Prisons yakabidhiwa viongozi wa dini, kimila kuinusuru

Muktasari:
- Kutokana na matokeo yasiyoridhisha ya Prisons, viongozi wa juu wa timu hiyo, wamewaita wadau wakiwamo viongozi wa dini, kimila, wafanyabiashara kujadili namna ya kuinusuru timu hiyo.
Kawia ufike. Ni neno unaloweza kueleza baada ya uongozi wa Tanzania Prisons kuwaita wadau kujadili namna ya kuinusuru timu hiyo kukwepa aibu ya kushuka daraja.
Prisons yenye makazi yake Ruanda, jijini Mbeya, haijawa na matokeo mazuri Ligi Kuu Bara, ikiwa nafasi mbili za mwisho kwenye msimamo kwa pointi 18 baada ya michezo 24.
Kwa sasa timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza nchini, imebakiza mechi sita pekee kumaliza msimu na kusubiri hatma yake kubaki au kucheza Championship msimu ujao.
Ili kuhakikisha Maafande hao wanabaki salama, uongozi wa timu hiyo chini ya Kamishina Msaidizi mwandamizi wa Jeshi hilo nchini, Kenneth Mwambije kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi hilo CGP, Jeremia Katungu wamewaita wadau usiku huu kujadiliana juu ya mwenendo wa chama hilo.
Walioitwa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Juma Homera, viongozi wa dini, viongozi wa kimira, wafanyabiashara, Chama Cha Soka mkoani humo (Mrefa) na wadau mbalimbali ili kujadiliana kumaliza vizuri mechi zilizobaki.
Akizungumza usiku huu Aprili 4, Kamishina Msaidizi mwandamizi wa Jeshi hilo, Mwambije amesema licha ya kuchelewa lakini bado muda upo kujipanga na michezo iliyobaki na kupata ushindi na timu kubaki salama Ligi Kuu.
"Kama kuna sehemu tulikosea tusameheane, tuwe wamoja hizi mechi zilizobaki tupate ushindi, hatujachelewa sana kwa kuwa huenda muda sahihi ni huu, kila mmoja kwa nafasi yake atusaidie," amesema kamishina huyo mwandamizi.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Maulid Surumbu amesema mpira ni sehemu ya ajira na uchumi na kuwaomba wadau wote kuchangia ili kuinusuru timu hiyo.
"Kuanzia mechi ijayo dhidi ya Kagera Sugar Aprili 6, tukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Homera tutakuwapo uwanjani kuhakikisha timu inashinda na kampeni inaanza rasmi kusapoti Prisons ibaki Ligi Kuu," amesema Kanali Surumbu.
Kiongozi wa kimila, Chifu Rocket Mwashinga amesema ameshangazwa na matokeo yasiyoridhisha ya timu hiyo na mechi zijazo lazima kieleweke akiomba wadau kuungana pamoja.
"Kama tunavyofanya kwa Mbeya City inashindikanaje kwa Tanzania Prisons? Hebu tushirikiane na tuko tayari sisi kupambana mechi hizi tushinde zote, hatukubali ishuke daraja," amesema Mwashinga.
Afisa Michezo mkoani humo, Robert Mfugale amesema kuwapo kwa timu nyingi ni sehemu ya kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na lazima wadau wote kushirikiana kuzinusuru timu zote.
"Kuna msimu tulipambana sana kuinusuru timu hii, sasa mbinu zilizotumika wakati ule basi tuutumie, lakini tusinyosheane vidole badala yake tumalize hili kisha turekebishane," amesema Mfugale.