Pointi 15 zamliza Omary Madenge

Muktasari:
- Kikosi hicho kilichoshuka daraja msimu wa 2021-2022, kilikatwa pointi hizo kutokana na kushindwa kufika katika mchezo dhidi ya Mbeya City uliopangwa kuchezwa Desemba 3, 2024, kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya kwa sababu za ukata.
KITENDO cha Biashara United kupokwa pointi 15 na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), kimemliza kocha wa kikosi hicho, Omary Madenge na kukiri ingekuwa ni miujiza kubakia Ligi ya Championship msimu ujao, licha ya juhudi kubwa zilizofanyika.
Kikosi hicho kilichoshuka daraja msimu wa 2021-2022, kilikatwa pointi hizo kutokana na kushindwa kufika katika mchezo dhidi ya Mbeya City uliopangwa kuchezwa Desemba 3, 2024, kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya kwa sababu za ukata.
Akizungumza na Mwanaspoti, Madenge alisema hawana jinsi tena na wanajipanga na kuanza maisha mapya First League, huku akiwaomba mashabiki wa kikosi hicho kuendelea kuwapa sapoti, akiamini watarejea tena wakiwa imara na washindani.
"Tulianza vizuri msimu huu, lakini katikati mambo yakaharibika, tumekubaliana na kilichotokea lakini sisi kama benchi la ufundi tumeumia sana kwa sababu hayakuwa malengo yetu, tunawaomba radhi mashabiki kwa kilichotokea," alisema Madenge.
Timu hiyo imekuwa ya kwanza kushuka daraja msimu huu baada ya kucheza mechi 29, ikishinda minane, sare sita na kupoteza 15, ikiburuza mkiani na pointi 15 na kwa sasa itaikaribisha Polisi Tanzania Mei 10, kwenye Uwanja wa Karume Mara.