Kocha Singida Black Stars amsifu Sowah

Muktasari:
- Singida Black Stars ipo nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 24 wameshinda 14, sare tano na kupoteza mechi tano, wamefunga mabao 35 wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 19.
BAADA ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma amesifu juhudi zilizooneshwa na wachezaji wake katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara.
Mbali na kupongeza wachezaji kwa ujumla, Ouma ameonekana kufurahishwa zaidi na mwendelezo mzuri wa mshambuliaji wa timu hiyo, Jonathan Sowah ambaye alifunga bao moja na kufikisha manane katika mechi nane alizocheza tangu atue hapo dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15 mwaka huu.
“Kazi ya mshambuliaji ni kutumia kila nafasi anayoipata, hicho ndio anachokifanya Sowah, ni mchezaji ambaye hawezi kukuacha salama akiwa ndani ya 18, nafurahishwa na muendelezo wake na mbali na kujipambania mwenyewe ameweza kutengeneza usawa mzuri eneo la ushambuliaji sasa nafasi nyingi zinatumika kisawasawa, papara hakuna,” alisema na kuongeza.
“Ujio wa Sowah kwa asilimia kubwa umetuliza safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa inaongozwa na Elvis Rupia ambaye ndiye kinara wa upachikaji mabao, naamini kama wote wataendelea kufunga kila wanapopata nafasi basi tunaweza kumaliza msimu tukiwa na wastani mzuri wa pointi na mabao ukichanganya na yanayofungwa na wachezaji wengine.”
Ushindi huo umeiwezesha Singida Black Stars kukusanya pointi zote sita msimu huu kutoka kwa Fountain Gate ikiifunga mabao matano baada ya mzunguko wa kwanza kushinda 2-0 na wa pili ikishinda 3-0 na kuifanya timu hiyo kuendelea kubaki nafasi ya nne kwenye msimamo ikifanikiwa kukusanya pointi 47 kwenye mechi 24.
“Kila mchezaji ametimiza wajibu wake ipasavyo hata washambuliaji wangu walikuwa makini kutumia nafasi kipindi cha kwanza, hii inaonyesha namna tunavyozidi kuimarika na kupambania malengo yetu ya msimu huu ambayo ni pamoja na kuipeleka timu hii kimataifa,” alisema Ouma.
Singida Black Stars ipo nafasi ya nne kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 24 wameshinda 14, sare tano na kupoteza mechi tano, wamefunga mabao 35 wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 19.