Mbeya Kwanza, Polisi Tanzania katika vita ya Ligi Kuu
Muktasari:
- Timu hizo zinakutana leo baada ya Polisi Tanzania kumaliza nafasi ya tatu na pointi 66 katika Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026, huku Mbeya Kwanza yenye maskani yake Tabora ikimaliza nafasi ya nne na pointi 61.
VITA ya kuisaka tiketi ya kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2026-2027 kupitia Play-Off, inaanza leo kati ya wenyeji Mbeya Kwanza dhidi ya Polisi Tanzania, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Timu hizo zinakutana leo baada ya Polisi Tanzania kumaliza nafasi ya tatu na pointi 66 katika Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026, huku Mbeya Kwanza yenye maskani yake Tabora ikimaliza nafasi ya nne na pointi 61.
Katika mechi mbili za msimu huu wa 2025-2026 ndani ya Ligi ya Championship, kila timu imeshinda nyumbani kwake, ikianza Mbeya Kwanza iliyoshinda mabao 4-2, Januari 11, 2026 kisha raundi ya pili kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi mkoani Kilimanjaro, Polisi ikashinda bao 1-0, Juni 14, 2026.
Mbeya Kwanza iliyouzwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi msimu uliopita wa 2024-2025, ilishuka daraja Ligi Kuu Bara msimu wa 2021-2022, baada ya kumaliza mkiani mwa nafasi ya 16 ikiwa imekusanya jumla ya pointi 25.
Msimu huo, Mbeya Kwanza, ilishinda mechi tano, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 28, hivyo ina kazi kubwa ya kupambana ili kurejea Ligi Kuu Bara.
Kwa upande wa Polisi, msimu wa 2024-2025, haukuwa mzuri baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, huku ikifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi 25, kufuatia kushinda mechi sita, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
Mshambuliaji wa Mbeya Kwanza, Boniface Mwanjonde amesema mechi ya leo ni ngumu kutokana na ushindani wa timu hizo, japo watapambana kwa ajili ya kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani ili kupunguza presha wakati watakapoenda kucheza ugenini.
Kwa upande wa nyota wa Polisi Tanzania, Naku James, amesema licha ya kushinda mechi ya mwisho dhidi ya Mbeya Kwanza, ila haitokuwa rahisi kwao kutokana na umuhimu wa timu zote mbili, hasa faida ya wapinzani wao wanaoanzia kuchezea nyumbani.
Timu hizo zinakutana katika Play-Off (mtoano) na mechi ya kwanza inapigwa leo Juni 28, huku marudiano ikipangwa kupigwa Julai 5 na mshindi wa jumla atakutana na atakayepoteza kutoka Ligi Kuu Bara kwa atakayemaliza kwenye nafasi ya 13 na 14.