Ruvu Shooting yaanza kibabe michuano ya U20 wilaya ya Morogoro 2022

Mshambuliaji wa Ruvu Shooting, John Chikungu akiruka daruga la mlinzi wa Chamwino Youth, Festo Kinongo katika michezo inayoendelea kufanyika katika uwanja wa Sabasaba Manispaa ya Morogoro ambapo katika mchezo wa kwanza dhidi ya Chamwino Youth imeweza kuibuka na ushindi wa bao 5-0. Picha na Juma Mtanda
Ruvu Shooting imeanza michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 20 wilaya ya Morogoro 2022 kwa nguvu kubwa baada ya kuipigisha kwata Chamwino Youth kisha kuwachapa bao 5-0 huku Kocha mkuu wa maafande hao akieleza kuwa uwanja unaofanyika michuano hiyo sio rafiki kwa vijana wake na vijana wake kushindwa kuonyesha kandanda safi.
Mashindano hayo yanafanyika kwenye uwanja wa Sabasaba kwa kukutanisha timu za vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 huku Ruvu Shooting, Kilombero Socer Net na Pwani Sports Foundation zikiwa timu alikwa zikiungana na timu wenyewe 21 za Manispaa ya Morogoro kuwania ubingwa wa michuano hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti (leo Mei 2) mkoani hapa, Kocha mkuu wa vijana wa Ruvu Shooting, Frank Msese alisema michuano hiyo ni mizuri japo uwanja umekuwa kikwazo kwa vijana wake kucheza soka analowafundisha.
Msese alisema uwanja unaotumika katika mashindano hayo sio rafiki kutokana na kuwa na vichuguu, manundu na sehemu kubwa kutoota nyasi (Kipara) lakini licha ya hali hiyo wameweza kuibuka na ushindi wa bao 5-0 mbele ya Chamwino Youth katika mchezo wao wa kwanza.
“Mashindano haya ni mazuri kwa vijana wetu kuweza kuonyesha vipaji vyao vya soka na kushindana na wenzao nasi tumefurahia na mchezo wetu na hawa Chamwino Youth tumepata ushindi mzuri wa bao 5-0.”alisema Msese.
Msese alisema uwanja huo endapo ungekuwa kwenye hali mzuri, vijana wake wangeweza kucheza soka zuri zaidi na kuvutia katika michuano hiyo.
Mabao ya Ruvu Shooting dhidi ya Chamwino Youth yalikwamishwa wavuni na Saidi Matola dakika ya 12, Abby Mikimba dakika ya 14, John Chinguku dakika ya 18,Sylvester Otto dakika ya 51 na Haruna Fadhir akihitimisha kwa kufunga bao la tano dakika ya 81 huku Chamwino Youth ikishindwa kupenya ngome ya wapinzani wao angalau kupata mabao ya kufutia machoz