Sillah: Bara inastahili namba nne Afrika

Muktasari:
- Sillah alisema tangu aanze kucheza Ligi Kuu msimu uliopita, huu ndio msimu bora kwake kwa kiwango binafsi na ushindani wa mechi kwa ujumla, unaowasaidia wachezaji kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzisaidia timu zao.
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah amesema kwa namna Ligi ya Tanzania ilivyo ngumu na ushindani wa juu inastahili kutajwa kati ya zilizo bora barani Afrika ambapo kwa sasa ipo nafasi ya nne.
Sillah alisema tangu aanze kucheza Ligi Kuu msimu uliopita, huu ndio msimu bora kwake kwa kiwango binafsi na ushindani wa mechi kwa ujumla, unaowasaidia wachezaji kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzisaidia timu zao.
“Ingawa hatujafikia malengo ya kuchukua ubingwa kama ilivyokuwa matarajio yetu wakati tunauanza msimu huu, hilo halitukatishi tamaa kuendelea kupambana na kuzidi kucheza kwa viwango vya ushindani dhidi ya timu pinzani hadi ligi itakapomalizika,” alisema Sillah na kuongeza;
“Katika Afrika ukitaja Ligi Bora na ngumu kuacha kuitaja Tanzania ambayo imekuwa kivutio kwa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kuja kuicheza kwa mafanikio makubwa na wengine wamefanikiwa kwenda mbali zaidi baada ya kufanya vizuri hapa.”
Msimu wa kwanza 2023/24, Sillah alifunga mabao manane kupitia mechi dhidi ya Yanga (Yanga 3-2, Oktoba 2023 ), (Azam 2-1 Yanga, Machi 13), (Azam 5-0 KMC, Desemba 7, 2023),(KMC 0-4 Azam, Septemba 19) kisha kuzifunga pia Geita Gold, Mashujaa na Mtibwa Sugar.
Sillah tayari kayafikia mabao manane ya msimu uliyopita na sasa katika mechi tatu zilizosalia dhidi ya Dodoma Jiji, Tabora United na Fountain Gate alisema anatamani afikishe angalau mabao 10.
“Nafahamu kuna presha kubwa katika mechi za kufunga msimu, lakini kiu yangu nikumaliza na mabao 10.”
Kuhusiana na kuhusishwa na Simba na Yanga huku ikisemekana hajaongeza mkataba mpya na timu yake Azam, alisema kwa sasa hayupo tayari kulizungumzia hilo.
“Nawekeza nguvu zaidi katika mechi zilizopo mbele yangu na bado ni mchezaji wa Azam hivyo siwezi kuzungumza kuhusiana na ofa za timu nyingine,” alisema Sillah, raia wa Gambia.