Kim Poulsen mitatu tena

SHIRIKISHO la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limemteua Kim Poulsen, raia wa Denmark kuwa kocha wa timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars).
Kim amesaini mkataba wa miaka mitatu kuifundisha Taifa Stars ambayo hivi sasa iko katika kinyang'anyiro cha kutafuta nafasi ya kucheza Fainali za AFCON pamoja na Kombe la Dunia zitakazofanyika 2022 katika nchi za Cameroon na Qatar.
Kocha huyo anachukua nafasi ya Etienne Ndayiragije ambaye hivi karibuni alifikia makubaliano na TFF kuvunja mkataba wake.
Poulsen aliwahi kuinoa Stars kati ya 2012-2013 ambapo kabla ya kupewa nafasi hiyo alikuwa kocha wa timu za Vijana Tanzania.
Kim pia alipokuwa mshauri wa maendeleo ya soka la Vijana, aliiwezesha Serengeti Boys kushiriki Fainali za Afcon zilizofanyika nchini Gabon 2017, kikosi kikiwa chini ya kocha Bakari Shime.