Pamba Jiji yaishusha rasmi Kagera Sugar ikiongeza presha Ligi Kuu

Muktasari:
- Ushindi wa Pamba Jiji umeongeza vita kwa timu nne kupambania kukwepa kucheza play off huku ikiishusha rasmi Kagera Sugar iliyoungana na KenGold iliyotangulia Championship.
Wakati Pamba Jiji ikichekelea ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KenGold, matokeo hayo yamepeleka kilio kwa Kagera Sugar ambayo imeaga rasmi Ligi Kuu na msimu ujao itacheza Championship.
Hata hivyo, licha ya ushindi huo kwa Pamba Jiji, unaongeza vita mpya ya kupambana kukwepa kucheza play off ya kubaki Ligi Kuu baina ya timu hiyo yenye pointi 30 sawa na Tanzania Prisons na KMC, huku Fountain Gate ikiwa nazo 29 huku Namungo na Coastal Union zikiwa na 31.
Kagera Sugar ambayo imedumu miaka 20 Ligi Kuu, kati ya mechi mbili zilizobaki hata ikishinda zote itafikisha 28 ambazo kimahesabu hazitakuwa na faida zaidi ya kushuka daraja ikiungana na KenGold iliyotangulia.
Katika mchezo wa leo, Pamba Jiji ndio ilikuwa na uhitaji zaidi wa pointi tatu, kutokana na presha ya kukwepa kushuka daraja ambapo ikicheza kwa ubora wake imeibuka na mabao 2-0.
Abdoulaye Yonta Camara alianza kumtesa kipa Castor Mhagama dakika ya 26 kabla ya kumtungua tena dakika ya 66 na kujihakikishia timu hiyo ushindi huo na kupanda nafasi ya 11.
Kocha Msaidizi wa Pamba Jiji, Mathias Wandiba amesema baada ya matokeo hayo kazi iliyobaki ni kutafuta pointi sita katika mechi mbili zilizobaki ili kujihakikishia kuwa salama Ligi Kuu.
Amesema matokeo ya leo yanawaweka katika nafasi ya play off, lakini hesabu za timu hiyo ni kujinasua katika hatari hiyo akieleza kuwa michezo dhidi ya JKT Tanzania na KMC watakazocheza jijini Mwanza ni za kufa na kupona.
"KenGold licha ya kuwa wameshashuka lakini wametupa upinzani, tunashukuru kwa ushindi huu ambao unatupeleka kwenye play off ila mpango wetu ni kujiondoa kwenye presha hiyo, hivyo mkakati ni kumaliza mechi mbili zilizobaki kwa ushindi," amesema Wandiba.
Kocha Mkuu wa KenGold, Omary Kapilima amesema kwa sasa wanasubiri kumaliza rasmi msimu akibainisha kuwa ni mengi yaliyosababisha timu kushuka daraja lakini zaidi kiufundi ni sehemu ya beki.
"Ukiangalia zaidi mechi zote tumeruhusu bao, tukubaliane na matokeo yote na tunasubiri tumalize Ligi tujipange upya na championship msimu ujao," amesema Kapilima.