Mambo ya ndani yaendeleza kicheko

Muktasari:
- Katika mashindano hayo timu tisa zinashiriki zikiwa zimepangwa katika makundi mawili huku la A likiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ujenzi, Maliasili na Singida MC ilhali lile la B lina Tanesco, NSSF, Dodoma Jiji na Uchukuzi.
TIMU ya kikapu ya Wizara ya Mambo ya Ndani imeinyoosha Maliasili kwa pointi 113-34 katika mashindano ya Mei Mosi yanayoendelea katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mwaja mjini Singida.
Katika mashindano hayo timu tisa zinashiriki zikiwa zimepangwa katika makundi mawili huku la A likiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ujenzi, Maliasili na Singida MC ilhali lile la B lina Tanesco, NSSF, Dodoma Jiji na Uchukuzi.
Wizara ya Mambo ya Ndani inayowakilishwa na wachezaji wengi wa timu ya Polisi itakayoshiriki Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), ilionyesha kiwango bora katika mchezo dhidi ya Maliasili na kufanikiwa kuzoa pointi hizo.
Mchezo huo kwa Mambo ya Ndani ni wa pili kushinda kwani ule wa kwanza iliishinda TRA kwa pointi 77-39.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa simu kutoka Singida, nyota wa Mambo ya Ndani, Augustino Kassim alisema uzoefu wao BDL ndiyo uliochangia kupata ushindi huo mkubwa.
Kassim anachezea Polisi alisema mashindano hayo pia ni mojawapo wa maandalizi kwa timu yake katika ligi hiyo mwaka huu.