Prime
Kila bao, Mpanzu anampa kocha laki

Muktasari:
- Nyota huyo anayemudu kucheza wingi zote mbili, aliwekeana ahadi na kocha Mohamed Mrishona ‘Xavi’ kwamba atakuwa akimlipa Sh100,000 kila atakapoifungia Simba mabao baada ya awali kuanza kwa kusuasua na kwenda kujifua kwa jamaa huyo maarufu, ikiwa ni kama shukrani.
ELLIE Mpanzu amewafunga mdomo wale wote waliokuwa wakimpopoa wakati alipoanza kuitumikia Simba iliyomsajili kupitia dirisha dogo, huku mabao aliyoanza kuyafunga akiwa na kikosi hicho yameanza kulipa kwa kocha binafsi wa mazoezi wa kiungo mshambuliaji huyo kutoka DR Congo.
Nyota huyo anayemudu kucheza wingi zote mbili, aliwekeana ahadi na kocha Mohamed Mrishona ‘Xavi’ kwamba atakuwa akimlipa Sh100,000 kila atakapoifungia Simba mabao baada ya awali kuanza kwa kusuasua na kwenda kujifua kwa jamaa huyo maarufu, ikiwa ni kama shukrani.
Mpanzu anafanya mazoezi binafsi chini ya kocha Xavi na walianza na programu ya kuuweka mwili wepesi, ufiti na namna ya ulengaji wa mipira kwenda golini, jambo ambalo staa huyo anaona linazaa matunda.

Mwanaspoti lilimtafuta kocha Xavi, ili kuthibitisha jambo hilo, naye alisema ni kweli lakini sio makubaliano ya lazima sana, isipokuwa ni mchezaji mwenyewe aliamua kumshukuru kwa njia hiyo.
Mpanzu alianza kufunga Februari 11, 2025 Uwanja wa KMC dhidi ya Tanzania Prisons 0-3 akiweka bao la pili la Simba, kisha akafunga bao la kwanza katika sare ya 2-2 dhidi ya Azam Feb 24, 2025 na bao la kwanza katika ushindi wa 6-0 mbele ya Dodoma Jiji mchezo uliopigwa Machi 14, 2025.
Xavi aliliambia Mwanaspoti, alianza kuonja matunda ya kazi yake kwa Mpanzu kuanzia mechi ya Dodoma Jiji, anachosisitiza ni staa huyo kufanya kwa upendo.
“Nimeshangaa umezipata wapi taarifa hizo, ila niliweke vizuri, Mpanzu nafanya kazi naye klabu moja anacheza timu ya wakubwa, mimi nafundisha Simba B. Tunachofanya ni mazoezi binafsi ambayo kwa mtazamo wake anaona yanamsaidia,” alisema Xavi na kuongeza;
“Kwanza Mpanzu huwa ananiita baba, licha ya kuwa kocha kijana ila ni mdogo sana kwangu, baada ya kufunga dhidi ya Dodoma Jiji alikuja kuniambia baba, chukua hii Sh 100,000 na kila nikifunga nitakuwa nafanya hivyo.”
Xavi aliongeza kuwa, licha ya jina la Mpanzu kutajwa kwa ukubwa kulingana na kazi anayoifanya kwa sasa, anajishusha na kuzidisha mazoezi ili kila anapoingia kucheza mechi awe na kitu tofauti.
“Kwa sasa kitu ambacho tunakifanyia kazi katika programu yetu ni mashuti ya kulenga lango ili aweze kufunga mabao mengi zaidi na anapenda kusikiliza na kuyafanyia kazi kwa bidii maelekezo anayopewa,” alisema Xavi na kuongeza;
“Anatamani kazi yake iwe na nguvu kuliko yeye kuzungumza sana na huwa anasema kila jina lake linapokuwa kubwa anapata deni la kufanya kazi kwa ukubwa zaidi.”

Mpanzu aliyesajiliwa na Simba akitokea AS Vita ya DR Congo, si pekee anayefundishwa na Xavi. Wengine ni Simon Msuva (Al-Talaba SC), Abdi Banda (Dodoma Jiji), Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (Huru), Feisal Salum (Azam FC), nk.
Wapo pia Wazir Junior (Dodoma), Opah Clement (Jul¡rez), Enekia Lunyamila (Mazaltan), Diana Msewa (Trabzonspor) na Joyce Lema wa JKT Queens.