Kiungo JKT aziingiza vitani Mbeya City, Mtibwa

Muktasari:
- Mtibwa na Mbeya City zimepanda daraja msimu huu kutokea Ligi ya Championship na tayari zimeanza maandalizi ya kufanya usajili kwa vikosi vya msimu ujao wa Ligi Kuu na zinaelezwa kuwa kila moja imekuwa ikimpigia hesabu kiungo huyo wa zamani wa Yanga.
KIUNGO mshambuliaji anayemaliza mkataba alionao na JKT Tanzania, Maka Edward ameziingiza vitani klabu zilizorejea Ligi Kuu Bara msimu ujao, Mtibwa Sugar na Mbeya City baada ya mwenyewe kuchomoa ofa ya kwenda mafunzoni katika kikosi cha sasa.
Mtibwa na Mbeya City zimepanda daraja msimu huu kutokea Ligi ya Championship na tayari zimeanza maandalizi ya kufanya usajili kwa vikosi vya msimu ujao wa Ligi Kuu na zinaelezwa kuwa kila moja imekuwa ikimpigia hesabu kiungo huyo wa zamani wa Yanga.
Mwanaspoti imepenyezewa kwamba City imeweka ofa kubwa kuliko Mtibwa, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa mchezaji huyo kutua mkoani Mbeya.
Chanzo cha ndani kilisema licha ya ofa ambayo mchezaji alipewa na JKT Tanzania ya kwenda kusomea kozi za kijeshi, alionekana kuitolea nje na kutamani kwenda kupata changamoto katika timu nyingine.
"Kama mambo yatakwenda sawa City ina nafasi kubwa endapo ofa za timu nyingine hazitakuja mezani kwake, tofauti na Mtibwa ambayo dau lake la usajili siyo kubwa," kilisema chanzo hicho na kuongeza;
"Nje na pesa Maka anatamani kusajiliwa na timu ambayo atakuwa anapata nafasi ya kucheza, ili kiwango chake kuwa juu ambapo itakuwa faida kwake kusajiliwa kwa dau kubwa."
Mbali na Yanga, Maka amewahi kucheza soka la kulipwa huko Morocco katika klabu za Moghreb Tetouan na Mat Reserve kisha kuitumikia Geita Gold kabla ya msimu huu kuibukia JKT Tanzania ambapo hadi sasa ameifungia bao moja tu katika Ligi Kuu.