Maximo noma, amshitukia Jaja

Kikosi cha timu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam kikifanya mazoezi
Muktasari:
Kama kuna shabiki wa timu pinzani na Yanga alikwenda katika mazoezi hayo ya jana Jumatano asubuhi kujaribu kuiba mbinu za mshambuliaji huyo mwenye mwili mkubwa uliojengeka kimazoezi, basi amepigwa chenga ya mwili kutokana na ratiba maalumu ambayo Mbrazili mwenzake, Maximo, amempangia Jaja.
MSHAMBULIAJI Mbrazili, Genilson Santana Santos ‘Jaja’ (pichani), ameanza rasmi kujifua katika kikosi cha Yanga, lakini benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Marcio Maximo ‘The Chosen One’ likamficha kwa kumzuia kugusa kabisa mpira.
Kama kuna shabiki wa timu pinzani na Yanga alikwenda katika mazoezi hayo ya jana Jumatano asubuhi kujaribu kuiba mbinu za mshambuliaji huyo mwenye mwili mkubwa uliojengeka kimazoezi, basi amepigwa chenga ya mwili kutokana na ratiba maalumu ambayo Mbrazili mwenzake, Maximo, amempangia Jaja.
Jaja bado hajasaini mkataba na Yanga, lakini anatarajia kufanya hivyo muda wowote baada ya Maximo na viongozi kuridhishwa na uwezo atakaouonyesha mazoezini.
Katika mazoezi hayo, kinyume na matarajio ya wengi, Maximo alimfua nyota huyo kwa dakika 45 ambazo Jaja alizitumia kwa kukimbia tu kabla ya kuagizwa anyooshe misuli na viungo na kutulia ikimaanisha siku yake ya kwanza Yanga iliishia hapo.
Awali Jaja aliyeonekana kutamani kuuchezea mpira mara baada ya kumaliza kukimbia katika kupasha misuli akiwa na nyota wenzake wa kikosi kizima, alifuatwa na Msaidizi wa Maximo Leonardo Neiva ambaye alimuamuru kuendelea kukimbia huku wenzake wakigeukia mazoezi ya ufundi yanayohusisha kuchezea mpira.
Akizungumza na Mwanaspoti, Neiva alisema, walipanga kumzuia Jaja kuanza na mazoezi ya pamoja na wenzake kutokana na kugundua mambo makuu mawili kupitia mshambuliaji huyo ambayo ni kumpa muda wa kumpumzisha baada ya safari ndefu halafu ameongezeka uzito hivyo kuhitaji mazoezi maalumu ya kumpunguza.
Neiva alisema jambo la kwanza, Jaja alionekana kutohitaji kuharakishwa katika kufanya mazoezi makali kutokana na safari yake ndefu kutoka kwao Brazil mpaka Tanzania ambapo alitumia saa 18 angani. Alisema kitaalamu ingeweza kuwa na athari kiafya endapo angefanya mazoezi ya nguvu na timu nzima.
“Ametumia saa 18 kutoka Brazil hadi hapa Tanzania, saa hizi ni tano kutoka alipoanzia safari ya kuja hapa na saa nyingine ni zile alizotumia kutoka mahali alipokuwa nchini Brazil hadi alipoanzia safari ya kuja Tanzania. Hii ni safari ndefu kwa haraka tumepiga hesabu ametumia saa 18 katika safari hiyo,” alisema Neiva.
“Hata jana (juzi Jumanne) alivyofika alitaka tukafanye mazoezi, lakini tulimkataza na hakufurahia hilo. Hata sasa ukimwangalia ni mtu anayetamani kuingia uwanjani, lakini hatutaki kufanya makosa hayo kwani anaweza kuumia na baadaye tukamuweka katika wakati mgumu.”
Jambo la pili ni kwamba Jaja amebainika kuongezeka uzito kwa kilo mbili kutokana na kuwa katika mapumziko ya ligi nchini kwao ambayo ilimalizika tangu mwezi Mei .
“Sasa amepangiwa ratiba maalumu ya kupunguza uzito wa mwili wake ili aweze kuwa sawa na kiwango cha nyota wa kikosi hicho ambao daraja lao la kiwango cha mazoezi lipo juu.
“Tumeshapanga kila kitu kuhusu anachotakiwa kufanya kuanzia sasa, kwanza ukianza na kesho (leo Alhamisi) anatakiwa kufanya mazoezi kama leo (jana) kwa asilimia 70 ambazo Ijumaa tutamuongezea kwa asilimia 10 hivyohivyo Jumamosi ataongezewa 10 zingine na Jumatatu ya wiki ijayo tunataraji atakuwa katika kiwango tunachokitaka.”
Akizungumzia hilo, Maximo alisema hana haraka na Jaja kwani ni aina ya straika anayemtaka ambapo sasa wanataka kumjenga kwanza kabla ya kuanza kuonyesha uwezo wake anaoujua.
“Achilia mbali Jaja, kila mchezaji namuamini sana hapa Yanga. Jaja namjua vizuri sina presha naye nipe siku tatu utajua ninachokiamini, kidogokidogo tutafika,” alisema Maximo.
Apewa jezi namba 15
Unaikumbuka jezi namba 15? Ilikuwa inavaliwa na mchezaji gani msimu uliopita? Jibu rahisi ni Shaaban Kondo ambaye hakufanikiwa kucheza hata mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara msimu huo kabla ya kuachwa katika dirisha la usajili msimu huu, lakini uongozi wa Yanga umecheka na kusema Jaja ataisafisha jezi hiyo.