Utamu: Mambo yaiva England

Kocha wa Manchester United Sir Alex Ferguson
LONDON, ENGLAND INAWEZEKANA Manchester United ikatawazwa mabingwa wa Ligi Kuu England keshokutwa Jumatatu badala ya Jumapili ijayo iwapo hesabu zitaenda kama zinavyoonyesha. Kikosi cha Alex Ferguson kitafanikiwa kutwaa ubingwa huo mapema iwapo Manchester City itafungwa na Tottenham kwenye mchezo wa kesho Jumapili na kisha wao wakaifunga Aston Villa hiyo keshokutwa Jumatatu. Manchester City inakwenda kupambana kwenye Uwanja wa White Hart Lane ikiwa nyuma ya Manchester United kwa pointi 13. Kama Man City ikifungwa na kisha United ikishinda, kikosi cha Roberto Mancini kitakuwa nyuma kwa pointi 15 ambazo hawawezi kuzifukia hata baada ya mechi zao zinazokuja. Awali Mancini alisema anafahamu Man United itapata ubingwa lakini anataka kuwachelewesha sherehe kidogo. Huenda kazi ya Man United ikawa nyepesi kwa kuwa Tottenham haiwezi kukubali kushindwa kwa sababu inapigania nafasi ya nne bora sambamba na Chelsea na Arsenal. Kama mambo yakienda kombo kwa Manchester United hiyo keshokutwa Jumatatu, basi itabidi isubiri hadi Jumapili ya wiki ijayo ili kutwaa ubingwa mbele ya Arsenal uwanjani Emirates. Mechi hiyo itakuwa ya kusisimua na hasa iwapo Robin Van Persie atanyakuwa ubingwa wa Ligi Kuu England kwenye uwanja wake wa zamani. Mchezaji huyo alihamia Manchester United msimu huu huku mashabiki wa Arsenal wakimzomea kuwa ana tamaa ya fedha. Hata hivyo mwenyewe alisema kuwa alikuwa akitafuta vikombe si fedha. Iwapo Van Persie akitwa ubingwa Emirates atawadhihirishia mashabiki wake wa zamani kuwa kweli alichoshwa na ukame wa vikombe unaoikabili Arsenal kwa miaka minane. Man City ina uhakika wa kukosa ubingwa wa England lakini ina uhakika wa kubaki kwenye nafasi ya pili, jambo hilo linafanya mbio za kusaka nafasi ya tatu na ya nne ziwe kali. Manchester United inaongoza kwa pointi 81, Man City iliyo nafasi ya pili ina pointi 68, Chelsea ya tatu ikiwa na pointi 61, Arsenal ya nne ina pointi 60, Tottenham inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 58 na Everton ikifuata kwa pointi 56. Man City, Tottenham na Chelsea zimecheza mechi 32 wakati klabu nyingine zote zimecheza mechi 33. Kikosi cha Andre Villas-Boas kilikuwa na nafasi kubwa ya kutua nafasi ya tatu, lakini kilipofungwa na Liverpool na Fulham katika siku za karibuni hesabu zake zilivurugika na hivyo kuikaribisha Everton, Arsenal na Chelsea kwenye mbio za nne bora. Chelsea ilishika nafasi ya tatu baada ya kuifunga Fulham mabao 3-0 Jumatano wiki hii na kuiondoa Arsenal kwenye nafasi hiyo baada ya kikosi cha Arsene Wenger kutoka suluhu na Everton, Jumanne wiki hii. Arsenal itakwaana na Fulham leo Jumamosi na kutoa presha kwa Chelsea ambayo itacheza na Liverpool huku Tottenham nayo ikiwa na kazi ngumu mbele ya Man City.