Prime
Mzize, Dube wamvuruga beki Simba

Muktasari:
- Hata hivyo, wakati Simba ikipoteza katika mchezo huo, mashabiki wao hawakuwa na tambo nyingi wakidai kwamba kwa sasa wanaendelea kusuka upya kikosi chao na kwamba, mchezo wa pili wa ligi hiyo ndiyo utakaoamua nani mbabe dhidi ya mwenzake katika michuano hiyo.
UNAJUA vita zinazotarajiwa kutokea wiki hii pale kwa Mkapa? Zipo nyingi kuanzia uwanjani hadi nje ya uwanja wakati watani wa jadi, Yanga na Simba wanapokutana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kukamilisha ng'we ya pili ya mashindano hayo, huku Mnyama akiwa na kumbukumbu ya kupoteza raudi ya kwanza kwa bao 1-0.
Hata hivyo, wakati Simba ikipoteza katika mchezo huo, mashabiki wao hawakuwa na tambo nyingi wakidai kwamba kwa sasa wanaendelea kusuka upya kikosi chao na kwamba, mchezo wa pili wa ligi hiyo ndiyo utakaoamua nani mbabe dhidi ya mwenzake katika michuano hiyo.
Sasa basi, beki wa Simba, Chamou Karaboue amesema tangu kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Azam Februari 24, 2025, amekuwa akijiandaa kukabiliana na washambuliaji wa Yanga, Clement Mzize na Prince Dube kwani anafahamu ubora walionao.
Beki huyo raia wa Ivory Coast amefichua amekuwa akifanya juhudi kuhakikisha anavaa kikamilifu viatu vya Che Fondoh Malone katika mchezo ujao wa Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga baada ya mwenzake huyo kuumia na kuzua hofu ya kukosekana Jumamosi.
Che Malone aliumia katika mchezo huo dhidi ya Azam na kutolewa dakika ya 20 nafasi yake ikichukuliwa na Chamou huku pia akikosekana mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union. Kama hatokuwa fiti, kuna asilimia kubwa za Chamou kuchukua nafasi yake kwani ndiye mbadala wake namba moja.
Kauli ya beki huyo inakuja wakati ukikaribia mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara na Yanga itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar baada ya duru la kwanza Simba waliokuwa wenyeji kufungwa 1-0.
Yanga imekuwa na safu kali ya ushambuliaji ikiongozwa na Clement Mzize na Prince Dube ambao kila mmoja ana mabao 10 kwenye ligi wakiongoza chati ya ufungaji sambamba na kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua, pia Simba nayo ina safu bora ya ulinzi ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache kwenye ligi ambayo ni manane ikifunga 46. Yanga imeruhusu mabao tisa.
Chamou ambaye alitua Simba msimu huu, amefanikiwa kucheza Kariakoo Dabi zote mbili akiwa pacha na Che Malone, ya kwanza katika Ngao ya Jamii alianza na kumaliza wakati Simba ikifungwa 1-0.
Kisha duru la kwanza katika mchezo wa ligi akatokea benchi kuchukua nafasi ya Abdulrazack Hamza, akacheza kwa dakika 22 na Simba ilichapwa 1-0 huku mabao yote yakifungwa yeye akiwa uwanjani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chamou amesema haikuwa taarifa nzuri kwake kusikia majeraha ya Che Malone kwani ni mchezaji muhimu wa eneo lao la ulinzi.
Amesema mchezo unaofuata ni wa muhimu zaidi kwao, hivyo beki huyo kuumia siku chache kabla ya mechi kubwa zaidi kwenye ligi dhidi ya Yanga sio jambo jepesi kuchukulika.
“Baada ya kuumia kwa Che Malone nilianza kujiandaa kiakili kujua namna gani nitakabiliana na washambuliaji wa Yanga.
“Hii ni mechi ambayo kama tutakosa matokeo mazuri itaturudisha nyuma kutokana na malengo yetu ya msimu huu,” amesema beki huyo na kuongeza:
“Yanga ina washambuliaji wenye kasi sana, hivyo natakiwa kuwa sawa ili kukabiliana nao kwenye eneo hilo na niweze kwenda nao sawa.”
Eneo la ulinzi la kati la Simba lina mabeki wanne ambao ni Abdulrazack Hamza na Che Fondoh Malone wanaopewa nafasi kubwa ya kucheza, huku Chamou Karaboue na Hussein Kazi wakibaki kuwa mbadala wao.
Hamza na Che Malone pacha yao ndiyo imeonekana kuwa imara zaidi ndani ya Simba msimu huu hivyo kitendo cha Che Malone kuumia, Chamou anatajwa kuwa chaguo la kwanza kuziba nafasi hiyo kuliko Hussein Kazi.
Muivory Coast huyo katika ligi msimu huu, amecheza mechi 12 kati ya 21 akitumika kwa dakika 872, huku upande wa kimataifa kuanzia hatua ya makundi akicheza mechi nne kati ya sita kwa dakika 124 na Simba imefuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho.