JKU inautaka ubingwa Muungano

Muktasari:
- JKU baada ya kufuzu fainali inatarajiwa kukabiliana na mshindi wa mchezo wa leo kati ya Zimamoto dhidi ya Yanga huku fainali hiyo ikipangwa kuchezwa kesho Alhamisi kwenye Uwanja wa Gombani.
JKU kutoka Unguja imetinga fainali ya Kombe la Muungano baada ya kuifunga Azam mabao 2-1, huku kocha wa timu hiyo, Haji Ali Nuhu akisema wanataka kubeba ubingwa.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema ushindi dhidi ya Azam ni mkakati waliojiwekea ili kutinga fainali.
Alisema ingawa mchezo unaofuata wa fainali utakuwa mgumu zaidi, lakini kutokana na maandalizi watakayoyafanya watahakikisha wanaondoka na ubingwa.
“Tunashukuru kwa kupata ushindi huu mgumu. Tulikuwa tumeshafungwa bao la mapema na wapizani wetu, lakini tukalisawazisha na tukaongeza tena. Ni jambo la faraja. Sasa tumeingia fainali, tunataka ubingwa,” alisema.
Nahodha wa timu hiyo, Fred Suleiman alisema bado hawajatosheka na ushindi huo, bali wataongeza nguvu zaidi katika mchezo wa fainali ili wabebe taji.
Alisema katika mchezo wa fainali watacheza kwa tahadhari na kuondoa upungufu uliyojitokeza katika hatu zilizotangulia kwa ajili ya kuhakikisha hawafanyi makosa.
JKU baada ya kufuzu fainali inatarajiwa kukabiliana na mshindi wa mchezo wa jana kati ya Zimamoto dhidi ya Yanga huku fainali hiyo ikipangwa kuchezwa kesho Alhamisi kwenye Uwanja wa Gombani.