Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mo Dewji aweka kitita mezani Simba ikifuzu nusu fainali CAF

Muktasari:

  • Simba ili ifuzu, inatakiwa kufunga mabao matatu kwenye mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikitakiwa kutoruhusu bao lolote kwenye wavu wao ili wavuke kigingi cha kupoteza kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa ugenini.

MATAJIRI wa Simba wamewaachia wachezaji wao kuamua kuwapeleka Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kukutana na kufanya uamuzi ambao Bilionea, Mohammed Dewji MO ameweka mezani mzigo wa maana.

Simba ili ifuzu, inatakiwa kufunga mabao matatu kwenye mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikitakiwa kutoruhusu bao lolote kwenye wavu wao ili wavuke kigingi cha kupoteza kwa mabao 2-0 kwenye mchezo wa ugenini.

MO Dewji amewatumia salamu wachezaji wa timu hiyo akitaka waambiwe kwamba kama watapambana kuhakikisha Simba inafuzu nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuiondosha Al Masry, basi watavuna Sh500 milioni.

Mapema inaelezwa MO Dewji alipanga kuwapa Sh400 milioni endapo wachezaji hao wangefanikisha kufuzu lakini baada ya matokeo ya kupoteza mchezo wa kwanza uliopigwa kule Misri jamaa akaongeza Sh100 milioni na kufikia Sh500 milioni.

Ahadi hiyo itakuwa ni mzuka mkubwa kwa wachezaji wa Simba ambao mapema walishakaa kikao kabla ya kuanza safari ya kurudi nchini wakitokea Misri, wakitaka kujirekebisha kwa kutumia nafasi watakazotengeneza.

“Tunajua tuna uwezo wa kuwaondoa hawa Waarabu kitu kinachohitajika ni hamasa kwa wachezaji wetu, na tajiri amefanya kitu cha kufuru sidhani kama kuna bonasi kubwa kama hii wamewahi kuipata kwa miaka ya karibuni,” alisema bosi huyo wa juu wa Simba na kuongeza:

“Tumekutana na tajiri (MO) na ametuambia tukawaambie wachezaji kwamba kama wanataka kufurahi basi washinde na Simba ifuzu hiyo fedha itaingia kwao haraka, hakuna masihara.”


DAWA YA UCHOYO WA PASI

Mbali na bonasi hiyo ya kufuru, Mwanaspoti linafahamu kuwa kutakuwa na mpango mwingine wa kukomesha ishu ya wachezaji kunyimana pasi za mabao kwani kila asisti na bao imewekewa dau la kufanana, hivyo mtoa pasi na mfungaji watapata mgawao sawa.

Simba ikiwa Misri kwenye mchezo wa kwanza mastaa wa timu hiyo walikosolewa kwa kutorahisishiana kazi wakionyesha kutanguliza sifa binafsi badala ya kucheza kitimu hatua ambayo matajiri hao wanataka isitokee Jumatano ambayo inaweza kuwakwamisha.

“Tunataka kuhakikisha hakuna kunyimana pasi tena, siku ile hili nalo lilitukwamisha, kuna wakubwa wanataka kutoa kila goli kiasi kisichopungua Sh2.5 milioni lakini pia aliyetoa asisti naye anapata kiasi kama hicho ili kila mmoja ashiriki kutengeneza ushindi ambao tunautaka.

“Kama dau lingewekwa kwa mfungaji pekee, basi kila mchezaji angekuwa akitamani kufunga hali ambayo ingeendeleza ile tabia ya kunyimana pasi lakini kwa hili itakuwa rahisi kupasiana kwani mfungaji na mtoa pasi wote watapata mgao sawa wa kuchangia bao,” alimaliza bosi huyo.

Wakati mikakati hiyo ikiendelea kwa Simba, tayari Al Masry wapo nchini kwa ajili ya mchezo huo uliopangwa kuanza saa 10:00 jioni huku ikitarajiwa kumkosa mshambuliaji aliyefunga bao la pili, John Ebuka kutokana na kusumbuliwa na misuli ya paja.

Mbali na kumkosa mshambuliaji huyo, Kocha wa Al Masry, Anis Boujelbene ameonekana kupata wasiwasi kuelekea mchezo huo kutokana na kile alichodai hawakuwa na muda mwingi wa kujiandaa kwani Jumamosi walilazimika kucheza mechi ya Kombe la Misri dhidi ya Ceramica Cleopatra na kupata sare ya 1-1, kisha Jumapili wakatua Dar.

“Nawapongeza mashabiki wa Al Masry kwa kuwa sehemu ya mchango wa ushindi mechi ya kwanza lakini bado hatujafuzu. Mechi ya kwanza ilikuwa ngumu sana dhidi ya mpinzani hodari, tulifanya bidii kubwa wakati wa mchezo.

“Lakini sasa mchezo wa marudiano una mambo mengine na tunatakiwa kukabiliana nayo. Nina wasiwasi sana kwa sababu tulicheza mechi dhidi ya Ceramica Cleopatra kwenye michuano ya Kombe la Misri siku mbili tu kutoka kucheza dhidi ya Simba,” alisema Boujelbene.

Simba ina mtihani wa kuhakikisha inafuzu nusu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kushindwa kufanya hivyo mara tano zilizopita walipocheza robo fainali.

Wekundu hao waliobaki pekee kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa msimu huu, wana rekodi ya kucheza robo fainali sita za CAF katika misimu saba kuanzia 2018-2019, huku tano zilizopita ikishindwa kuvuka na sasa kuwa kwenye mtego mkubwa.

Katika harakati za kuondoa rekodi hiyo mbovu, tayari Simba imepoteza mchezo wa ugenini kwa mabao 2-0, hivyo lazima ipambane kuhakikisha wapinzani wao hawapati bao watakaporudiana Jumatano hii huku wao wakitakiwa kushinda 3-0 ili kuweka rekodi mpya.

Mbali na fedha hizo walizowekewa na mabosi wao, pia kwa kila bao la ushindi ambalo Simba itafunga itakuwa na thamani ya Sh5 milioni kufuatia kampeni ya Bao la Mama inayotolewa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo ya CAF.

Pia kuna fedha kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambapo timu zitakazofuzu nusu fainali zitakuwa na uhakika wa kupata dola 750,000 (Sh2 bilioni), lakini kama Simba itaishia robo fainali, itapewa dola 550,000 (Sh1.5 bilioni).