Noble aitwa kamati ya maadili Fountain Gate

Muktasari:
- Fountain ilikumbana na kipigo hicho cha nyumbani katika mchezo huo uliopigwa Jumatatu ya wiki hii na kuifanya iwe kinara wa kuruhusu mabao mengi zaidi (51) hadi sasa katika Ligi Kuu ikiipiku hadi KenGold iliyokuwa ikiongoza na iliyoshuka daraja rasmi ikivuna pointi 16 na kufungwa mabao 50.
KIPA wa Fountain Gate raia wa Nigeria, John Noble ameitwa Kamati ya Maadili ya klabu hiyo, kwa lengo la kuhojiwa kutokana na makosa mawili aliyofanya ya kuruhusu mabao mawili yaliyochangia timu hiyo kulala 4-0 mbele ya Yanga siku zilipokutana kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara.
Fountain ilikumbana na kipigo hicho cha nyumbani katika mchezo huo uliopigwa Jumatatu ya wiki hii na kuifanya iwe kinara wa kuruhusu mabao mengi zaidi (51) hadi sasa katika Ligi Kuu ikiipiku hadi KenGold iliyokuwa ikiongoza na iliyoshuka daraja rasmi ikivuna pointi 16 na kufungwa mabao 50.
Katika mchezo huo kipa Noble aliruhusu bao dakika ya 38 lililofungwa na Clement Mzize baada ya kuutema mpira uliopigwa kichwa na Prince Dube aliyeunganisha frii-kiki ya kiungo mshambuliaji Stephane Aziz KI.
Wakati Fountain ikijipanga kujipu mapigo, Noble kwa mara ya pili tena katika dakika ya 43 alifanya makosa baada ya kushindwa kuumiliki mpira na kupiga pasi fupi iliyonaswa na Aziz KI aliyepiga bao la pili kabla ya kocha Robert Matano kumtoa nje na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahim Parapanda aliyeruhusu pia mabao mawili na mchezo huo kuisha kwa kichapo cha 4-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha alisema ni kweli nyota huyo ameitwa katika Kamati ya Maadili kwa ajili ya kumhoji juu ya kiwango alichokionyesha, kisha baada ya hapo watatoka na majibu.
“Siwezi kusema moja kwa moja tutasitisha mkataba wake au vipi kwa sababu tunasubiria ripoti ya benchi la ufundi itueleze kile ilichokiona kwa utashi wao kisha tutatoka na tamko kuhusu yeye, hivyo nikiri ni kweli tumemuita,” alisema Kidawawa.
Kwa upande wa Noble alipotafutwa na Mwanaspoti kuzungumzia sakata hilo, alisema baada ya mchezo huo amekuwa na wakati mgumu, ingawa ataenda kueleza kile kilichotokea, kisha kuanzia hapo atakuwa na wigo mpana wa kuelezea mustakabali wake.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Tabora United, huenda mkataba wake wa mwaka mmoja wa nyongeza ukasitishwa kwa makubaliano ya pande mbili, kutokana na makosa anayoyafanya hadi sasa.
Noble aliyechezea ASC Kara ya Togo, alitua nchini kwa mara ya kwanza Julai 31, 2023, akitokea Enyimba ya kwao Nigeria na kujiunga na Tabora United aliyoitumikia kwa msimu mmoja, kisha kutua Fountain Gate ambayo zamani Singida Fountain Gate.