Miroshi ashindwa kuandika rekodi Ulaya

Muktasari:
- Endapo bingwa wa Kombe la Uturuki itakuwa imeshafuzu moja kwa moja michuano ya Ulaya kwenye ligi, nafasi hiyo itachukuliwa na timu itakayomaliza nafasi ya nne.
KIRAKA wa Goztepe inayoshiriki Ligi Kuu ya Uturuki, Novatus Dismas Miroshi ameshindwa kuandika historia nyingine kwenye michuano ya Ulaya baada ya chama lake kumaliza nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi.
Iko hivi. Mabingwa wa ligi kuu na mshindi wa pili ndizo zinakata tiketi ya kushiriki katika raundi ya pili ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (Champions League), huku ya tatu na mshindi wa Kombe la Uturuki (Turkish Cup) zinapata nafasi ya kucheza katika raundi ya pili ya mchujo ya Europa Conference League.
Endapo bingwa wa Kombe la Uturuki itakuwa imeshafuzu moja kwa moja michuano ya Ulaya kwenye ligi, nafasi hiyo itachukuliwa na timu itakayomaliza nafasi ya nne.
Chama hilo la Mtanzania huyo, licha ya kuwa katika nafasi nzuri ya kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na kujihakikishia kushiriki Europa League, ilijikuta ikipoteza mechi mbili kati ya tatu za mwisho.
Kama Miroshi angefuzu kucheza michuano hiyo, ingekuwa mara yake ya pili na angekuwa Mtanzania wa pili kufanya hivyo baada ya Mbwana Samatta aliyefuzu akiwa na PAOK FC.
Msimu wa 2022/23, Miroshi akiitumikia Shakhtar Donetsk ya Ukraine kwa mkopo akitokea Zulte Waregem ya Ubelgiji alicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kama ambavyo Samatta alitangulia kucheza michuano hiyo msimu wa 2019-20 akiwa na Genk ya Ubelgiji na alifunga bao dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield licha ya timu yake kulala kwa mabao 2-1.
Miroshi alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Porto, chama lake likitandikwa mabao 3-1, mechi ambayo alianza na kumaliza dakika zote 90 na kumfanya aingie kwenye kitabu cha historia ya kuwa Mtanzania wa pili kucheza michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani Ulaya.