Mwambusi kumbe amepania Yanga

Muktasari:

HUKO Jangwani kumenoga, kwani Kocha Juma Mwambusi amebainisha mipango yake ndani ya kikosi hicho kwa kubadilisha gia kwenye aina ya soka analotaka lipigwe na vijana wake, akili yake ikiwa ni kuhakikisha anamaliza ubishi dhidi ya watani, Simba wanaotetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

HUKO Jangwani kumenoga, kwani Kocha Juma Mwambusi amebainisha mipango yake ndani ya kikosi hicho kwa kubadilisha gia kwenye aina ya soka analotaka lipigwe na vijana wake, akili yake ikiwa ni kuhakikisha anamaliza ubishi dhidi ya watani, Simba wanaotetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Simba inashikilia taji la VPL kwa msimu wa tatu mfululizo, huku kwenye msimamo ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 46, nyuma ya Yanga inayoongoza kwa pointi 50, lakini Wekundu wa Msimbazi wana viporo vitatu vinavyoweza kuwainuaa juu Wanajangwani.

Mwambusi anayekaimu nafasi ya kocha mkuu wa timu amebainisha hayo juzi katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti kwenye mazoezi ya timu hiyo, katika Uwanja wa Avic, Kigamboni.

Timu ya Mwanaspoti iliyokuwa kwenye viwanja hivyo kwa saa nne kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12 jioni na kushuhudia pia mazoezi ya timu hiyo ilizungumza na kocha Mwambusi ambaye ameeleza aina ya soka analolitaka kwenye timu hiyo.

“Mimi ni muumini wa ‘direct football’ ndiyo nahitaji Yanga icheze,” alisema kocha Mwambusi katika mahojiano hayo na kuendelea.

“Tunafanya mazoezi ya ufiti na mbinu, tunakwenda vizuri na bahati nzuri wachezaji wamejitoa, sina shaka kwamba Ligi itakapoendelea tutazidi kuwa bora zaidi na kufanya vema.”

Akizungumzia harakati za ubingwa, ambao timu hiyo inapewa presha na watani wao Simba, Mwambusi amesema bado ubingwa huo upo wazi.

“Ligi bado sana na kwenye msimamo Yanga ndiyo tunaongoza, suala la ubingwa ni la muda tu, hivyo tupeni muda na nasisitiza lengo liko pale pale,” alisema kocha huyo mzawa.

Mwambusi alipewa jukumu la kupendekeza ni kocha gani anataka awe msaidizi wake, kipindi hiki akikaimu ukocha mkuu baada ya kuondoka kwa Cedric kaze, huku klabu ikiwa kwenye mchakato wa kutafuta kocha mkuu.

“Tayari nimekabidhi majina ya makocha watatu ambayo siwezi kuyataja na uongozi ndiyo utasema kati yao yupi atakuwa msaidizi wangu,” alisema.

Alisema wakati wowote kuanzia sasa, mmoja wa makocha hao atajumuishwa kwenye kikosi hicho kuwa msaidizi wake.

“Kocha nitakayefanya naye kazi ni yule aatakayeendana na falsafa yangu, kama nilivyosema mimi ni muumini wa ‘direct football’, hivyo kocha atakayekuja lazima apite humo, naamini ni ndani ya muda mfupi kuanzia sasa mmoja kati ya watatu niliowapendekeza atakuwa ameungana nasi,” alisema.

Licha ya kutoweka wazi kama aliomba nafasi ya kuwa kocha mkuu wa Yanga, Mwambusi alisema uwezo huo anao na kukabidhiwa kijiti hicho ni jukumu la uongozi wa klabu hiyo.

“Naamini nina sifa za kuwa kocha mkuu ndiyo sababu niko hapa na ninatimiza jukumu hilo, ikitokea nimeaminiwa na kupewa kijiti hicho sitoshindwa, ingawa hilo ni la uongozi,” alisema Mwambusi.

Kauli ya kocha huyo imekuja siku kadhaa tangu baadhi ya wadau wa michezo kueleza kuwa Yanga inaweza kunolewa na kocha mzawa na ikafanya vema.

“Huo ni uamuzi wa uongozi hauko chini yangu, liko mikononi mwao,” alisema kocha Mwambusi.

Usikose makala ya mahojiano hayo maalumu na Mwambusi kuanzia kesho kwenye Mwanaspoti

Imeandikwa na Imani Makongoro, Mwanahiba Richard na Ramadhani Elias