Kocha Polisi Tanzania akubali yaishe

Muktasari:
- Timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya 10 na pointi zake 31, baada ya kushinda michezo minane, sare saba na kupoteza 12, kati ya 27, hivyo hata ikishinda mechi zake zote tatu zilizobaki haiwezi kuingia nne bora ili kucheza mtoano 'play-off'.
KOCHA wa maafande wa Polisi Tanzania, Mussa Rashid amesema timu hiyo inapigania heshima ya kumaliza vizuri msimu huu, baada ya malengo waliyojiwekea ya kupigania nafasi nne za juu kukwama, kutokana na gepu la pointi dhidi ya washindani wake.
Timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya 10 na pointi zake 31, baada ya kushinda michezo minane, sare saba na kupoteza 12, kati ya 27, hivyo hata ikishinda mechi zake zote tatu zilizobaki haiwezi kuingia nne bora ili kucheza mtoano 'play-off'.
"Malengo yetu yalikuwa ni kumaliza ndani ya nafasi nne za juu ili tucheze michezo ya play-off, hilo limeshindikana kwa sababu ya ushindani uliokuwepo na wapinzani wetu, kwa sasa tunapambana kumaliza kwa heshima mechi zilizobakia," alisema.
Kocha huyo wa zamani wa timu za African Sports na Green Warriors, amejiunga na kikosi hicho akitokea Biashara United ya Musoma, ambako ameungana kikosini na Bernard Fabian aliyeanza nacho msimu huu, ingawa kwa sasa ameteuliwa msaidizi wake.
Kikosi hicho kilishuka daraja msimu wa 2022-23, kikimaliza katika nafasi ya 15 kwa pointi zake 25, baada ya kucheza michezo 30 ya Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hiyo kilishinda sita, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao yake 25 na kuruhusu 54.