Pina amaliza msimu kibabe, aziita timu mezani

Muktasari:
- Mshambuliaji huyo ambaye ameibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar, amefanikiwa kuvunja rekodi ya msimu uliopita iliyowekwa na Suleiman Mwalimu alipofunga mabao 20, huku yeye akiongeza moja zikiwemo hat trick mbili na kutoa asisti 12.
MSHAMBULIAJI wa timu ya Mlandege, Abdallah Iddi 'Pina' amesema malengo aliyojiwekea msimu huu wa 2024-25 ikiwemo timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) na kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo, yametimia ambapo kwa sasa anataka kucheza soka nje ya Zanzibar.
Katika ufungaji, Pina amefanikiwa kuvunja rekodi ya mchezaji wa zamani wa KVZ FC ambaye kwasasa anakipiga Wydad Casablanca ya nchini Morocco, Suleiman Mwalimu aliyefunga mabao 20.
Pina ambaye anashikilia rekodi mbili msimu huu ya kufunga mabao 21 akiibuka mfungaji bora sambamba na kufunga mabao saba katika mchezo mmoja dhidi ya Tekeleza waliposhinda 11-1, amesema amemaliza msimu kwa furaha.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pina amesema katika mchezo wa mwisho kuhitimisha msimu waliposhinda 4-2 dhidi ya New City huku yeye akifunga mabao mawili, kipindi cha kwanza alikuwa na presha kubwa kwasababu alikuwa anatamani kufikia lengo la kuwa mfungaji bora na timu yake kutwaa ubingwa.
Hata hivyo, amesema kipindi cha pili aliingia bila hofu na presha kwani alikuwa tayari amefunga mabao mawili na alipochaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo haikumshtua kwani ni miongoni mwa mipango yake kufunga na kuwa mchezaji bora kila mchezo.
"Msimu umemalizika nikiwa na mafanikio makubwa ambayo niliyapanga na mipango yangu kwasasa ni kutoka nje ya Zanzibar kuonesha uwezo wangu, timu iliyokuwa inanihitaji naikaribisha kwa mazungumzo," amesema Pina.
Miezi kadhaa iliyopita, Pina alihusishwa kufanya mazungumzo ya kujiunga na Yanga SC, lakini mwenyewe amefichua kwamba ishu hiyo bado itabaki kuwa tetesi tu.
"Kinachosemakana kuwa nimeshafanya mazungumzo na kupewa mkataba na Yanga sio kweli, hayo ni maneno ya watu," amesema Pina na kuongeza.
"Sio Yanga tu, timu yoyote ambayo inataka kuja mezani kwa mazungumzo ikaribie nipo kwa hilo na itakayofanikiwa ndio nitajiunga nayo."
Ijumaa ya Juni 6, 2025, Ligi Kuu Zanzibar ilifikia tamati kwa msimu wa 2024-25 ambapo Mlandege imetwaa ubingwa kwa kufikisha pointi 62 sawa na KVZ, lakini tofauti ya mabao imewabeba.
Mlandege imetwaa ubingwa huo uliokuwa ukishikiliwa na JKU ambayo msimu huu imemaliza ligi nafasi ya tano.