VIDEO: Soka lambeba beki Yanga, apandishwa cheo KMKM

Muktasari:
- “Sina budi kushukuru kikosi changu kwa kuweza kunisapoti kwa kila hatua. Nitaendelea kuipambania nchi yangu," amesema Sajenti Ibrahim Bacca ambaye wazazi wake pia ni askari.
KIKOSI Maalumu cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM) kimempandisha cheo beki wa Yanga SC, Ibrahim Hamad "Ibra Bacca", kutoka Koplo hadi Sajenti. Hii ni kutokana na mchango wake mkubwa katika soka, huku akiendelea kuwa mchezaji muhimu kwa timu yake na taifa.
Bacca ameonesha kiwango bora ndani ya Yanga, akisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mbalimbali tangu alipojiunga nayo Januari 14, 2022 akitokea KMKM. Uamuzi wa KMKM kumpandisha cheo ni ishara ya kuthamini juhudi zake, si tu kama mwanajeshi, bali pia kama mwanamichezo anayeliletea heshima taifa.
"Sina budi kushukuru kikosi changu kwa kuweza kunisapoti kwa kila hatua. Nitaendelea kuipambania nchi yangu," alisema Sajenti Ibrahim Bacca, akionesha furaha yake kwa hatua hiyo. Beki huyo wa kati, ambaye ana ndoto kubwa katika soka, anasema atahakikisha anaendelea kuipa heshima Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Kikosi cha KMKM, ambacho kimemruhusu Bacca kuitumikia Yanga, ni moja ya vyombo muhimu vya ulinzi Zanzibar. Kinahusika na kulinda mipaka ya bahari dhidi ya magendo, uvuvi haramu, na vitendo vingine vya kihalifu vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa.
Zaidi ya kuwa chombo cha ulinzi, KMKM pia hushiriki katika operesheni za uokoaji baharini na kuhakikisha usalama wa vyombo vya majini. Kikosi hiki kimekuwa msaada mkubwa katika juhudi za kulinda rasilimali za bahari na kudhibiti uhalifu unaoweza kufanyika katika ukanda wa Pwani.
Kwa upande wa soka, Bacca amekuwa mhimili mkubwa katika safu ya ulinzi ya Yanga SC. Akiwa sehemu ya kikosi hicho, ameisaidia klabu yake kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Bara, Kombe la FA (3) na Ngao ya Jamii (3). Huu ni ushahidi wa mchango wake mkubwa ndani ya timu.
Mafanikio yake hayajaishia tu kwenye soka la ndani. Bacca alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2023, ambako walipoteza kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria kufuatia matokeo ya jumla kuwa 2-2, mechi ya kwanza Yanga nyumbani ilifungwa 1-2, ugenini ikashinda 0-1.
Kwa upande wa timu ya taifa, Bacca amekuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars ambacho kilipata tiketi ya kufuzu kwa fainali zijazo za mataifa ya Afrika ambazo zitafanyika Morocco, lakini pia beki huyo alikuwa kwenye kikosi cha Stars kilichoshiriki fainali zilizopita kule Ivory Coast mwaka 2023 ambapo timu iliishia hatua ya makundi.
Kucheza soka huku akiendelea kuwa askari wa KMKM, Bacca kwake haijawa kikwazo. Nidhamu na mafunzo aliyopata jeshini vimemsaidia kuwa mchezaji mwenye maamuzi sahihi na uwezo wa kupambana uwanjani.