Mabula anaitaka namba Taifa Stars

Muktasari:
- Mara ya mwisho kuwa katika kikosi timu ya taifa ilikuwa Februari 22, 2021 kwenye mashindano ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana U-20 dhidi ya Morocco akikaa benchini.
KIUNGO wa Kitanzania, Alphonce Mabula ni miongoni mwa nyota wanaofanya vizuri kwenye kikosi cha Shamakhi FC na mwenendo huo inaonyesha ni wazi anaitaka nafasi kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Mara ya mwisho kuwa katika kikosi timu ya taifa ilikuwa Februari 22, 2021 kwenye mashindano ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana U-20 dhidi ya Morocco akikaa benchini.
Hata hivyo, eneo analocheza wapo nyota ambao wamekuwa wakiitwa na kucheza mara kwa mara,
Himid Mao, Adolf Mtasingwa, Novatus Miroshi na wengine.
Tangu amejiunga na chama hilo msimu huu akitokea FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu Serbia amekuwa na wakati mzuri wa kuanza na kuonyesha kiwango bora.
Hadi sasa Mabula amecheza mechi 13 kwa dakika 888 akifunga mabao mawili na asisti moja chama hilo likiwa nafasi ya saba kwa pointi 35.
Chama hilo linashiriki Ligi Kuu ya Azerbaijan na Mabula amejiunga kwa mkataba wa miezi sita wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja.