Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kaseja afunguka ishu ya kuuza mechi Simba

TATHMINI za wadau wa soka, zinamtaja Juma Kaseja kama kipa bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania ndani ya miaka 15. Amezichezea klabu za Moro United, Simba, Yanga, Kagera Sugar, Mbeya City na KMC.

Anatajwa kama mchezaji mwenye nidhamu kubwa ndani na nje ya uwanja kuanzia kwenye mazoezi, nidhamu ya fedha mpaka kujituma katika mechi.

“Mpira hauna njia ya mkato, ili ucheze mpira lazima ujiandae, maandalizi ya mpira ni mazoezi, lazima ufanye mazoezi kwa bidii na ikiwezekana utenge muda wa kufanya mazoezi ya ziada, mbali na yale wanayotoa walimu, na hiyo ndio siri kubwa iliyonifanya mimi leo kuwa kwenye kiwango bora mpaka sasa,” anasema kimpa huyo wa KMC ya Kinondoni.

ISHU YAKE NA MAXIMO

Kuna nyakati Kaseja ilidaiwa kwamba alikuwa haziivi na Kocha wa Taifa Stars, Mbrazil, Marcio Maximo mwaka 2006-2010.

“Kwa kipindi kile, nilikuwa kwenye kiwango bora kabisa na kulikuwa kuna ushindani mkubwa kati yangu na golikipa aliyekuwa anamuanzisha (Ivo Mapunda) kwenye timu.”

“Hivyo kuna baadhi ya watu waliokuwa wanatamani mimi nikicheza golini, hivyo lile shinikizo la nje ya uwanja ndio ambalo lilileta mpasuko kati yangu na mwalimu, lakini mimi na mwalimu wala hatukuwahi kugombana au kukwaruzana,” anasema huku akiongeza kuwa hakufurahia kitendo cha Mapunda kufungwa mabao manne kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Senegal kama ilivyotafsiriwa kipindi kile.

Kaseja anasema kuna makipa wengi ambao yeye kwa mtazamo wake wana uwezo mkubwa wa kuja kuwa bora zaidi na tegemeo, ambao wanaweza kupiga hatua kubwa zaidi ya aliyopiga yeye.

“Kikubwa waendelee na jitihada zao na kusikiliza kile watakachokuwa wanashauriwa , wasichague watu wa kuwaambia, ikiwa kwa wadogo hata kwa wakubwa na hata wale ambao hawapo kwenye tasnia ya mpira maana kila mtu ana jicho lake la kuona, nina imani wakijumuisha na jitihada zaidi watafika mbali pengine zaidi ya hapa nilipo mimi,” anasema.

MECHI HII HAISAHAU

Simba na Ismailia ya Misri, ambao ulikuwa ni mchezo wa hatua ya makundi ya mashindano ya klabu bingwa Afrika.

Katika mchezo huo Simba iliambulia kichapo cha mabao 2-1 chini ya Kocha James Siang’a (marehemu) huku bao pekee la Simba akifunga Emmanuel Gabriel ambaye alipokea pasi kutoka kwa Boniface Pawasa.

“Wakati ule nakumbuka, nilikuwa kwenye kiwango bora kabisa kwenye maisha yangu ya soka, licha ya kupoteza bado inabaki kuwa mechi ambayo naikumbuka ziku zote,” anasema na kuongeza kuwa alisomea ukocha dhumuni lake likiwa kutaka kujua na kutambua mazingira ya mpira halisi, ikiwa ni pamoja na aina ya mazoezi ambayo wamekuwa wanapewa yanasaidia kwenye nini hasa.

USAJILI WAKE WA KWANZA

“Nakumbuka pesa yangu ya kwanza ambayo niliipata baada ya kusaini Moro United, niliitumia kufanya nauli kwenda kwenye msiba wa baba yangu na kiasi kilichobakia nikamuachia mama yangu ambacho alikitumia kuendeshea gharama za 40 ya mzee.”

IMANI ZA KISHIRIKINA

“Nimetangulia kusema kuwa Mungu ndiyo kila kitu, siamini kama ukiwa na imani za kishirikina unaweza ukawa bora katika maeneo mengi.”

Kaseja anaongeza kwa kusema kuwa hata hao waganga pia wamekuwa na watoto wao ambao wanacheza mpira, lakini bado wanaendelea kucheza tu hapa hapa, ingekuwa mpira unaendana na imani hizo wangewafanyia ili waende huko Real Madrid ama Manchester United.

SIMBA NA YANGA KUNA TOFAUTI?

“Kwa Simba na Yanga tofauti ni zile rangi zao na itikadi zao na viongozi ni wale wale, japokuwa niliishi muda mrefu Simba, lakini kiuhalisia hakuna tofauti,” anasema.

Kutoka Simba kwenda Yanga; “Ulikuwa ni uamuzi mgumu kwakuwa watu wengi hawakutegemea, lakini siku ya mwisho tunaangalia maisha kwakuwa mpunga ulikuwa mrefu, pia nakumbuka mpaka naingia chumba cha kusaini mkataba na Yanga, kuna baadhi ya viongozi wa Simba waliniambia kwamba nisaini tu.”

“Dau ni lilikuwa kubwa na wao wasingeweza kunipa pesa kama ile, kwahiyo nilipata baraka zao zote, japo iliwauma baadhi ya watu, lakini maisha yanaendelea,” anasema.

KIPIGO CHA YANGA

Akiwa Yanga kwenye mechi ya Mtani Jembe alifungwa na Simba baada ya kunyang’anywa mpira alipojaribu kumpiga chenga Awadh Juma, ambaye aliunasa mpira na kufunga katika lango tupu.

“Kwenye ile mechi nakumbuka ilikuwa ndio nacheza kwa mara ya kwanza baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, takribani miezi mitano hivi sikuwa nimecheza mechi yoyote.”

“Wakati huo ndio nilikuwa nimesajiliwa kutoka Simba, makosa kama yale walishafanya magolikipa wengi na wakubwa duniani, na mimi bahati nzuri kwenye maisha yangu ya mpira huwa siogopi kukosea,” anasema.

“Mbuyu Twitte, Haruna Niyonzima na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ndio walikuwa wachezaji wa kwanza waliokuja kuniambia kwamba hiyo imeisha na makosa kwenye mpira yapo na wala usikae tena ukafikiria,” anaongeza.

“Nakumbuka pia wakati nasaini kwa mara ya kwanza Moro United kwenda kucheza Ligi Kuu, ndio siku hiyo nilipopata taarifa za kifo cha baba yangu, hili tukio kamwe sitokuja kulisahau na ndio ikasababisha nichukue ile pesa yangu ya usajili na kuitumia kama nauli,” anasema.

KUUZA MECHI

“Watu wanasema kuwa Kaseja ni mchawi ndo maana hadi leo anacheza, Kaseja anauza mechi lakini hadi leo bado ninacheza, mimi naamini ukiuza mechi, mfano ukiwa Simba ukiwauzia Yanga, Simba watajua tu kwasababu maisha ya viongozi hawa klabu hizi nje ya uwanja ni marafiki wanakaa meza moja, wanakunywa na wanaongea lugha moja, “ anasema.

“Nili-potoka Simba kwenda Yanga baada ya muda nikatoka tena Yanga kurudi Simba, siamini kwamba Simba wangekubali kunirudisha tena kwenye timu yao kama wakati wanajua kuwa nilikuwa nawauzia mechi wakati nipo Yanga.

“Kwahiyo mimi nadhani hivyo ni vitu ambavyo vipo tu mtaani na huwezi kuzuia watu kuongea, naamini kama ningekuwa na tabia hiyo, sidhani hata kama leo hii ningekuwa nacheza mpira.

“Kama unavyojua nimepita klabu nyingi, na bahati nzuri hawa viongozi karibia wote ni marafiki kwahiyo wangekuwa wanaambiana kwamba mimi nina tabia za kuuza mechi nisingekuwa nacheza hadi leo,” anasema.

MECHI NGUMU

“Watu wanaweza wakashangaa, lakini mechi ngumu kwangu ilikuwa ni dhidi ya Ethiopia, tulikuwa tumeongezwa watu wachache sana, kutoka timu ya wakubwa kwenda kushirikiana na timu ya wachezaji wa timu za vijana ambao ndio walikuwa wengi, ulikuwa ni mchezo mgumu kwanza kutokana na baridi halafu mashabiki walikuwa ni wengi kweli kweli.

“Ilifikia mahali hadi Kapteni Mexime wakati ule akanifuata na kuniambia, hawa jamaa wanahitaji kupata hata bao moja ili watulize ile presha, maana walikuwa wanashambulia muda wote katika dakika 45 za kwanza, na mimi pia nilikuwa bora sana katika mchezo huo,” anasema.

Kaseja anasema mchezo huo walipoteza kwa kufungwa bao moja, lililoingia kupindi cha pili na hii ilitokana na wao kuwa pungufu baada ya kadi nyekundu aliyoipata Said Sued katika dakika ya saba.

“Ulikuwa ni mchezo mgumu hadi kapteni akaniambia kuwa kwa kasi waliyokuwa nayo wangepata hata bao moja wangetulia, lakini mimi pia nilikuwa kwenye kiwango bora kabisa,” anaongeza.

Unajua ni nini kimetokea kati yake na Yanga?

Usikose mwendelezo wa makala hii kesho Jumatano.