Wakimbiaji 700 kushiriki Fistula Marathon Arusha

Muktasari:
- Mbio hizo kwa msimu wa nne zinatarajia kufanyika Mei 25, 2025 jijini Arusha kwa ajili ya kusaidia utoaji elimu juu ya ugonjwa wa fistula, kuwa unatibika lakini pia kusaidia upatikanaji wa fedha za matibabu kwa zaidi ya wanawake 250 wanaojitokeza wenye matatizo ya ugonjwa wa Fistula ya uzazi.
Wanariadha wa kimataifa, Failuna Abdi Matanga na Angelina John, wamejitosa kuwa mabalozi wa mbio za Fistula Marathon zinazolenga kusaidia matibabu ya wanawake wanaoathirika na ugonjwa huo wakati wa kujifungua.
Mbio hizo kwa msimu wa nne zinatarajia kufanyika Mei 25, 2025 jijini Arusha zikishirikisha wakimbiaji zaidi ya 700 ikiwa ni kwa ajili ya kusaidia utoaji elimu juu ya ugonjwa wa fistula, kuwa unatibika lakini pia kusaidia upatikanaji wa fedha za matibabu kwa zaidi ya wanawake 250 wanaojitokeza wenye matatizo ya ugonjwa wa Fistula ya uzazi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi leo Aprili 7, 2025, meneja wa mbio hizo, Doreen Moshi amesema zitashirikisha zaidi ya wakimbiaji 700 wa umbali wa kilomita tano, 10 na 21 ikiwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ugonjwa wa Fistula duniani.
Amesema lengo kubwa la Taasisi ya Martenity Afrika kuandaa mbio hizo ni kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo lakini pia jinsi ya kutibiwa ili kuwaweka wanawake salama dhidi ya uzazi.
“Taasisi yetu tunatoa elimu na matibabu ya ugonjwa wa Fistula lakini pia huduma ya uzazi kwa wanawake wenye hali duni kiuchumi bure kuanzia malazi, chakula na usafiri kufuata tiba wanapotoka nyumbani au mikoani,” amesema Doreen.
Amesema kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya wagonjwa wapya 3,000 wa fistula kila mwaka, huku zaidi ya wagonjwa 15,000 hawaripotiwi.
“Kati yao ni wanawake 1,300 pekee ndio wanapata matibabu kila mwaka, ndio maana tumeandaa mbio hizi ili kuhakikisha kila mwanamke aliyeathirika na fistula anapata matibabu kwa wakati,” amesema.
Amesema fedha zitakazokusanywa kupitia tukio hilo zitaelekezwa moja kwa moja kwa ajili ya kugharamia upasuaji bila malipo, matibabu, usafiri, na malazi kwa wagonjwa wa fistula katika Kituo cha Uzazi cha Kivulini kilichopo Ngaramtoni, Arusha.
Amesema mbio zitafanyika kwenye Viwanja vya Magereza, kuelekea Barabara ya Mzunguko ya Afrika Mashariki (East Africa Bypass) hadi Azimio na Majengo, na kurejea kupitia Barabara ya Arusha-Makuyuni.
Mabalozi wa mbio hizo, akiwemo nyota wa kimataifa wa riadha Failuna Abdi Matanga, ametoa wito kwa wanariadha wenzake na wananchi kwa ujumla kushiriki mbio hizo kama sehemu ya kutoa sadaka yao kwa wanawake wanaopitia changamoto ya ugonjwa wa fistula.
“Hii ni zaidi ya mbio, tunaweza kusema ni harakati ya kurejesha utu na afya kwa wanawake katika jamii zetu wanapokumbana na shida hii katika kipindi cha kujifungua,” amesema Failuna.
Takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) zinaonyesha zaidi ya wanawake 20,000 nchini Tanzania wanaishi na fistula ya uzazi kwa sasa.
Naye mwanariadha Angelina John amesisitiza ingawa hali hii inatibika kupitia upasuaji, maelfu ya wanawake bado wanaendelea kuteseka kimya kimya kutokana na ukosefu wa huduma hiyo.
“Tushiriki katika mbio hizi ili kuongeza uelewa na kuhakikisha kila mwanamke aliyeathirika anapata matibabu kwa wakati.
“Nimeamua kuwa balozi kwa sababu Marathon ya Fistula haihusu tu kuchangisha fedha bali ni jukwaa lenye nguvu la kuongeza uelewa, kupunguza unyanyapaa, na kutetea huduma bora za afya ya uzazi kote nchini,” amesema Angelina.