Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sowah, Mukwala waingizwa vitani Sauzi

Muktasari:

  • Awali ilielezwa Kaizer ilikuwa ikiwapigia hesabu Joshua Mutale (Simba), Feisal Salum (Azam) na kipa Diarra Djigui (Yanga), lakini upepo umebadilika ghafla baada ya kudaiwa benchi la ufundi limevutiwa na mastraika hao ili kwenda kutatua eneo la ushambuliaji ambalo lilikuwa likimtegema Chivaviro na Makabi Lilepo.

KITENDO cha Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kujiandaa kuachana na straika Ranga Chivaviro, kumeibua vita mpya kwa nyota wanaokiwasha katika Ligi Kuu Bara, Jonathan Sowah wa Singida Black Stars na Steven Mukwala wa Simba wanaohusishwa kuwindwa na AmaKhosi.

Awali ilielezwa Kaizer ilikuwa ikiwapigia hesabu Joshua Mutale (Simba), Feisal Salum (Azam) na kipa Diarra Djigui (Yanga), lakini upepo umebadilika ghafla baada ya kudaiwa benchi la ufundi limevutiwa na mastraika hao ili kwenda kutatua eneo la ushambuliaji ambalo lilikuwa likimtegema Chivaviro na Makabi Lilepo.

Ipo hivi. Mwanaspoti lilisharipoti juu ya Kaizer Chiefs kuhitaji saini ya Sowah ikiingilia dili za Simba na Yanga ambazo pia zinahitaji huduma ya mshambuliaji huyo na faili la Mukwala limetua mezani rasmi ili kuona ni staa gani atafaa kuendana na kasi ya timu hiyo.

Na taarifa za karibuni ni kwamba kuna mazungumzo yanaendelea baina ya uongozi unaomsimamia Mukwala na Kaizer Chiefs kujadili dili la straika huyo kama wanaweza kuununua mkataba uliobakia Msimbazi.

Mukwala alisajiliwa na Simba msimu huu kwa mkataba wa miaka mitatu akitokea Asante Kotoko ya Ghana alikofunga mabao 14 na kwa sasa katika Ligi Kuu Bara anamiliki mabao 12 na asisti tatu kupitia mechi 25 alizocheza.

Wakati huohuo inaripotiwa kuwa Sowah nyota wa kimataifa kutoka Ghana, awali amekuwa akihusishwa na Yanga iliyoelezwa ilijifungia naye jijini Dar es Salaam Aprili mwaka huu ili kuwekana sawa, lakini Kaizer kupitia kocha Nasreddine Nabi imetajwa kummezea mate baada ya kuonwa katika mechi dhidi ya Simba.

Nabi alikuwa nchini na kushuhudia mechi ya Ligi Kuu kati ya Simba na Singida BS ambapo Msimbazi ilishinda 1-0 kabla ya kwenda kupasuka kwa mabao 3-1 katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) iliyochezwa Manyara, ambapo kocha huyo wa zamani alimtuma skauti wa klabu kuwasoma zaidi nyota hao.

Sowah tangu ajiunge na Singida katika dirisha dogo la Januari, mwaka huu, akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya amefunga mabao 11 ya Ligi Kuu akizidiwa manne na kinara kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua anayeongoza akitupia 15.

Na sasa wakati nyota huyo akionyesha kiwango hicho, timu mbalimbali zimeonyesha uhitaji wa kuipata saini yake na mbali na Yanga inayoripotiwa tangu awali kumhitaji nyingine ni Al-Hilal Omdurman ya Sudan na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Kaizer kimelieleza Mwanaspoti kuwa, kocha Nabi ndio amependekeza uongozi wa timu hiyo kufanya juu chini ili uweze kuinasa saini ya mmoja kati ya mastaa hao.

Nabi anahusishwa pia na Jean Ahou na Joshua Mutale anaowataka kutoka katika kikosi cha Simba, huku pia akimtaka Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayekipiga Azam FC.

Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kwamba pamoja tayari mazungumzo kwa timu zote mbili Simba na Singida BS yameanza kwa ajili ya kufanikisha kunasa mshambuliaji mmoja kati ya hao.

“Mukwala amebakiza mkataba wa miaka miwili sawa na Sowah ambae pia inaelezwa bado ana mkataba wa mwaka na nusu kuendelea kuitumikia Singida BS, lakini kuna mazungumzo ya pande zote yanayoendelea itategemeana na ofa ya Kaizer Chiefs kama itakuwa na manufaa kwa mchezaji na klabu,” kimesema chanzo hicho na kuongeza:

“Endapo Simba ikifanikiwa kumuuza Mukwala basi itambakiza Leonel Ateba aliye na mabao 12 ambaye yupo katika mstari wa kukatwa jina lake, wakati kwa upande wa Singida watabaki na Elvis Rupia na inaelezwa kuwa wapo kwenye mchakato wa kusajili mshambuliaji mwingine mpya.”