Fountain Princess yasaka tatu Mashujaa

Muktasari:
- Timu hiyo iko nafasi ya nane kwenye msimamo na katika mechi 14, imeshinda nne, sare mbili na kupoteza nane ikikusanya pointi 14.
KOCHA Mkuu wa Fountain Gate Princess, Camil Mirambo amesema wanahitaji kupata pointi tatu kwenye mechi ya leo dhidi ya Mashujaa Queens ili kuitafuta nafasi ya nne.
Timu hiyo iko nafasi ya nane kwenye msimamo na katika mechi 14, imeshinda nne, sare mbili na kupoteza nane ikikusanya pointi 14.
Ikipata ushindi kwenye mchezo huo, itasogea hadi nafasi ya sita na kufikisha pointi 17 na itaishusha Bunda yenye 15.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mirambo alisema safari yao ya kuitafuta nafasi ya nne inaanzia kwenye mchezo huo na anaamini watapata matokeo kutokana na ubora wa timu hiyo.
Aliongeza makosa ya washambuliaji wake ya kutotumia vyema nafasi wameyafanyia kazi mazoezini na kilichobaki ni dakika 90 za kuamua mechi hiyo.
"Tulikuwa na mapumziko ya mwezi mzima kujiandaa na tumeelekezana baadhi ya vitu hasa kwa washambuliaji kutumia nafasi moja wanayopata kugeuza kuwa bao," alisema Mirambo.