Namba zamkatisha tamaa Kocha Azam

Muktasari:
- Azam kwa sasa ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 51 baada ya kucheza mechi 25 na Taoussi alisema matumaini ya wao kutwaa ubingwa msimu huu yamevunjika huku akiitaja Yanga kushika hatma yao kuendelea kusalia nafasi waliyopo sasa.
KIPIGO cha bao 1-0 ilichokipata Azam mbele ya Singida Black Stars, kimemfanya kocha wa timu hiyo, Rachid Taoussi kuonyesha dalili za waziwazi amekata tamaa.
Azam kwa sasa ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 51 baada ya kucheza mechi 25 na Taoussi alisema matumaini ya wao kutwaa ubingwa msimu huu yamevunjika huku akiitaja Yanga kushika hatma yao kuendelea kusalia nafasi waliyopo sasa.
Tofauti yao na vinara Yanga ni pointi 10 kabla ya mchezo wa jana.
Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema; “Sio rahisi kushinda mechi zote, tuna uwezo wa kumfunga kila mpinzani anayekuja mbele yetu, lakini kuna wakati tukubali hatuwezi kushinda kwa kila mechi. Tunahitaji umakini zaidi katika mechi zijazo kwa sababu hakuna mchezo utakaouwa rahisi.”
“Hatma ya nafasi yetu ipo mikononi mwa Yanga katika mchezo wetu unaofuata na tunahitaji matokeo mazuri kwa sababu anayetukimbiza tumemuacha kwa pointi moja na amekuwa na mfululizo wa matokeo mazuri kwa mechi za karibuni tofauti na sisi,” alisema kocha huyo.
Azam baada ya kutoka kufungwa 1-0 ugenini, itarejea nyumbani kuikaribisha Yanga katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, mechi ikipangwa kuchezwa Alhamisi wiki hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar.
Kuhusu mchezo huo, Taoussi alisema hautakuwa rahisi na umebeba kisasi kwa sababu wapinzani wao ambao wanapambana kutetea taji la ligi hawatakubali kupoteza tena dhidi yao baada ya kuwafunga duru la kwanza.
“Tuna vita nyingi kwenye nafasi tuliyopo, matokeo mazuri ndio kipaumbele chetu, tunaiheshimu Yanga lakini hatupo tayari kupoteza mechi mbili mfululizo, tutarejea mchezo uliopita kwa kuangalia mokosa yetu na kufanyia kazi kabla ya kumvaa mpinzani wetu ajaye,” alisema Taoussi.
Pointi ilizonazo Azam kwa sasa ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo, zinaifanya kuwa na wasiwasi na Singida Black Stars kufuatia kupishana moja tu.
Azam ikiwa imebakiwa na mechi tano zenye pointi 15 kama ikishinda zote itamaliza na 66, ambazo ni pungufu ya tatu ilizomaliza nazo msimu uliopita iliposhika nafasi ya pili.