Ihefu yaishitua Yanga

Mbeya. Yanga inakamilisha mechi yake ya mwisho kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara leo kwa kuivaa Ihefu ugenini lakini kocha msaidizi wa kikosi hicho, Juma Mwambusi ameingiwa na hofu.
Mechi mbili mfululizo ambazo Ihefu imeshinda kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Sokoine Mbeya ndizo zimempa hofu Mwambusi, ambaye amekiri wanatakiwa kuikabili timu hiyo kwa tahadhari kubwa ili isiharibu rekodi yao.

Hadi sasa, Yanga ambayo ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 40 ndiyo timu pekee kwenye Ligi Kuu Bara ambayo haijapoteza mchezo wowote na inataka kupata ushindi leo ili imalize mzunguko wa kwanza kwa rekodi hiyo.
Yanga inatakiwa kuwa makini na Ihefu leo baada ya timu hiyo kuonyesha kiwango kikubwa katika mechi mbili zilizopita ilipoifunga Kagera Sugar mabao 2-1 kisha ikaichapa KMC bao 1-0.

Ihefu katika mechi 16 ilizocheza mpaka sasa imeshinda tatu tu huku ikitoka sare michezo minne na kupoteza tisa na iko nafasi ya 16 ikiwa na pointi 13.
Hata hivyo safu ya ulinzi ya Ihefu inatakiwa kujipanga leo dhidi ya Yanga ambayo katika mechi mbili zilizopita imepata ushindi wa zaidi ya mabao mawili ilipoichapa Mwadui mabao 5-0 na Dodoma Jiji mabao 3-1.
“Tunajua kuwa tunakutana na timu ya aina gani. Mechi itakuwa ngumu kwani Ihefu ana morali kwa sasa baada ya kushinda mechi mbili mfululizo, hivyo wapo tayari kuendelea kupambana na kutuzuia kupata pointi tatu,” alisema Mwambusi.

Katika mechi za jana, Gwambina ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Gwambina mjini Misungwi.
Mbeya City walianza mchezo vizuri na kufanikiwa kutangulia kwa bao la mapema lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Kibu Dennis, lakini wageni walishindwa kumalizia dakika moja ya mwisho na kuruhusu bao kusawazishwa.