Mashine mpya Yanga hii hapa

Muktasari:
MWANASPOTI imejiridhisha kwamba Yanga imeachana rasmi na dili la Edward Manyama wa Namungo pamoja na Dark Kabangu wa Motema Pembe.
MWANASPOTI imejiridhisha kwamba Yanga imeachana rasmi na dili la Edward Manyama wa Namungo pamoja na Dark Kabangu wa Motema Pembe.
Yanga ilikuwa inamuwinda straika mwili jumba, Kabangu mwenye mabao sita msimu huu lakini imeamua kuachana naye baada ya mchezaji huyo kudengua huku akitaka kuja mwakani itakapomalizika michuano ya Chan nchini Cameroon jambo ambalo Yanga hawawezi kulisubiri.
Kocha Cedrick Kaze amewekeza nguvu kwenye beki wa kati mzawa na kuachana na Manyama ambaye alikuwa anapigiwa debe na vigogo kadhaa wa Yanga. Za motomoto ambazo Mwanaspoti imejiridhisha nazo ni kwamba Yanga imerudisha nguvu kwa straika Mkongo, Idris Mbombo anayekipiga kwenye klabu ya Nkana ya Zambia lakini vilevile muda wowote kuanzia wiki hii watamalizana na beki wa kati ambaye ni mzawa na wamemfanya siri kwelikweli.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba mazungumzo na Mbombo yanaendelea vizuri na muda wowote dili hilo linaweza kukamilika ingawa huenda likawagharimu Yanga fedha nyingi kutokana na ubora wa mchezaji huyo ambaye akiingia kwenye boksi ni nadra kukosa kucheka na nyavu au kutoa asisti.
“Yule Kabangu tumeachana naye, straika ambaye tuko mbioni kumalizana naye ni Mbombo, vitu vingi tunaendelea naye vizuri na uhakika wa kumpata upo,” alidokeza mmoja wa viongozi wa Yanga.
Lakini akasisitiza pia Kocha Kaze amewaambia kwamba anataka beki wa kati mzawa hivyo watasajili wachezaji watatu tu kwenye dirisha dogo. Kwa maana ya Saido Ntibazonkiza ambaye yupo tayari Jangwani, Mbombo pamoja na beki mzawa ili kumuongezea changamoto Lamine Moro ambaye amekuwa na pancha za mara kwa mara

Dirisha dogo la usajili limefunguliwa Desemba 16 na litafungwa Januari 15 mwakani.
MSIKIE HERSI
Mjumbe wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Injinia Hersi Said licha ya kutotaka kuweka wazi kwasasa wanapambania mchezaji yupi, alisisitiza kwamba; “Tuna nafasi moja tu tumebakiza kwaajili ya dirisha dogo, kuna mchezaji kutoka nje ambaye anakuja lakini siwezi kusema jina maana bado hatujamalizana naye. Nafasi ni siri yetu lakini ni mchezaji mzuri sana.”

Yanga imechana pia jina la Muivory Coast Gbagbo Junior Magbi aliyetemwa na Wydad Casablanca ya Morocco akimpisha Saimon Msuva aliyesajiliwa.
KUHUSU NIYONZIMA
Hersi amefichua Haruna Niyonzima aliongezewa mkataba wa miezi sita tu; “Ni maelekezo ya kocha, pia mkataba wake umemalizika huku Ligi ikiwa haijaisha ndio maana tumemuongezea mpaka mwisho wa msimu.
“Bado kuna nafasi ya kufanya mazungumzo baada ya mkataba huu kumalizika na hata yeye mwenyewe anajua na sisi tunaelewa hilo.”

Niyonzima tangu alivyokuja kocha Kaze hajawa chaguo la kwanza katika kikosi chake huku habari zikidai kwamba Kocha huyo amempa changamoto mchezaji huyo ili ajitume na kurejesha morali yake na kuisaidia Yanga kuelekea kwenye mbio za ubingwa.