusha kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na straika Steven Mukwala akiwa mcheza wa tatu kufunga hat-trick katika ligi msimu huu nyuma ya Prince Dube na Stephen Aziz KI.
Wakati dabi ukiwa ndio mchezo unaofuata kati ya timu hizo, kocha wa Yanga, Hamdi Miloud akiwasifu mastaa wake kuonyesha ukomavu mkubwa dhidi ya Pamba, lakini amekuwa kujipa muda akitenga siku mbili za kujipanga kwa ajili ya Dabi ya Kariakoo.
Kikosi hicho kilikuwa na michezo miwili mfululizo ugenini kikicheza dhidi ya Mashujaa na Pamba Jiji, na kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 8-0 katika mechi zote.
Mabingwa hao watetezi hadi sasa wameweka rekodi ya kucheza mechi 22 wakijizolea alama 58 wakiongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hamdi alisema jana amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake.
“Kwenye hizi mechi tano zilizopita baada ya sare dhidi ya JKT, wachezaji wangu walionyesha ukomavu mkubwa wakiendelea kufanya mabadiliko machache ninayoendelea kuwapa,” alisema.

KUHUSU SIMBA
Mchezo unaofuata kwa Yanga itakuwa nyumbani ikiikaribisha Simba, huku kocha huyo akisema utakuwa ni wa timu kubwa mbili bora Bara.
“Kuhusu mchezo dhidi ya Simba, zinakwenda kukutana timu mbili bora msimu huu zinazoendelea kupishana juu ya msimamo. Nataka kukaa siku mbili - leo (jana) na kesho (leo) kuwaza ni namna gani nitaingia tofauti kwenye mchezo huo mgumu. Lakini naamini wachezaji wangu watafanya kitu kikubwa, kwani Yanga tutaingia kivingine ili tupate ushindi,” alisema.
Yanga imeizidi Simba alama nne kileleni, huku wababe hao wa Jangwani wakiwa mbele kwa kucheza mechi 22 ilhali Wekundu 21.
Mabingwa hao mara tatu mfululizo wanaonyesha kujiamini kutokana na alama za mtani wao kuwa chini, kwani hata akicheza mechi ijayo na hawezi kuwafikia.

ANAVYOCHANGA KARATA ZAKE
Ushindi wa Yanga wa mabao 3-0, ilioupata juzi dhidi ya Pamba Jiji, umemfanya kocha Hamdi kutembelea nyayo za mtangulizi wake, Sead Ramovic aliyeondoka na kutimkia CR Belouizdad ya Algeria, kutokana na rekodi zao za sasa.
Hamdi aliyejiunga na Yanga Februari 4, mwaka huu, kuchukua nafasi ya Ramovic, tangu ajiunge na kikosi hicho ameendeleza rekodi bora katika michezo ya Ligi Kuu Bara msimu huu, jambo linaloonyesha amefuata nyayo za mtangulizi wake kikosini.
Kocha huyo tangu ajiunge na Yanga ameiongoza katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara. Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, alijiunga na Yanga akitoka Singida Black Stars aliyojiunga nayo Desemba 30, mwaka jana, akiiongoza katika michezo sita, ambapo kati ya hiyo ameshinda mitano na kutoka sare mmoja hadi sasa.
Michezo ya ushindi ni (6-1) v KenGold, (6-1) v KMC FC, (2-1) v Singida Black Stars, (5-0) v Mashujaa FC, (3-0) v Pamba Jiji na suluhu ya (0-0) v JKT Tanzania, ambapo safu ya ushambuliaji ya timu hiyo imefunga mabao 22 na kuruhusu matatu.
Akizungumza baada ya mchezo wa juzi, Hamdi alisema licha ya uwanja kutokuwa rafiki kwa nyota wa kikosi hicho, lakini anashukuru kwa viwango bora walivyovionyesha ambavyo vimewasaidia kuondoka na pointi tatu muhimu.
“Nilichohitaji ni pointi tatu tu bila ya kujali idadi ya mabao. Ni mwenendo mzuri ambao tunazidi kuuonyesha mechi baada ya mechi. Hili ni jambo nzuri kwetu kwa sababu linatujengea ari ya kujiamini na kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea.”

Kwa upande wa Ramovic, raia wa Ujerumani, alijiunga na Yanga Novemba 15, mwaka jana kisha kuondoka Februari 4, mwaka huu, akiiongoza timu hiyo katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara na kushinda yote, ikiwa ni ushindi wa asilimia 100, kikosini.
Ramovic katika Ligi Kuu alianza na ushindi wa (2-0) v Namungo FC, (3-2) v Mashujaa FC, (4-0) v Tanzania Prisons, (4-0) v Dodoma Jiji, (5-0) v Fountain Gate na (4-0) v Kagera Sugar, huku akifunga pia jumla ya mabao 22 na kuruhusu mawili.
Ramovic aliyeondoka kwa makubaliano ya pande mbili, mbali na Ligi Kuu Bara aliiongoza katika michezo sita ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akishinda miwili, sare miwili na kupoteza pia miwili, akifunga mabao matano na kuruhusu sita.
Kwenye Ligi ya Mabingwa, Yanga ilimaliza nafasi ya tatu kundi ‘A’ na pointi nane nyuma ya Al Hilal ya Sudan iliyomaliza na pointi 10, huku MC Alger ya Algeria ikimaliza na pointi tisa wakati TP Mazembe ya DR Congo ilimaliza nazo tano.
Katika Kombe la FA, Ramovic aliiongoza Yanga kwenye mchezo mmoja ambao ulikuwa wa hatua ya 64 bora, ambapo kikosi hicho chenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani kilishinda kwa mabao 5-0 dhidi ya Copco FC kutoka jijini Mwanza.
Kwa ujumla, Ramovic aliiongoza Yanga katika michezo 13 akishinda tisa, sare miwili na kupoteza miwili, akifunga mabao 32 na kuruhusu manane, huku kwenye Ligi Kuu akiiacha nafasi ya pili na pointi 42, nyuma ya Simba iliyokuwa na 43.
Ramovic alichukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyeondoka Novemba 15, mwaka jana ambaye aliiongoza timu hiyo katika michezo 10 ya Ligi Kuu Bara, ambapo alishinda minane na kupoteza miwili mfululizo iliyomfanya kutimuliwa ndani ya kikosi hicho.
Hatua ya Gamondi kufukuzwa ilijiri baada ya timu hiyo kupoteza michezo miwili mfululizo akianza na (1-0) v Azam FC na (3-1) v Tabora United na katika mechi hizo 10, Yanga ilikuwa ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zake 24.

Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia, Nasreddine Nabi aliyeipa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC), mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tangu ateuliwe kukiongoza kikosi hicho, Gamondi alikiongoza katika jumla ya michezo 40 ya Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2023-2024, hadi huu wa sasa wa 2024-2025, ambapo kwa ujumla kati ya hiyo alishinda 34, sare miwili na kupoteza minne.
Katika michezo hiyo 40 ya msimu uliopita na huu wa sasa, safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Gamondi ilifunga jumla ya mabao 85 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, ambapo kiujumla kwa misimu miwili alikusanya pointi zake 104.
Gamondi amechukua mataji matatu na timu hiyo akianza na Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023-2024 na kuifanya Yanga kufikisha jumla ya mataji yake 30, tangu mwaka 1965, akachukua Kombe la Shirikisho la FA, sambamba na Ngao ya Jamii mwaka 2024.