Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wasifu wa CEO mpya Simba huu hapa…

Ikiwa siku 27 tangu klabu ya Simba ilipoachwa solemba na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wake, Senzo Mazingisa aliyejiuzulu ghafla na kukimbilia Yanga, klabu hiyo imemtangaza Barbara Gonzalez kushika nafasi hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohamed ‘MO’ Dewji amuelezea kiongozi huyo kama jembe jipya na lenye uwezo mkubwa wa kuiletea maendeleo Simba.

Barbara Gonzalez, amezaliwa jijini Dar es Salaam miaka kadhaa iliyopita, baba yake akiwa ni raia wa Colombia na Mama Mtanzania, mbali kuwa msaidizi wa Mohamed Dewji, pia ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mohamed Foundation aliyojiunga nayo Aprili, 2016 ambayo imekuwa ikitoa msaada wa huduma za kijamii kwa makundi mbalimbali nchini.

Pia anahudumu katika Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Young African Leaders Initiative (YALI) iliyo chini ya Rais wa zamani wa Marekani, Barrack Obama ambayo lengo lake kuu ni kuwekeza katika viongozi wa kizazi cha baadaye barani Afrika.

Mbali na wadhifa huo, Barbara pia ni mshauri wa taasisi ya Deloitte Consulting Limited Tanzania na pamoja na hilo, amefanya kazi katika miradi kadhaa iliyo chini ya mashirika makubwa duniani miongoni mwao yakiwa ni USAID, UNICEF, Benki ya Dunia na Plan International.

Mwanadada huyo ana uzoefu wa kutosha na ni mbobezi wa masuala ya utawala na uongozi akiwa na Shahada ya Uzamili ya Utawala na Maendeleo aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Uchumi na Sayansi ya Siasa kilichopo London, England.

Alipata shahada yake ya kwanza aliipata katika Chuo Kikuu cha Manhattanville College kilichopo New York, Marekani ambako alihitimu kwa ufaulu wa juu katika Sayansi ya Siasa na Uchumi.

Muda mfupi baada ya uteuzi wake mashabiki wa Simba walikuwa wakiwatambia wenzao wa Yanga kwenye mitandao ya kijamii wakidai kwamba huyo ndiye kiboko yao huku wengine wakiwakejeli kwamba “njooni mumchukue na huyu.”

Barbara anakuwa mwanamke wa kwanza nchini kushika wadhifa huo katika soka la Tanzania, baada ya Simba kumtangaza rasmi jana kutokana na maamuzi ya kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo iliyokutana juzi Ijumaa.

Dewji alisema Barbara ambaye pia amekuwa Mjumbe wa Bodi hiyo, ndiye atakayeshika nafasi hiyo iliyoachwa na Senzo na wanamwamini kutokana na uwezo wake wa kiutendaji.

“Napenda kutumia fursa hii kumtambulisha kwenu, Mtendaji Mkuu mpya aliyeteuliwa na klabu ya Simba ambaye ni Barbara Gonzalez. Bodi ya Wakurugenzi ya Simba inaomba mumpatie ushirikiano na tunaamini ataifanya klabu yetu ipige hatua,” alisema Mo Dewji.

Mwanadada huyo ana kazi kubwa ya kuhakikisha anaanzia pale alipoishia mtangulizi wake ili kuipeleka Simba mbele, licha ya ukweli ana uzoefu mkubwa ndani ya klabu hiyo iliyoasisiwa mwaka 1936 ikiwa na mataji 21 ya Ligi Kuu Bara.