Nini kinachoisumbua Azam FC?

Muktasari:
- Msimu wa 2024/25 umegeuka kuwa ‘mwaka wa shetani’ kwa matajiri wa Chamazi waliowekeza mamilioni, lakini wameambulia patupu kila shindano.
NI msimu ambao mashabiki wa Azam FC wanataka umalizike haraka. Kuanzia mapema katika Ngao ya Jamii hadi sasa ligi ikielekea ukingoni, kila tumaini limekuwa kama jua la asubuhi lililofunikwa na mawingu.
Msimu wa 2024/25 umegeuka kuwa ‘mwaka wa shetani’ kwa matajiri wa Chamazi waliowekeza mamilioni, lakini wameambulia patupu kila shindano.
Katika fainali ya Ngao ya Jamii iliyofanyika Agosti 2024, Azam ilipoteza kwa kipigo cha mabao 4-1 mbele ya Yanga. Huo ulikuwa ni mwanzo mbaya msimu huu.

Haikuchukua muda mrefu kuhalalisha tahadhari hiyo. Mwezi huohuo, Azam ilicheza dhidi ya APR ya Rwanda kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali. Ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar haukutosha kwani ilipoteza ugenini kwa mabao 2-0 Uwanja wa Amahoro, hivyo kuondolewa kwa jumla ya mabao 2-1.
Matokeo hayo yaliulazimu uongozi kuchukua uamuzi mgumu. Youssouph Dabo, aliyekuwa kocha mkuu aliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Rachid Taoussi aliyekuwa na matumaini ya kuifufua Azam.
Lakini badala ya neema, Taoussi alipambana na misukosuko ileile. Mwezi Machi, mwaka huu, Azam ilikutana na Mbeya City katika Kombe la FA. Ikiwa na wachezaji wa daraja la juu na kocha mwenye uzoefu, iliondolewa hatua ya 16 bora na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship kupitia mikwaju ya penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.

Kwa mara nyingine, mashabiki walibaki na huzuni, wakijiuliza “ni nini hasa kinaendelea Chamazi?” Hali hiyo ikaongeza presha kwa benchi la ufundi, wachezaji na hata viongozi.
Mechi za Ligi Kuu Bara nazo hazikutoa ahueni. Licha ya kuonyesha mchezo wa kuvutia katika vipindi fulani, matokeo hayakuwa rafiki. Azam walipoteza michezo muhimu dhidi ya Yanga (2-1) na Singida Black Stars (1-0) wakijikuta wakiwa nyuma ya Simba na Yanga kwa tofauti kubwa ya pointi.
Kwa sasa, Azam inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 54 baada ya michezo 27. Hali hiyo inaweka presha kwenye michezo mitatu iliyosalia dhidi ya Dodoma Jiji, Tabora United na Fountain Gate, hasa kwa kuwa na pointi moja mbele ya Singida.

Hofu ni kuwa kama Azam itaendelea na mwenendo huo wa kutofanya vizuri inaweza kuporomoka hadi nafasi ya nne, jambo ambalo litazidisha uchungu kwa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo ambao walitegemea kuona angalau kombe moja likienda Chamazi.
Azam pia iliingia kwenye Kombe la Muungano ikiamini huo ungeweza kuwa mkombozi. Mchezo wa kwanza ilishinda bao 1-0 dhidi ya KMKM, lakini ilijikuta ikifungashwa virago katika hatua ya nusu fainali kwa kufungwa 2-1 na JKU ya Zanzibar.
Winga wa Azam, Idd Seleman ‘Nado’ alionekana kuvunjika moyo akisema: “Naomba mashabiki watusamehe, tumejisikia vibaya kuondolewa kwenye mashindano. Niliamini kuwa tutachukua ubingwa wa Muungano. Tulichojifunza ni kutodharau timu yoyote.”

Kauli hiyo ilitafsiriwa na wengi kama kilio cha mchezaji aliyechoka kuona ndoto ikipasuka mara kwa mara mbele ya macho yake.
Katika mashindano matano ambayo Azam imeshiriki msimu huu Ngao ya Jamii, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la FA, Kombe la Muungano na Ligi Kuu yote imeambulia patupu.
Hali hiyo imetoa taswira mbili; kwanza ni kwamba uwekezaji mkubwa hauwezi kufanikisha mafanikio bila mipango sahihi ya kiufundi, pili kuna hitaji la mageuzi makubwa ndani ya klabu.
Swali kubwa sasa ni kama Rachid Taoussi ataendelea kuaminiwa kwa msimu mwingine licha ya kushindwa kuibeba timu msimu huu.

Nyota wa zamani wa Yanga SC, Credo Mwaipopo akizungumzia hali inayopitia Azam alisema: “Tatizo la nadhani ni la kisaikolojia ndani ya timu. Wana kila kitu, miundombinu na usajili mzuri lakini hawana roho ya ushindi. Wachezaji hawachezi kama watu wanaoumia kwa ajili ya klabu.
“Timu inapofika hatua ya mashindano makubwa utulivu unawatoka. Hili ni jambo la ndani zaidi ya benchi la ufundi. Wanaweza kubadilisha kocha mara 10 lakini kama hawawezi kujenga utambulisho wa kupambana kama timu kubwa wataendelea kulia kila msimu.”
Kocha wa zamani wa Gwambina na Mtibwa Sugar, Mohamed Badru amewataka waajiri wake hao wa zamani kwenye timu za vijana kujipa muda na kutafuta njia nzuri za kukabiliana na hili.
“Kiukweli Azam inawatu wanaoupenda sana mpira. Sasa huu ni wakati wa kutafuta namna nzuri ya kubadilisha hiki ambacho kinaendelea, naamini wanaweza kuifanya klabu hiyo kuwa tishio,” alisema.
Hata hivyo, bado Azam wana nafasi ya kumaliza katika nafasi ya tatu, ambayo inaweza kuwapa nafasi ya kushiriki tena mashindano ya kimataifa msimu ujao, endapo watatumia michezo mitatu iliyobaki kama fursa ya kujirekebisha na kujenga morali mpya.
Kwa mashabiki, bado matumaini hayajakufa. Lakini kwa viongozi wa Azam FC, huu ni wakati wa kufanya kazi zaidi ya kuzungumza. Mwaka wa Shetani haumaanishi mwisho wa dunia lakini ni onyo kali kuwa mabadiliko hayakwepeki.