Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yaliyojificha sakata la kipa Fountain Gate

Muktasari:

  • Muda mfupi baada ya Fountain Gate kupoteza mchezo dhidi ya Yanga kwa mabao 4-0 juzi Jumatatu kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uongozi wa timu hiyo uliamua kumsimamisha Noble ambaye hivi sasa amesharejea kwa Nigeria akingojea uamuzi dhidi yake.

Nyuma ya adhabu ya kusimamishwa kwa kipa John Noble wa Fountain Gate kuna sababu mbili kubwa ambazo zimefanya timu hiyo ambayo inatumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati, Manyara kuchukua uamuzi huo.

Muda mfupi baada ya Fountain Gate kupoteza mchezo dhidi ya Yanga kwa mabao 4-0 juzi Jumatatu kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uongozi wa timu hiyo uliamua kumsimamisha Noble ambaye hivi sasa amesharejea kwa Nigeria akingojea uamuzi dhidi yake.

“Ni kweli uongozi wa Fountain Gate umemsimamisha kipa John Noble kwa ajili ya kupisha uchunguzi dhidi yake. Uamuzi huo umechukuliwa kwa ajili ya usalama wa mchezaji mwenyewe maana baada ya mchezo watu wengi walionyesha kutofurahishwa naye,” alisema ofisa habari wa timu hiyo.

Katika mchezo huo, Noble aliruhusu mabao mawili ya kizembe ambayo ni la kwanza na la pili jambo lililopelekea benchi la ufundi kumfanyia mabadiliko mara baada ya kufungwa bao la pili.

Kosa la kwanza alifanya katika dakika ya 38 alipopangua vibaya mpira wa faulo wa Aziz Ki Stephane ambao ulimkuta Clement Mzize aliyeukwamisha wavuni.

Dakika ya 43, Noble alifanya kosa lingine la kupiga pasi mkaa kwa Aziz Ki ambayo ilitumiwa vyema na nyota huyo wa Burkina Faso kuipatia Yanga bao la pili, matokeo ambayo yalibaki hivyo hadi filimbi ya mapumziko ilipopulizwa.


Mbili zilizomponza

Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili umebaini mambo mawili yaliyochangia kuifanya Fountain Gate kuchukua uamuzi huo.

Jambo la kwanza ni muendelezo wa makosa ambayo amekuwa akiufanya kipa huyo katika mechi za timu hiyo.

“Huyu kipa kuna asichokifahamu ni kwamba kuna watu wetu maalum ambao wamekuwa wakifuatilia mienendo ya wachezaji wetu ndani na nje ya uwanja. Sio kipa mbaya kwa maana ya uwezo lakini kuna nyakati amekuwa akifanya uzembe ambao unaigharimu timu na haonyeshi kujutia wala kubadilika,” kilifichua chanzo cha uhakika ndani ya Fountain Gate.

Ushahidi wa hilo unaweza kuthibitishwa na kauli ya kocha Robert Matano ambaye baada ya mchezo dhidi ya Yanga, alimtuhumu Noble kuwa ameifungisha timu yake.

“Magoli ya leo (juzi) ni ya kupeana, Golikipa ametutoa kwenye mchezo, huwezi ukafanya makosa kama yale halafu utegemee timu kurudi mchezoni. Kwa makosa yale hata Yanga wenyewe wasingerudi mchezoni, Golikipa ametuangusha,” alisema Matano.

Historia inakumbusha kuwa Tabora United ambayo Noble aliwahi kuichezea msimu uliopita, iliamua kutoendelea na mkataba na kipa huyo mara baada ya kufanya uzembe ulioipa bao JKT Tanzania katika mechi ya mchujo wa kuwania kubaki Ligi Kuu baada ya Noble kusababisha penalti iliyoizawadia JKT Tanzania bao la kusawazisha.

Kipa huyo alidaka mpira na kisha akauachia ukawahiwa na Ismail Aziz wa JKT Tanzania na mara baada ya mchezaji huyo kuumiliki, Noble alimchezea faulo iliyosababisha penalti iliyopigwa na Ndemla na kipa huyo kuicheza kisha mpira ukamfikia Martin Kiggi aliyeujaza wavuni.

Sababu ya pili ni mahusiano yasiyo mazuri baina ya kipa huyo na benchi la ufundi tangu mchezo dhidi ya Simba uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 ambao alionyeshwa kadi nyekundu kwa kupoteza muda.

Wakati anatoka nje ya uwanja, kipa huyo hakupeana mkono na Matano na baada ya hapo kocha huyo alisema kuwa kipa alifanya kosa la kizembe.

“Kipa alifanya mambo ya kitoto. Wewe umeshapewa kadi ya njano bado unapoteza muda na tumeshamaliza idadi ya wachezaji wa kuingia. Sipendelei mimi kama kocha hivyo sikufurahi kama kocha,” alisema Matano.


Takukuru waingia kazini

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Manyara, Bahati Haule, amesema wameanza rasmi kuchunguza tuhuma za Noble kuona kama kuna viashiria vya rushwa.

“Ni kweli hata sisi tumesikia kuwa magoli aliyofungwa huyo kipa yalikuwa na utata kwamba bao la kwanza alipigiwa shuti dogo akatema mpira kwa uzembe na goli la pili alirudisha mpira golini.

 “Sheria hiyo (ya Takukuru kifungu cha 15 kilichofanyiwa marekebisho na kupitishwa na Bunge mwaka 2024) imeongezewa suala la kuwa rushwa ya uchaguzi, rushwa michezoni, kamari na michezo ya kubahatisha na mambo ya burudani,” amesema Haule.


Makipa wafunguka

Kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda, alisema makosa ya Noble ni ya kizembe.

“Nikizungumzia kiwango katika mchezo huo kilikuwa chini, hali hiyo inamshushia heshima kama kipa wa kigeni ambaye anatakiwa afanye zaidi ya kile kinachotakiwa kufanywa na wazawa ndiyo maana mashabiki wamekuwa na wasiwasi naye ingawa kiufundi nikiwa kama kocha naona ni makosa ya kizembe.

“Mfano bao la pili baada ya kutoka ndani ya 18 alipaswa aupige mpira mrefu, sasa akawa anataka apige chenga alirudi nao ndani, wakati anafahamu anacheza na Yanga iliyo na washambuliaji hatari, mechi kubwa za Simba na Yanga ndizo alitakiwa aonyeshe ukubwa wake na ukomavu wa kuibeba timu,” alisema Mapunda.

Kipa na kocha zamani wa makipa Simba, Idd Pazi alisema: “Mara nyingi nasema sifa za kipa wa kigeni lazima awe na kiwango bora zaidi ya wazawa, mfano bao la pili kulikuwa na haja gani ya kupiga chenga wakati anajua Yanga ina washambuliaji hatari kama siyo kuwataka maneno ya watu kumshambulia?” alihoji Pazi.