Wanasubili nini Bongo Hawa

Muktasari:
Wachezaji hawa kutokana na uwezo wao, wana kila sababu ya kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi
WACHEZAJI wa Kitanzania hivi sasa wanaondoka na kwenda kujaribu soka la kulipwa nje ya nchi, hii ni baada ya kuona kwamba nje kuna fursa kubwa zaidi ya hapa Tanzania.
Zamani wachezaji wengi walikuwa wakitoka lakini baada ya muda mfupi walikuwa wanarejea nchini tena na kujiunga katika klabu za Kariakoo na kuendelea na maisha mengine kama kawaida.
Leo hii tumeona kwamba wachezaji wengi wameanza kuamka baada ya kumuona mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samatta aking’ara barani ulaya na kuanza kuingia katika rada ya baadhi ya klabu nchini Uingereza.
Licha ya kwamba njia zimeanza kufunguka kwa wachezaji kutoka kwa wingi kama tulivyoona kwa Himid Mao kwenda Misri katika klabu ya Petrojet, alianza kuonyesha nia mapema ya kutaka kutoka baada ya kufanya majaribio katika klabu mbalimbali barani Ulaya, huku Abdi Banda akiondoka kwenda Afrika Kusini (Baroka Fc) na Simon Msuva (Al Jadida, Morocco) na Hassan Kessy (Nkana Fc, Zambia).
Kutoka kwa wachezaji hawa kumelifanya Taifa kujiamini pindi timu ya Taifa inapokuwa inacheza mchezo wowote kutokana na kwamba wana kikosi chenye wachezaji ambao wameshapata uzoefu wa nje ya Tanzania.
Mwanaspoti limewaangalia wachezaji wengine ambao ni kama wanachelewa wanapokuwa wanaendelea kukipiga ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na uwezo wao walionao.
IBRAHIM AJIB
Uwezo wake alionao wadau wengi wa soka walikuwa wanajua kwamba mchezaji huyu aliyeibukia Simba, hatokuwa na muda mrefu ndani ya kikosi hicho.
Alikuwa mchezaji pendwa ndani ya Simba, uwezo wake wa kuchezea mpira ulikuwa ukiwavutia mashabiki wa klabu hiyo na wengi walitegemea kuona kwamba ataondoka nchini atakapomaliza mkataba wake lakini ghafla alitua Yanga na kufanya watu wengi wabaki midomo wazi.
Akiwa ndani ya Yanga juzi tu amefunga goli la aina yake katika mchezo dhidi ya Mbao, goli ambalo liliamsha hisia za mashabiki na kuanza kujiuliza anasubili nini hapa bongo.
Kumuuza Ajib hivi sasa ni rahisi mno kwasababu tayari yupo katika fomu ya kiwango cha juu, lakini anatakiwa afanye maamuzi sahihi ya kuondoka lakini vile vile pia watu sahihi waibuke na kusaidia vijana wenye vipaji kama hawa.
BENO KAKOLANYA
Hakuna jina linalotajwa hivi sasa nchini kama hili. Uwezo wake aliouonyesha katika pambano la watani wa jadi liliwafanya mashabiki wa klabu zote mbili waliimbe jina lake.
Kakolanya katika msimu uliopita alikuwa akisumbuliwa na majeraha, wengi waliona kama alifulia lakini kipa huyo alikuja kuonyesha maajabu baada ya kwenda Mbeya kwenye mchezo dhidi ya Prison na alicheza kwa kiwango cha juu licha ya kuwa na majeraha.
Huu ndio muda sahihi kwake kutafuta soko nje ya nchi huku kuitwa kwake katika timu ya Taifa kumezidi kumuongezea soko kwani inakuwa rahisi kwake kupata timu.
Wadau na wapenzi wa soka pamoja wanatakiwa kumpa moyo kipa huyu kijana ambaye ndio kwanza ameanza kula matunda yake tangu asajiliwe na kikosi hicho.
MUDATHIR YAHYA
Ni kati ya viungo ambao wamekuwa katika kiwango kikubwa katika Ligi Kuu Bara. Mudathir baada ya kuondoka katika klabu ya Azam kwa mkopo na kwenda Singida United alifungua macho ya mashabiki wengi wa soka.
Azam ilibidi wahakikishe wanambakiza mchezaji huyo na walifanikiwa kutokana na kumuongezea mkataba na kuwa nae, lakini hata hivyo akajikuta anafanya vizuri akiwa na kikosi chake cha timu ya Taifa, Zanzibar Heroes.
Huu ndio muda sahihi wa Mudathir kufanya maamuzi ya maisha katika soka lake kutokana na kwamba yupo moto, lakini vile vile Azam wanatakiwa wasiingie tamaa ya pesa na kuweka vizuizi.
AISH MANULA
Hakuna ubishi kwamba huyu ndiye Tanzania One hivi sasa kutokana na kuwa panga pangua katika kikosi cha timu ya Taifa. Uwezo wake tangu akiwa Azam ndio ulifanya Mabosi wa Simba kuweza kuvunja kibubu na kumsajili katika kikosi chao.
Manula tangu ajiunge Simba amekuwa kipa namba moja akiwapa changamoto Said Nduda pamoja na Emmanuel mseja ambaye ameondolewa katika kikosi hicho, hata alivyokuja Deogratius Munish bado Manula ameonyesha ukomavu.
Akimaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu anabidi afikilie kutafuta timu ya kucheza nje ya nchi, kwasababu kama akiendelea kuzunguka katika klabu za hapa hapa nchini sifa yake inaweza kupotea kama ambavyo ilivyokuwa kwa makipa wenzie.
HABIB KYOMBO
Alikuwa ndio mfungaji bora katika mashindano ya kombe la Fa msimu uliopita, uwezo wake msimu uliopita ulifanya klabu mbalimbali zivutiwe na huduma yake ikiwemo Simba.
Hata hivyo aliamua kumwaga wino katika kikosi cha Singida, tangu amejiunga katika kikosi hicho amekuwa mchezaji ambaye yupo katika kiwango kikubwa, hali ambayo ilifanya atoke aende Mamelod Sundowns kwenye majaribio.
Majibu yake bado imekuwa sintofahamu lakini kama kweli amefuzu kama ambavyo inadaiwa basi ndio muda sahihi wa yeye kuondoka na kwenda kutafuta maisha nje ya nchi.
Umri wake ni sahihi kwake kutoka kwenda kutafuta maisha ya soka la kulipwa nje ya nchi, kwani ni mchezaji ambaye katika upande wa ushambuliaji amekamilika.
Thomas Jerome
[email protected]